Saturday, May 31, 2014

Sigara inauwa watu milioni sita



MIONGONI mwa athari za tumbaku ni saratani ya koo na mapafu, kuziba kwa mishipa midogo ya damu, kupungua nguvu za kiume, kuwa na ukurutu, saratani ya kizazi, mimba kuharibika, vidonda vya tumbo na matatizo ya kusikia.
Athari nyingine ni vidole, meno na mdomo kubadilika rangi, ngozi kukunjamana, matatizo ya mapafu, mifupa na moyo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa karibu watu milioni sita hufa duniani kila mwaka kutokana na athari za matumizi ya tumbaku.

Kati ya wanaokufa, 600,000 ni wale wanaovuta hewa iliyochanganyika na moshi wa sigara kutoka kwa mtumiaji.
WHO wametafiti na kubaini kuwa hadi ifikapo mwaka 2030, matumizi ya tumbaku yatasababisha vifo vya watu milioni nane kila mwaka. Asilimia 80 ya vifo hivyo vitatokea katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni mwao.
Hili ni janga jingine kwa taifa ambalo Serikali inapaswa kulichukulia kwa umuhimu wa kipekee, kuokoa afya za Watanzania ambao sehemu kubwa maisha yao ni magumu kutokana na kipato kidogo.
Tatizo kubwa hapa nchini ni kwamba watumiaji wa tumbaku hususan wavuta sigara hufanya hivyo hadharani.
Kuvuta hadharani, kwanza, kunawaathiri wasiovuta sigara na pili, kunahamasisha wengine hususan watoto kuona kuwa uvutaji ni sehemu ya ufahari na starehe.
Utafiti uliyofanywa mwaka 2008 na Global Youth Tobacco Survey (GYTS) ulibaini kuwa asilimia 10.6 ya wanafunzi nchini wanavuta sigara.
Hii inaashiria kuwa watumia tumbaku watazidi kuongezeka iwapo Serikali haitachukua hatua za haraka.
Inafahamika kuwa tayari Bunge lilipitisha sheria ya kukomesha uvutaji sigara hadharani.
Tatizo ni kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bado haijachukua hatua sahihi za kuweka kanuni hasa za kukataza uvutaji wa sigara hadharani.
Leo hii wavuta sigara wanafanya hivyo bila wasiwasi kwenye maeneo ya starehe, vituo vya daladala, mitaa yenye msongamano wa watu na hata ndani ya nyumba wanamoishi na familia zao.
Inawezekana kabisa Serikali inahofia kuweka kanuni zinazokataza uvutaji sigara hadharani kwa wasiwasi wa kukosa mapato kutoka kwenye kodi kubwa wanayokusanya kutoka kwenye viwanda vya sigara.
Kama asemavyo mkurugenzi wa WHO, Dk Margreth Chan, “kuongeza kodi ni njia bora zaidi ya kupunguza watumiaji wa tumbaku na kuokoa maisha ya watu wengi”.
Leo hii, kila baada ya sekunde sita, mtu mmoja hupoteza maisha kutokana na matumizi ya tumbaku.
Swali ni kwamba, je, Serikali iendelee kujivunia mapato makubwa kwenye tumbaku wakati wananchi wake wanateketea?
Serikali inapaswa kufahamu pale wananchi wake wanapoathirika kwa tumbaku, inatumia fedha nyingi hata kuliko ya zile walizokusanya kutoka kwenye biashara ya tumbaku ili kuwatibu waathirika.
Mfano mzuri ni utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2010 na kubaini kuwa Serikali ilitumia Sh6.4 trilioni kuwatibu wagonjwa wa saratani iliyotokana na matumizi ya tumbaku.
Serikali haina budi kuongeza kodi kwenye bidhaa zitokanazo na tumbaku kwenye bajeti yake ya mwaka 2014/15.
Kwa maana hiyo, Serikali itakuwa imeendana na kauli mbiu ya kuhamasisha watu kutotumia tumbaku duniani.
Kauli mbiu hiyo iliyotolewa na WHO inaeleza kuwa kodi ikiongezwa kwenye bidhaa zitokanazo na tumbaku kutawafanya watumiaji wengi hasa wale wapya kutojiingiza kwenye uraibu huo.
WHO inaamini kwamba matumizi ya tumbaku yakipungua dunia itakuwa imepiga hatua kuokoa maisha ya wanaokufa kutokana na tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment