Friday, May 16, 2014

MV Ruhuhu yasababisha watu kupoteza maisha


Na Albano Midelo
WATU wanaendelea kupoteza maisha katika mto Ruhuhu kutokana na kuvuka mto huo kwa mtumbwi baada ya kivuko cha MV Ruhuhu kushindwa kufanyakazi karibu msimu mzima wa mwaka.
Kutofanyakazi kwa kivuko cha Ruhuhu kinachounganisha wilaya za Nyasa mkoani Ruvuma na Ludewa mkoani Njombe kunasababisha vifo vya  watu wanaoamua kuvuka mto Ruhuhu kwa kutumia mitumbwi.

Wiki hii watu wanne wamepoteza maisha wakati wanajaribu kuvuka mto Ruhuhu kwa kutumia mtumbwi,kasi ya maji ya mto Ruhuhu ilisababisha kupindua mtumbwi na kusababisha vifo vya watu wote waliokuwa wanavuka kutoka Lituhi wilayani Nyasa na kwenda  wilayani Ludewa.
Kaimu afisa mtendaji wa kata ya Lituhi Joseph Chawala amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kueleza kuwa miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya mtumbwi huo ni mama aliyekuwa na mtoto na kwamba hadi sasa wamefanikiwa kupata mwili wa mtu mmoja ,miili mingine ukiwemo wa mama na mtoto wake bado haijapatikana hadi sasa.
Hata hivyo alisema juhudi za wakazi wa Lituhi kuendelea kuitafuta miili mingine bado zinaendelea ingawa alisema inawezekana miili hiyo imesombwa na maji hadi ziwa Nyasa.
Chawala alisema wakazi wa kata ya Lituhi wapatao 12,000 wanapata shida kuvuka kutokana na kivuko mto M.V Ruhuhu kuhshindwa kufanyakazi kwa mtu mrefu hali ambayo inasababisha kuamua kuvuka kwa kutumia mitumbwi jambo ambalo limekuwa linasababisha ajali ya mitumbwi hiyo kupinduka na kusababisha vifo.
“Kivuko cha Ruhuhu kinafanya kazi kwa miezi mitatu tu kwa mwaka kinaanza mwezi Juni hadi Agosti,hali hiyo inatokana na serikali kushindwa kujenga gati bora kwa ajili ya kuweka nanga kivuko kinapotoka upande mmoja wa mto na kwenda upande mwingine,maji ya mto Ruhuhu yanapokuwa mengi kivuko hakiwezi kupaki kwa sababu gati yake imejengwa vibaya’’,alisema Chawala.
Alisema kuwa magari yanashindwa kuvushwa katika kivuko hicho hali ambayo inasababisha kuzunguka kutoka Lituhi, Songea hadi Njombe kisha Ludewa mjini safari ambayo inachukua siku nzima wakati kwa kutumia kivuko cha M.V Ruhuhu  ni mwendo wa saa moja hadi Ludewa mjini.
Baadhi ya wakazi wa Lituhi na Ludewa walisema kivuko cha Ruhuhu ni kero ya muda mrefu ambayo hata Rais Jakaya Kikwete anaifahamu na aliahidi kuitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa inagharimu maisha ya watu kila mwaka pia inazorotesha maendeleo yao kiuchumi.
Julius Challe mwenyekiti wa kitongoji cha Lituhi anasema wakazi wa Lituhi wanapata matatizo makubwa kutokana na ukosefu wa huduma za kivuko cha Ruhuhu hawajui lini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa ni tatizo la muda mrefu ambalo serikali imekuwa itoa ahadi zisizotekelezeka za kujenga daraja.
Joseph Mhagama miaka 69 anasema kivuko hicho licha ya kuwa ni kipya na injini zake zote mbili na zinafanyakazi, tangu mwaka huu umeanza hakijafanyakazi  na  serikali haishituki kutokana na idadi ya watu wanaopoteza maisha kila mwaka kutokana na  kuvuka mto Ruhuhu kwa njia ya mtumbwi.
Wananchi wanaotegemea kivuko hicho kwa kiwango kikubwa ni kutoka vijiji vya Msungu,Ilela,Mbongo,Manda,Lupingu na Ngerenge wilayani Ludewa mkoani Njombe na vijiji vya Lituhi,  Nkaya, Mwelampya,Kihulu,Litumbakuhamba na Ngingama wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
 Mbunge wa Mbinga Magharibi Kapteni John Komba (CCM), amewahi kuiomba Serikali kujenga daraja katika mto Ruhuhu  ili kuwawezesha wananchi kuvuka mto huo kwa urahisi kutokana na tatizo la kivuko cha M.V Ruhuhu.
Katika swali lake lililoulizwa bungeni kwa niaba yake na mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo, lilieleza kuwa wananchi wamekuwa wakipata shida kuvuka mto huo kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kivuko cha MV Ruhuhu katika kipindi karibu chote cha mwaka.
Alisema kivuko kipya kilichopo kwenye mto huo kimekuwa kikishindwa kufanya kazi wakati wa masika maji yanapokuwa mengi na pia wakati wa masika kutokana na kina kifupi cha maji hali aliyosema inasababisha usumbufu kwa wananchi.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Miundombinu alisema kuwa Serikali inafahamu tatizo lililopo katika kivuko hicho kipya kushindwa kutumika katika baadhi ya misimu ya mwaka.
Alisema kabla ya kununuliwa kwa kivuko hicho kulikuwa na tatizo kubwa la kivuko kwani kivuko kilichokuwepo kilikuwa ni chakavu ambapo kiliendeshwa kwa kuvutwa na kamba kwa kutumia nguvu za binadamu.
Alisema Serikali iliamua kununua kivuko hicho kama suluhisho la muda wakati ikiendelea na mikakati ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja  ambalo litawahakikishia usafiri wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Alisema wakati mwingine kupungua kwa kina cha maji katika mto huo kumekuwa kukichangiwa na uharibifu wa mazingira ambapo alitoa wito kwa wananchi wanaoishi kandokando ya mto huo kushiriki kikamilifu katika kutunza mazingira ya mto huo ili maji yasipungue.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005, Chama cha Mapinduzi kiliahidi kupitia Ilani yake kutatua tatizo la vivuko kadhaa nchini, kimojawapo kikiwa ni kivuko cha mto Ruhuhu mkoani Ruvuma ambacho kinaitwa kivuko cha M.V Ruhuhu ingawa ni kivuko kipya  kinashindwa kufanyakazi karibu msimu wote wa mwaka.

No comments:

Post a Comment