Na
Albano Midelo
WANAWAKE 280 katika kijiji cha Lundusi kata ya
Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma wanahitaji huduma ya kupimwa kwa hiari
virusi vya ukimwi ili kutambua afya zao.
Wanawake hao wametoa
ombi la kutaka kupimwa virusi vya UKIMWI
kwa hiari baada ya kupata elimu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yaliyoendeshwa na shirika la maendeleo ya
wanawake Ruvuma RUWODA.
Mafunzo hayo
yamefanyika kwa wiki moja katika vitongoji vya Ringa,Lundusi,Dodoma na
Kiburungi vilivyopo katika kijiji cha Lundusi chenye wakazi zaidi ya 2500
ambapo wananchi hao wameweza kujifunza mada mbalimbali zilizotolewa na Radbord Ngonyani ambaye ni mratibu wa shirika
la RUWODA.
Kulingana na mratibu
huyo wa RUWODA, mada ambazo zimefundishwa katika mafunzo hayo ambayo
yalishirikisha jumla ya watu 350 ni pamoja kuzuia maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto(PMTCI),ongezeko la vituo vya huduma na
wajibu wa jamii katika kuzuia maambukizi.
Mada nyingine ni
lishe kwa mtoto aliyeambukizwa virusi vya UKIMWI toka kwa mama kwenda mtoto,,uwezekano
wa mama mjamzito wa kumwambukiza mtoto,namna ya kuzuia maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na uwezo wa mama mjamzito kuzuia
maambukizi kwenda kwa mtoto.
Ngonyani amezitaja
mada nyingine ambazo zimefundishwa kuwa ni athari za kuishi na virusi vya
UKIMWI,mahitaji ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI,wajibu wa jamii katika
kuzuia virusi vya UKIMWI na UKIMWI,uaminifu katika mahusiano ya mapenzi na
mkakati wa kuhamasisha umuhimu elimu na faida ya kuzuia maambukizi ya virusi
vya UKIMWI na UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mratibu huyo wa
RUWODA amefurahishwa na wanawake wa kijiji cha Lundusi kuamua kwa hiari kutaka
kupimwa virusi vya UKIMWI ambapo ameahidi kuwasiliana na mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Songea ili kutoa wataalamu wa upimaji waweze kwenda
katika kijiji hicho kuwapima wanawake wanaotaka kupima kwa hiari.
“Wananchi
waliojitokeza kutaka kupimwa kwa hiari watasaidia serikali kupata takwimu
sahihi za maambukizi ya virusi vya UKIMWI na namna ya kuwasaidia watakaobainika
kuathirika,tatizo la ,maambukizi ya virusi vya UKIMWI bado kubwa katika wilaya
ya Songea’’,alisema.
Sera ya
afya Tanzania ya mwaka 2007 inatamka
wazi Serikali inafanya juhudi kubwa kukabiliana na janga la UKIMWI. Hata hivyo,
kutokuwepo mwitikio sahihi wa kukabiliana na janga la UKIMWI miongoni mwa
wananchi, kunaendelea kuathiri juhudi za kukabiliana na janga hili.
Kulingana
na sera hiyo, hali hiyo, inaendelea kuathiri nguvu kazi, kuongeza vifo, yatima,
umaskini na gharama za matibabu pamoja na kuathiri ustawi, uchumi na usalama wa
taifa.
Kudhibiti maambukizi na ya Virusi vya UKIMWI
nchini na kutoa matunzo na tiba ya kupunguza makali ya UKIMWI.Serikali
itaendelea kushirikiana na wadau katika kukabiliana na janga la UKIMWI katika nyanja zote zikiwemo,
kinga, huduma za tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya na majumbani, ili
kupunguza athari zinazosababishwa na VVU/UKIMWI.
Kulingana
na takwimu za UKIMWI kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Mkoa
wa Njombe, Mbeya Iringa na Ruvuma ni vinara wanaoongoza kwa maambukizi ya
Virusi vya Ukimwi nchini.
Njombe inaongoza kwa asilimia 14.8
ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu
kwa asilimia 9.
Mikoa
mingine na asilimia za maambukizi katika mabano ni Ruvuma (7.2), Shinyanga
(7.4), Dar es Salaam (6.9) Rukwa (6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9),Tabora (5.1),
Kagera (4.8) na Geita (4.7).
Kwa
mujibu wa takwimu hizo mkoa wa Mara
(4.5), Mwanza (4.2), Mtwara (4.1), Kilimanjaro (3.8), Kigoma (3.4), Simiyu
(3.6), Morogoro (3.8), Singida (3.3), Dodoma (2.9), Manyara (1.5), Lindi (2.9),
Tanga (2.4), Unguja (1.9) na Pemba (0.3).
Takwimu
hizo zinatokana na utafiti uliofanyika mwaka juzi hadi mwaka jana. Hata hivyo
kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzani maambukizi ya Ukimwi
yanapungua kwa kasi ndogo.
Hata hivyo shirika la Afya Ulimwenguni WHO limetoa takwimu zinazoonyesha
kuwa maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 50 katika nchi 13 za kusini mwa
jangwa la sahara ikiwemo Tanzania.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1999
inakadiriwa kuwa watu wazima na watoto milioni 33.6 walikuwa wanaishi na virusi
vya UKIMWI na watu milioni 16.3 walikuwa tayari wamefariki dunia katika nchi
zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara.
Pamoja na takwimu za shirika la afya
duniani kutoa matumaini makubwa kwa nchi za kusini mwa jangwa la sahara bado
nchi za Afrika mashariki zinawajibika kuongeza jitihada za kukabiliana na
maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI
hasa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja
kutoa huduma kwa watu wanaoishi
na virusi vya ukimwi.
Kwa maoni na ushauri
andika:albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment