Na Albano Midelo
NGORO pichani ni aina ya kilimo kinachohifadhi mazingira kwa njia ya asili ambacho kinaaminika kilianza kutumika na wakulima wa kabila la wamatengo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma zaidi ya miaka 300 iliyopita.
Kilimo cha ngoro
kilianzishwa na wazee maarufu wa kabila la wamatengo waliotokea nchini Malawi
katika karne ya 17 ambapo tayari vizazi zaidi ya 10 vimepita hivi sasa tangu
kilimo cha ngoro kilipoanzishwa wilayani Mbinga.
Moja ya madhumuni ya kuanzisha kilimo hiki ni
kuudhibiti udongo wa juu wa ardhi ambao
kwa kawaida huondolewa na maji au upepo
kutokana na mmomonyoko wa ardhi ya juu ambayo ina rutuba nyingi ya
kuifanya mimea iweze kustawi vizuri na hatimaye kutoa mavuno mengi na bora.
‘‘Tunajua kuwa udongo
ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi
vizuri, Kutoweka kwa udongo wa juu toka shambani au bustani kwa njia ya
mmomonyoko ni hasara kubwa , kwa vile kunasababisha upungufu wa mavuno. Hivi
basi lazima kuzingatia hifadhi ya ardhi ili mkulima aweze kupata mazao bora’’,anasema
Ngwatura Ndunguru mbunge mstaafu wa Mbinga.
Njia za kuhifadhi
ardhi zinaweza kutumiwa kwa kutegemea hali ya hewa, mazingira ya eneo kama ni
maeneo ya mwinuko au tambarare. Hata hivyo zinaweza kutumika njia mbili au tatu
katika shamba moja. Ziko njia kuu mbili za kuhifadhi ardhi ambazo ni njia za
asili au za kienyeji na njia ya kisasa ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina na
wataalamu.
Wataalamu
wazungumzia ngoro
Wataalamu wakongwe
kama akina Bike mwaka 1938,
Stenhouse mwaka 1994, Temu na Bisanda mwaka 1966 wanaeleza kuwa Wamatengo
walilazimika kutumia kilimo cha ngoro
ili kuhifadhi udongo mzuri uliopo katika miteremko hiyo. Ngoro hulimwa
kwa kuchimba mashimo madogo madogo katika miteremko hiyo.
Katika mashimo hayo
hupandwa mazao kama maharage,mahindi na ngano kwenye kingo za mashimo hayo.
Mkulima hufyeka shamba lake na kuzipanga nyasi zilizokatwa katika mistari
kwenda juu mpaka chini na toka upande wa kushoto kwenda kulia.
Mkulima akipindua udongo wa chini kuwa juu na
chini ya udongo wa juu hukata nyasi na udongo wenye rutuba hugeuka kuwa mboji
na polepole udongo wenye rutuba huongezeka. Maji ya mvua yakisimama katika
mashimo hayo madogo hulinda unyevu wa
ardhi na kukinga mmomonyoko wa ardhi.
Inaaminika kuwa
kilimo cha ngoro ambacho tunaweza kukiita draft agriculture kinahusishwa na
shughuli za kuwepo kwa mapango ya kuishi.Historia ya wilaya ya Mbinga
inaonyesha kuwa,hapo zamani wananchi wa wilaya ya Mbinga walikuwa na tabia ya
kufanya kilimo cha kuhamahama.
Wakulima wakati huo
walilima sehemu moja na wanapogundua sehemu hiyo rutuba imemalizika walikuwa
wanahamia sehemu nyingine yenye rutuba na kuendesha kilimo bila kujali athari
za kimazingira ambazo zilikuwa zinajitokeza kutokana na aina hiyo ya kilimo.
Kutokana na kuwepo
kwa mapango, wazee hao wa kabila la wamatengo waliamua kuanzisha kilimo cha
kulima na kufukia majani ili kupata mbolea
ya asili hivyo kuendesha kilimo walichokiita ngoro katika sehemu moja bila
kuhama huku wakirutubisha ardhi na kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na
ardhi ya Mbinga kuwa na milima yenye
miteremko mikali.
Mbunge mstaafu wa
Mbinga Ngwatura Ndunguru anasisitiza
kuwa wamatengo tangu wameanza kutumia kilimo cha ngoro miaka 300 iliyopita hadi
sasa wamekuwa wanazalisha vyakula kwa wingi pamoja na kuhifadhi mazingira kwa
njia ya asili kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokea kwenye miteremko ya milima
ya umatengo wilayani humo.
Anabainisha zaidi
kuwa kilimo cha ngoro ni sawa na mchanganyiko wa kilimo cha umwagiliaji mvua zinaponyesha maji huingia taratibu
kuingia kwenye mmea na kuzuia udongo usiharibiwe na kwamba yale majani
yaliyowekwa chini yanaoza ambapo katika msimu mwingine wa kilimo majani yaliota
kwenye shimo yatafyekwa mazao yaliosalia
yatavunwa na kutandazwa kwenye shimo na kufukuliwa majani ya mwaka jana ambayo tayari
yanakuwa mboji.
