Saturday, May 31, 2014

Chanjo ya malaria kufanyakazi kwa asilimia 100


WAKATI vifo zaidi ya 700,000 vitokanavyo na Malaria vikitokea ukanda wa Jangwa la Sahara kila mwaka wanasayansi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) wakishirikiana na kampuni ya Marekani wameanza majaribio ya chanjo mpya inayotarajiwa kuzuia malaria kwa asilimia 100.
Awali majaribio ya chanjo hiyo iitwayo Sanaria PfSPZ yalifanyika Marekani na kudaiwa kuwa watu sita wasiougua malaria walijaribiwa na ilifanikiwa kwa asilimia 100 baada ya wote kutoambukizwa ugonjwa huo.

Watu hao sita kutoka Marekani walifanyiwa majaribio kwa kupewa chanjo hiyo kisha kuwekewa vimelea vya malaria na kundi jingine hawakupewa chanjo na kuwekewa vimelea vya ugonjwa huo na matokeo yalionyesha wale ambao hawakupata chanjo walipata malaria.
Mkurugenzi Mtendaji wa IHI, Dk Salim Abdulla alisema endapo majaribio ya chanjo hiyo yatafanikiwa basi hiyo itakuwa ni hatua ya mafanikio kuelekea kupata chanjo inayoweza kutoa kinga kamili dhidi ya vimelea vya malaria.
Mwanzilishi na Mwanasayansi Mkuu wa Kampuni ya Sanaria inayotengeza chanjo hiyo, Dk Stepehen Hoffman alisema ingawa majaribio hayo yapo katika hatua za awali za utafiti matokeo yakiwa mazuri itatumika kutokomeza malaria duniani.
Mtafiti Mkuu wa chanjo hiyo, Dk Seif Shekalage wa IHI alisema katika kulinganisha utafiti uliofanyika Marekani, IHI ilitumia vijana wa Kitanzania 96 kutoka vyuo vikuu vya nchini nia ikiwa ni kuangalia ubora wa chanjo hiyo.
CHANZO GAZETI LA  MWANANCHI



No comments:

Post a Comment