Thursday, June 5, 2014

Wajawazito wanachanganywa na wagonjwa wa kawaida

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Likuyu Said Rupia
Na Albano Midelo
WANAWAKE wajawazito katika kijiji cha Likuyuseka wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanadai wanadhalilishwa kupata huduma ya uzazi katika zahanati ya kijiji hicho ambayo haina chumba maalum cha kujifungulia.

Kijiji cha Likuyuseka kipo mpakani na mradi wa mgodi wa uchimbaji wa madini ya urani uliopo ndani ya
pori la akiba la Selous ambalo lilitangazwa na shirika la umoja wa mataifa la UNESCO mwaka 1980 kuwa eneo hilo ni urithi wa Dunia.
Wakizungumza  na mwandishi wa makala hayo akinamama hao walisema zahanati hiyo Haina chumba maalum kwa ajili ya kujifungulia hali ambayo imesababisha  chumba cha kujifungulia  wajawazito kuwa mkabala na chumba cha wagonjwa wa kawaida hali ambayo  inawadhalilisha wanawake wanaojifungua.
“Kila kitu ambacho kinafanywa na muuguzi wakati anamsaidia mama mjamzito kujifungua,wagonjwa wengine wanasikia,hali hii inatudharirisha sisi wanawake,ilitakiwa ijengwe chumba maalum kwa  ajili ya wazazi kujifungulia,wanawake wengine wanaona aibu hawafiki hapa kujifungulia,wanajifungulia kwa wakunga wa jadi na kuhatarisha maisha yao’’,alisema Fatuma Rajabu.
Hata hivyo hakuna utafiti ambao umefanyika kuzunguka katika vitongoji vya kijiji hicho ili kubaini idadi ya wanawake walioamua kujifungulia kwa wakunga wa jadi,lakini baadhi ya wanawake waliohojiwa wamedai kuwa kuna wanawake hawaendi kujifungulia katika zahanati hiyo kutokana na kuona aibu.
“Upande mmoja daktari anahudumia wagonjwa wa kawaida,upande wa pili muuguzi mkunga anaangaika kumuhudumia mama mjamzito, wagonjwa wengine wakiwepo watoto,vijana na wanaume wanasikia  kila kitu,ni aibu sana kwa mama anayejifungua ndiyo maana  wengine hawaendi kujifungulia hapo’’,alidai Mariam Rashid
Mwenyekiti wa kijiji cha Likuyuseka Athuman Rupia amekiri zahanati ya kijiji hicho kukosa chumba maalum kwa ajili ya kujifungulia akinamama wajawazito  hali ambayo imesababisha wajawazito kujifungulia sehemu ya chumba ambacho pia kinatoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa mengine.
“Akinamama wajawazito wanapata shida wakati wa kujifungua hali hiyo inaweza kuchangia kuongeza tatizo la uzazi usio salama kwa kuwa kuna taarifa kuwa baadhi yao hawafiki kujifungulia katika zahanati hiyo kwa sababu ya aibu,wagonjwa wengine wanawasikia unajua tena ndiyo maana kunakuwa na wodi ya wazazi’’,alisema.
Katika kukabiliana na hali hiyo mwenyekiti huyo wa serikali ya kijiji amesema mwaka huu kijiji kimefyatua tofali kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kujifungulia wajawazito ili  kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kulinda hadhi ya mwanamke ambaye ni nguzo ya familia katika jamii.
Kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho Maulid Kapolo alisema licha ya kuwepo changamoto ya kutokuwepo chumba cha wazazi, tatizo la vifo vya mama na mtoto lipo lakini sio kwa kiwango kikubwa kwa kuwa wataalamu wa afya daktari na wauguzi wapo  na madawa yanapatikana  katika zahanati hiyo ambayo inahudumia watu zaidi ya 7000 .
Wilaya  ya Namtumbo ina vituo 43 vya kutolea huduma za afya. Kati ya hivyo, vituo vya afya ni sita,vinne vya serikali na viwili vya shirika la dini, Zahanati 37 kati ya hizo zahanati 43 za serikali  na zahanati tatu za taasisi za dini tatu..
Taarifa ya idara ya afya ya Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo imeyataja malengo makuu ya uboreshaji wa huduma za afya kuwa ni kuongeza kiwango cha chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 90 hadi 95 ifikapo 2015.Pia kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano, vifo vya kinamama vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Katika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia hususani lengo la tano la kupunguza vifo vya wajawazito, takwimu za wizara ya afya zinaonyesha kuwa vifo vya wajawazito vimepungua kwa asilimia 21 kutoka vifo 578  kwa kila vizazi hai Laki Moja kati ya mwaka 2004/2005 hadi vifo 454 kwa kiwango hicho kati ya mwaka 2009/ 2010.
 Benedicto Ngaiza ni Mganga Mafawidhi  katika  hospitali ya rufaa mkoani Ruvuma anaeleza mikakati ya hospitali hiyo ni kuongeza juhudi katika kuisaidia Serikali ili kuzuia vifo vya wanawake ambavyo hutokea wakati wa kujifungua.
Alisema licha ya juhudi kufanywa na Serikali na wadau katika kupunguza vifo vya akinamana, bado takwimu zinaonyesha kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya. Na kwamba  inatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha wanawake wote wanajifungua salama bila kifo kutokea.
Alisema kuzinduliwa kwa dawa hiyo ni silaha nyingine katika mapambano ya kumkomboa mwanamke dhidi ya vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua.
 Wanawake 8,700 hufariki Dunia kila mwaka nchini Tanzania kutokana na matatizo ya ujauzito na hasa wakati wa kujifungua. Takwimu hizi zinaonesha takribani wanawake 24 hupoteza maisha kila siku huku ikikadiriwa mmoja kufa kila baada ya saa moja.
 Hata hivyo Sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza mipango madhubuti ya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana katika kila kata ambapo kila kijiji kinatakiwa kuwe na Zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya na wataalamu wenye taaluma.
Vingi kati ya vifo hivi vingeweza kuzuilika kama huduma za dharura zingekuwepo katika Vituo vya Tiba wakati wa kujifungua. Huduma zenyewe ni kama vile chumba cha upasuaji na wataalamu wake, vifaa tiba na uwezekano wa kuongezewa damu.
“Si sahihi mama mjamzito kufa wakati wa kujifungua au kupoteza uhai wake kwa kuleta kiumbe kingine duniani, hii haiwezi kukubalika. Na inasikitisha zaidi pale maisha ya mama huyu yanapotea hata kwa mambo ambayo yanaweza kuzuilika,” anasema Rais Kikwete katika hotuba yake mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki-moon.
Sera  ya afya inaeleza  wazi kuwa serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine yakiwemo mashirika mbalimbali itahakikisha inaboresha huduma za afya ili ziwe na mazingira mazuri na vifaa tiba. Hata hivyo sera hiyo inakwenda kinyume na hali halisi unapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya hasa vijijini mazingira sio rafiki.
Mazingira ya zahanati ya kijiji cha Likuyuseka yanafanana na mazingira mabovu ya kutolea huduma ya mama na mtoto katika baadhi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na hata hospitali za rufaa katika nchi nzima.
Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya afya ya uzazi ya Kitaifa wa serikali mwaka 2010 (TDHS) kila siku wajawazito 23 wanapoteza maisha kwa matatizo mbalimbali ya uzazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Serikali imeweka malengo ya Milenia  kufikia vifo 54 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2015,Utafiti umebaini licha ya malengo hayo ambayo yamebakiza miezi tu, wanawake 906 wamefariki dunia kwa matatizo ya uzazi mkoani Mbeya mwaka 2012.
 Baadhi ya sababu ambazo zinasababisha vifo vitokanavyo na uzazi kuwa ni pamoja na ugonjwa wa Malaria, damu kupungua kwa mama mjamzito, kutokwa kwa damu nyingi wakati wa kujifungua, uambukizi wa homa kali, huduma hafifu, VVU na kifafa cha Mimba.
Changamoto kubwa kwa serikali ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kutambua umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya afya na zahanati ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa kujifungua uzazi salama.
Huko nchini Uganda wanaharakati wa kutetea haki za wajawazito wanaitaka mahakama ya kikatiba itangaze kuwa mama kufariki akijifungua ni ukikwaji wa haki zake.
Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya nchini Uganda, takriban wanawake 16 hufariki kila siku wakijifungua, nchini Uganda. Kutokana na hali hiyo wanawake wakiongozwa na  wanaharakati 100 wa kutetea haki za akinamama wajawazito walifanya maandamano ya amani na kutembea kilomita tano kutoka ofisini kwao hadi kwenye mahakama ya katiba.
"Tunataitaka serikali itangaze kuwa akinamama wajawazito kufariki wakiwa hospitalini ni ukiukwaji wa haki zao za kuishi na afya bora. Pili, tuliwasilisha malalamiko yetu kwenye mahakama ya kikatiba miezi saba iliopita na kufikia sasa hatujapata jibu lolote. Tunaiomba  mahakama itoe msimamo kuhusu suala hilo’’,anasema Nakibuuka Nuru mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Uganda.
Wanaharakati wa kutetea haki za akinamama wajawazito wanaitaka serikali nchini Uganda kuwaajiri wakunga na madaktari wa kuwahudumia  wajawazito na kwamba kesi nyingi za wajawazito wanaofariki ni kwa sababu hawakupata usaidizi unaofaa kwa wakati unaofaa kutokana na takwimu kuonyesha kuwa mkunga mmoja nchini Uganda anahudumia hadi wajawazito 50 kwa siku..
Ingawa sheria  nchini Uganda kama vile Tanzania inasema mama mjamzito akienda kwenye hospitali ya serikali  anatakiwa kupata huduma za bure wakati wa kujifungua hali ni tofauti kwa kuwa akinamama hulazimishwa kununua vifaa vya kujifungulia kama vile pamba, wembe na vinginevyo.
Wakati hayo yanajiri nchini Uganda ,Takwimu za shirika la afya Duniani WHO, zinaonyesha kuwa idadi ya vifo vya kimamama vimepungua duniani kutoka nusu milioni mwaka 1980 hadi chini ya vifo 350,000 mwaka 2008.
 Kwa mujibu wa uchunguzi ulioshapishwa na jarida la The Lacent, idadi ya kinamama wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito imepungua kwa zaidi ya asilimia 35, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Nchi kama vile China, Misri, Ecuador na Bolivia zimefanikiwa kufikia malengo ya kimataifa ya kupunguza idadi ya wanawake wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito,
Hata hivyo nchi za Marekani na Norway zikiripotiwa kushuhudia ongezeko la vifo hivyo. Wengi wanasema kwamba, sababu kuu inayosababisha ongezeko la vifo hivyo katika nchi hizo mbili ambazo ni tajiri na zenye huduma bora ya tiba ni kuongezeka magonjwa miongoni mwa kinamama wajawazito pamoja na kinamama kubeba mimba katika umri mkubwa.




No comments:

Post a Comment