RAIS Jakaya Kikwete ameagiza kuimarishwa kwa udhibiti katika viwanja vya
Ndege vya Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (Kia), kutumiwa
kupitisha dawa za kulevya kwenda nje na kuingia nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la
tatu la abiria JNIA, Dar es Salaam Rais Kikwete alisema hajaridhishwa na
kasi ya udhibiti wa dawa za kulevya katika viwanja hivyo.
Alisema inashangaza dawa za kulevya zinapita katika viwanja hivyo na
watendaji wote wapo na zinakwenda kukamatiwa Afrika Kusini.“Sijaridhishwa, unasikia kila siku mtu amekamatwa Afrika Kusini
na dawa za
kulevya, sijui mwanamuziki gani, siridhishwi hata kidogo,” alisema.
Rais Kikwete alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi
Suleiman Suleiman kuhakikisha mianya hiyo inazibwa vinginevyo ataanza
kumwadabisha yeye kisha wengine watafuata... “Nitaanza na wewe mkurugenzi na
mwenyekiti wako wa bodi. Mtu anakuja hapa, sijui mwanamuziki gani, mara
yoo...yoo... kwa kuwa mnamfahamu anapita, hatuwezi kuwa namna hiyo.”
Aliagiza apewe orodha ya majina ya maofisa wanaodhaniwa kujishughulisha na
biashara hiyo naye atawaondoa kwa kuwa sheria inamruhusu... “Rais hashtakiwi,
nitawaondoa, nipeni majina kwa kuwa kinachotokea hivi sasa kinaonyesha wote
tunafanya biashara ya dawa za kulevya, wengine inatuumiza sana tunaonekana wote
ndicho tunachofanya.”
Alibainisha kuwa haingii akilini kusikia kuna kitu kinakwamisha udhibiti wa
dawa hizo katika viwanja hivyo ikiwamo Sheria ya Ununuzi wa Umma... “Miaka
miwili hiyo sheria gani kwa kitu cha Sh2.5 milioni... je, ingekuwa Sh600
milioni si ndiyo kungegeuzwa gulio?” alihoji.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alifafanua baadaye kuwa Rais
alikuwa anazungumzia kuchelewa kufungwa kwa mfumo wa kubaini dawa za kulevya
uwanjani hapo, kutokana na mchakato mrefu wa sheria hiyo.
Jengo la abiria
Rais Kikwete alisema atahakikisha Hazina inatoa fedha zinazotakiwa
kuharakisha ujenzi wa jengo hilo la abiria ambalo litakuwa na maegesho ya ndege
18 kwa wakati mmoja, litakalohudumia abiria milioni sita kwa mwaka badala ya
milioni 2.5 wa sasa.
Mradi huo ambao unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa ya BAM ya
Uholanzi, utagharimu Sh518 bilioni na Serikali iliahidi kutoa asilimia 50 ya
fedha hizo sawa na Sh89 bilioni huku kiasi kingine kikitolewa na Serikali ya
Uholanzi.
Hata hivyo, hadi sasa fedha hizo hazijatolewa jambo ambalo liliwahi
kulalamikiwa na Mkurugenzi wa TAA kwamba linakwamisha ujenzi huo. Jengo hilo
litakuwa na mifumo yote ya mawasiliano, usalama na uendeshaji na maegesho yenye
uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote, zikiwamo Airbus 380.
Awali, Suleiman alisema uwanja huo utakamilika kwa wakati kutegemeana na
upatikanaji wa fedha na hivyo kuondoa msongamano wa abiria katika uwanja wa
sasa (Terminal II) ambao licha ya kuhudumia milioni 2.5, uwezo wake ni
kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Kabla ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi huo, aliweka jiwe la msingi katika
ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
katika eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo hilo, Rais Kikwete aliagiza Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha inatayarisha haraka iwezekavyo ramani ya ujenzi
wa kituo hicho cha mafunzo kwa madaktari kinachotarajiwa kuwa kikubwa zaidi kwa
Afrika Mashariki na Kati.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

No comments:
Post a Comment