WALIMU katika shule
za msingi nchini wamekuwa wanaendelea
kuwafanyisha kazi watoto wa shule za
msingi bila kuzingatia muda wa masomo hali ambayo inachangia kushusha kiwango
cha elimu nchini.
Mwandishi wa makala
haya ameshuhudia hivi karibuni wanafunzi karibu wote shule ya msingi Mfuate pichani kulia
iliyopo kata ya Likuyuseka wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wakifanyishwa kazi
ya kubeba tofali muda wa masomo.
Mkazi wa kijiji cha
Likuyu ambaye hakutaka jina lake kuandikwa alisema watoto kufanyishwa kazi
imekuwa ni kitu cha kawaida katika shule za kata hiyo na kusisitiza kuwa watoto
wanatumika pia kuwachotea walimu maji,kuosha vyombo na kazi nyingine za
nyumbani.
“Huku ni mbali sana
na makao makuu ya wilaya hivyo walimu wanawafanyisha kazi wanafunzi kwa
kutambua hakuna anayeweza kuona ingawa
viongozi wa serikali za vijiji wanaona
hali hii lakini hakuna anayekemea hivyo imekuwa jambo la kawaida tu’’,alisisitiza.
Uchunguzi ambao
umefanywa mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma umebaini tatizo la wanafunzi
kufanyishwa kazi mbalimbali muda wa masomo na baada ya masomo ni kubwa hali
ambayo inachangia kushusha taaluma.
Odo Komba mkazi wa
Liuli anasema kuna baadhi ya walimu wakuu wamekuwa wababe wanafanyisha kazi za
kubeba kuni,tofali,maji na wengine wanawatumia watoto wao kuvua samaki muda wa
masomo ametolea mfano shule ya msingi Muungano iliyopo kata ya Liuli imekithiri
kwa vitendo vya kutumikisha wanafunzi.
Tatizo la wanafunzi
kufanyishwa kazi muda wa masomo halipo Namtumbo na Nyasa mkoani Ruvuma pekee
bali pia kulingana na mwandishi wa kujitegemea Fransis Godwin uongozi
wa shule ya msingi Kising’a Isimani wilaya ya Iringa ulituhumiwa
kuwatumikisha kazi wanafunzi wakati wa vipindi vya masomo.
kuwatumikisha kazi wanafunzi wakati wa vipindi vya masomo.
Kitendo hicho kililaniwa vikali na
baadhi ya wazazi ambao watoto wao wanasoma katika
shule hiyo ambapo wameiomba wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi
kuingilia kati suala la utumikishaji wanafunzi wakati na baada ya masomo kwa
kuwa bado ni sugu nchini.
Wazazi
hao walidai kuwa uongozi wa shule
hiyo kila siku kabla ya
watoto kuingia madarasani wamekuwa wakiwatuma katika
kazi mbali mbali ikiwemo ya kuchota maji ya walimu.
Hata hivyo baadhi ya Halmashauri nchini
zimeanza kuchukua hatua kukabiliana na kuwatumikisha watoto kwa mfano
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, iliwahi kumvua madaraka ya ukuu
wa Shule ya Msingi Kitunga, Mwalimu Salvatory Roman, kutokana na tabia yake ya
kuwafanyisha kazi wanafunzi katika muda wa masomo.
Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya
Muleba, Pastory Kajuna,alisema Halmashauri hiyo ilifikia hatua hiyo baada ya
kuchoshwa na tabia aliyokuwa amejijengea mwalimu mkuu huyo ya kuwatumikisha
wanafunzi wa shule hiyo anavyotaka.
Alisema uongozi wa Halmashauri kupitia idara ya elimu ulishasambaza waraka maalumu katika shule zote zilizoko katika Halmashauri hiyo zinazowataka walimu kuacha kuwatumikisha wanafunzi wakati wa muda wa masomo.
Zaidi ya nusu ya Watanzania ni watoto, kuwekeza
kwa watoto kunanufaisha familia, jamii na ni kwa mustakbali wa Tanzania. Dira
ya Tanzania inayostawi kiuchumi inaweza kufikiwa tu ikiwa watoto watakua wakiwa na afya, wenye kupata lishe
bora, elimu bora na kulindwa dhidi ya vurugu, udhalilishaji na unyonyaji.
Kila nchi iliyofikia kuwa na maendeleo
ya kiuchumi ya kipato cha wastani imewekeza kwa watoto kwa kiwango kikubwa.
kuwekeza kwa watoto kwenye elimu bora, huduma za afya zilizoboreshwa na
kuwalinda watoto dhidi ya vurugu na udhalilishaji huzaa matunda yanayosababisha
kuwepo kwa uchumi imara, kupungua kwa uhalifu na kuwepo kwa familia zenye afya
bora.
Maendeleo makubwa yanaweza kupatikana
kwa kuzihamasisha jamii , kuongeza uwajibikaji na uwazi na kuhakikisha kuwa
Sheria ya Watoto inatekelezwa kikamilifu ili kuwalinda watoto.
Pamoja na kuwepo kwa mikataba ya
kuwalinda watoto dhidi ya utumikishwaji,tatizo hili lnaongezeka kwa kasi na
watoto kujikuta wakikosa haki zao za msingi kama kucheza,kupata elimu, kutunzwa
na kulindwa.
Watoto wamejikuta wakigeuka vibarua
katika mazingira hatarishi kama inavyothibitishwa na shirika linaloshughulika
na utafiti la(REPOA) ambapo mwaka 2006 matokeo yanaonyesha asilimia 20 ya
watoto kuanzia miaka 7-17 wanatumikishwa katika kazi zenye madhara.
Mwaka 2009 Bunge lilitunga Sheria ya
mtoto namba 21 yenye lengo la kudumisha haki za watoto na kuwapa haki
kisheria,ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo faini ya utumikishaji wa watoto ni
kiasi kisichopungua milioni tano na suala hilo kuachiwa mahakama kupanga kiasi
kulingana na uzito wa kosa.Sheria hiyo inataka watoto kupewa kazi nyepesi
zisizoweza kuathiri maumbile yao na makuzi.
Kila
mwaka Juni 12 ni siku ya kimataifa ya kupambana na ajira dhidi ya
watoto,kulingana na shirika la kazi Ulimwenguni (ILO) watoto milioni 215
wanafanyishwa kazi, nusu yao katika mazingira hatarishi.
Watoto
hawa hufanyishwa kazi katika machimbo ya dhahabu, wanatupa taka kutoka katika
majumba ya watu wengine, Watoto wanashindwa kusoma,kuandika na kuhesabu baadhi
yao wanashindwa hata kuandika majina yao wala kusoma kitabu, hawapati fursa
kabisa ya kucheza .
Utafiti
kutoka shirika la kazi Duniani unaonyesha kuwa maelfu ya watoto wanatumikishwa
katika kazi mbalimbali barani Afrika kwa mfano Zaidi ya watoto 500,000
wanafanyishwa kazi hatarishi nchini
Burkina Faso.
Kulingana
na ILO Karibu nusu wanafanyakazi nchini
Burkina faso katika takriban machimbo 600 ya dhahabu ni watoto. Mikono midogo
ya watoto hao hutumika kuvunja vunja mawe ili kuweza kupata dhahabu. Miili
midogo ya watoto hao hutumika kupenya
katika mashimo madogo ya machimbo ya dhahabu.
Mapafu
ya watoto hao huvuta hewa chafu ya kemikali zenye sumu kemikali za asidi salfuriki huku malipo kwa
watoto hawa yakiwa ni shida kwani hupewa
chakula tu.
Mwandishi Köpp Dirke aliyefanya utafiti wa
kutumikishwa watoto nchini Burkinafaso anasema katika maeneo ya machimbo watoto
wanafanyishwa kazi muda wote isipokuwa mchana na kwamba hakuna Muda wa kisheria
wa kufanyakazi katika Migodi wa dhahabu nchini Burkina Faso.
Kulingana na mwandishi huyo shule nyingi
katika eneo lenye machimbo ya dhahabu zina wanafunzi wachache. Watoto hawana muda wa kwenda shule asilimia kubwa ni
watoro.Hata hivyo Shirika la umoja wa mataifa ya kuwahudumia watoto (UNICEF)
hat limefanikiwa kuwarejesha watoto 7,000 shule.
Umoja wa Mataifa uliteua rasmi mwaka 1979, kuwa ni mwaka
Kimataifa wa Mtoto. Hii ilifuatiwa na kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa
Haki za Mtoto mwaka 1989 na hatimaye mwaka 1990 mkataba ulianza kutekelezwa
ukiwa kama sheria za kimataifa kuhusu haki za mtoto.
Mkataba huo wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za
mtoto ulikuwa ni sheria ya kimataifa inayotaka kuzingatiwa kwa haki za watoto
wote ulimwenguni hadi wanapokuwa wamefikia umri wa miaka18. Baadhi ya haki za
mtoto ni kulindwa, kuendelezwa, kuishi, kupata elimu, chakula, malazi na huduma
zingine muhimu kama matibabu.
albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917

No comments:
Post a Comment