WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid amesema maduka ya dawa yatakayobainika kuuza dawa za malaria zilizokwisha muda yatafungiwa na kunyang’anywa leseni ya biashara.
Akizungumza katika mkutano wa kujadili malaria na mikakati yake
uliofanyika katika maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani, Dk Rashid alisema uuzaji wa dawa zilizokwisha muda na zilizopigwa marufuku kama tiba ya malaria, ndicho chanzo cha kuzorota kwa vita dhidi ya ugonjwa huo
.
“Mmiliki wa duka ambaye kwa kawaida ni Mfamasia atanyang’anywa cheti na hatoweza kufanya tena biashara hiyo na duka hilo litafungiwa. Haya ndiyo mambo ambayo tunayafanyia kazi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha dawa za malaria zinatolewa kwa usahihi,” alisema Dk Rashid.
Akifafanua kuhusu matumizi ya dawa za malaria aina ya SP, Waziri alisema maduka ya dawa yanayouza dawa aina ya SP (metacelfin) kama tiba wanafanya makosa kwani dawa hizo ni kwa ajili ya kinga ya malaria kwa wajawazito tu na si tiba.
Alisema dawa mseto au Alu ndiyo dawa sahihi kwa ajili ya tiba ya malaria na imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Katika mkutano huo Dk Rashid pia alisema maambukizi ya malaria yameshuka kwa asilimia 50 na hivyo kuifanya Tanzania kufikia lengo la millennia namba nne.
Alisema kwa sasa wagonjwa wengi wanaofika katika vituo vya afya wanagundulika kuwa na homa lakini si malaria, jambo ambalo alisema linahitaji kufanyiwa kazi.
“Malaria husababisha vifo, hali duni na kuzorotesha shughuli za kiuchumi hivyo ni vyema kuwekeza zaidi katika rasilimali fedha na watu katika vita hii,” alisema.
Dk Rashid alisema bado wizara inaendelea kufanyia kazi changamoto za ubora wa dawa, usugu na viwatilifu ili kupata ufumbuzi kamili wa maambukizi ya malaria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, (IHI) Dk Salim Mshinda alisema taasisi hiyo bado inaendelea kufanya utafiti wa kina kuhakikisha tiba, chanjo na vyanzo vyote vya maradhi ya malaria vinapatiwa ufumbuzi na hatimaye ugonjwa huo kutokomezwa.
Dk Mshinda alisema kwa sasa IHI inaendelea kuangalia namna ya kutafuta kinga dhidi ya mbu waenezao malaria kabla ya usiku wa manane baada ya utafiti kuonyesha kuwa mbu wamebadili tabia.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

No comments:
Post a Comment