John Mbunda(80) mkazi
wa kijiji cha Kilanga Juu wilayani Mbinga anasema wamatengo walianzisha
mfumo maalumu ya kilimo cha ngoro
uliyowasaidia uliyojulikana kwa jina la “Ingoro,” mfumo ambao uliwawezesha
kuendelea kulima kwenye maporomoko ya milima bila ya kusababisha mmomonyoko wa
udongo au kuathiri vibaya rutuba kwenye mashamba yao.
Alex Ndunguru mkazi
wa kijiji cha Ilela anasema wenyeji wa Mbinga walilazimika kubuni kilimo cha ‘ngoro ili
kuhifadhi udongo mzuri ulio katika miteremko ya Umatengo na kwamba ngoro ndiyo
mkombozi katika kilimo kwa kuwa kilimo kimekuwa endelevu badala ya mfumo wa
zamani ambao wamatengo walifanya kilimo cha kuhamahama.
‘‘Nafurahia
sana kilimo cha ngoro ambacho tunachimba vishimo katika miteremko na kupanda
mazao kama maharage,mahindi, ngano, kwenye kingo za vishimo hivyo ambapo
mkulima hutayarisha shamba kwa kufyeka nyasi,kisha kuzipanga nyasi zilizokatwa
katika mistari, kuzigeuza na zikioza hupatikana udongo wenye rutuba’’,alisisitiza
Ndunguru.
Teknolojia
ya ngoro ni bora
Utafiti wa kina umeonyesha wazi kwamba teknolojia ya ngoro ni bora zaidi katika
kilimo,ambapo wakulima kutoka maeneo
mbalimbali nchini wamekuwa wakifika katika wilaya ya Mbinga kujionea wenyewe na
kujifunza teknolojia hiyo ya kilimo cha ngoro na kwenda kuanzisha aina hiyo ya
kilimo katika maeneo yao kwa lengo la kuhifadhi ardhi na kutunza mazingira kwa
muda mrefu.
Moja ya faida ya kilimo cha ngoro ni kwamba hata kama mvua hazitanyesha, bado shamba litaendelea kuwa na unyevunyevu kutokana na maji yaliyomo ndani ya mashimo hayo,isitoshe wakati wa mavuno, mabaki ya nafaka huwa yakitupwa kwenye mashimo hayo,husababisha shamba kustawi vizuri zaidi kutokana na mbolea iliyowekwa.
Moja ya faida ya kilimo cha ngoro ni kwamba hata kama mvua hazitanyesha, bado shamba litaendelea kuwa na unyevunyevu kutokana na maji yaliyomo ndani ya mashimo hayo,isitoshe wakati wa mavuno, mabaki ya nafaka huwa yakitupwa kwenye mashimo hayo,husababisha shamba kustawi vizuri zaidi kutokana na mbolea iliyowekwa.
Ngoro
kivutio cha utalii
Kulingana na Mbunge mstaafu wa Mbinga Ndunguru tayari wameanza
kukitangaza kilimo hicho na kukiingiza kuwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii
ambavyo vinapatikana katika wilaya ya Mbinga pekee na hakuna sehemu nyingine
yeyote duniani inayoendesha kilimo cha aina hiyo.
Baadhi ya
wageni ambao wamekuwa wakitembea kwenye
magari kupitia barabara ya Mbinga hadi Mbambabay wilayani Nyasa pamoja na
maeneo mengine ya milima ya umatengo wamekuwa wakisimama mara kwa mara kwenye
milima hiyo na kuchukua picha za kawaida na video kwenye kilimo cha ngoro
ambacho kimeonekana kuwavutia watu wengi
wa ndani na nje ya nchi hasa mimea inayochomoza na kuonekana mfano wa mapambo yaliopambwa juu ya milima.
Wizara
yatambua kilimo cha ngoro
Wizara ya Kilimo
Chakula na Ushirika imeanzisha Mradi wa kufufua Mifumo muhimu ya asili ya
kilimo Duniani (Global Importance Agricutural Heritage System- GIAHS) ili
kuendeleza Kilimo cha asili (Oranic Farming) na kumpunguzia mkulima gharama za
uzalishaji.
Afisa mkuu wa kilimo kutoka idara ya matumizi bora ya ardhi Firmat Banzi anasema mradi huo unatekelezwa na Shirika la chakula na kilimo Duniani (FAO) ambao unalenga kutambua mifumo ya asili na endelevu ya kilimo na ufugaji ili kumsaidia mkulima na kwamba mradi unagharimu zaidi ya dola laki mbili ambazo zimetolewa na Serikali ya Ujerumani.
Alisema kuwa katika Afrika Mashariki nchi ya Tanzania na Kenya ilichaguliwa kufufua mifumo hiyo kwa kuwa na sehemu muhimu za kilimo na kwamba baada ya kuchanguliwa nchi ya Tanzania ilipendekeza mifumo mitatu ya kilimo asili ukiwemo mfumo wa Ngoro ambao unatumiwa na kabila la wamatengo.
Mifumo ya asili ya kilimo ilianza kupendekezwa dunia toka mwaka 2002 na baadhi ya nchi zimeanza kutumia mifumo hii, baadhi ya nchi hizo ni Japani, Philipino, China na Ujerumani.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment