Sunday, January 31, 2016

Wananchi waipongeza CARITAS Songea



Na Livingston Benson-OUT
Baadhi ya wakazi wa kata tano katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambazo zimezungukwa na mradi wa uchimbaji wa madini ya uranium(urani) wamelipongeza shirika la CARITAS kwa kutoa elimu ya madhara ya madini hayo kiafya na kimazingira.
Wakazi hao walitoa pongezi hizo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya uelewa wa madini ya uranium
awamu ya pili yaliofanyika katika ukumbi wa CARITAS jimbo kuu la Songea.


Mwezeshaji wa mafunzo hayo Leonard Mgaya alisema mafunzo hayo yalianza Novemba mwaka 2014  hadi Desemba mwaka 2015 ambayo yalishirikisha wawakilishi 30 kutoka kata zinazozunguka mradi wa urani wilayani Namtumbo ambazo ni kata za Likuyuseka, Mgombasi,Mchomolo,Kitanda na Lwinga.
Mgaya alibainisha matokeo ya mradi wa mafunzo hayo ambayo pia yalishirikisha waandishi wa habari 30 kutoka mkoani Ruvuma yamewezesha wakazi wanaozunguka mradi kuelewa madhara ya madini ya urani na kuchukua tahadhari pale wanapofanyakazi mgodini ili wasipate madhara.
Hata hivyo mmoja wa washiriki ambaye pia ni mwenyekiti wa asasi ya Tanzania mineral mining Trust Fund Wilbert Mahundi ambaye  pia ni diwani wa kata ya Ruhuwiko,alitaja changamoto kubwa iliyojitokeza katika mradi huo ni vitisho kutoka serikalini kwa kuwa inapinga madhara ambayo yanatajwa na wataalam ambayo yanaweza kupatikana kutokana  na madini ya uranium.
Wakizungumza katika hitimisho la mafunzo hayo baadhi ya washiriki wamependekeza kuundwa na kuimarisha mtandao wa urani katika ngazi ya vijiji na kata ili kuendelea kujenga ufahamu wa madhara yanayoweza kuletwa na madini ya urani.
Washiriki hao pia wamependekeza kuwepo na usaidizi wa kisheria kwa wananchi wote ambao watathibitika wameathirika na madini ya urani kwa sababu kwa mujibu wa sheria kila mtanzania anatakiwa kuishi katika mazingira safi na salama.
Utafiti wa mradi wa Urani wilayani Namtumbo umekamilika  ambapo  Mradi wa madini hayo katika Mto Mkuju wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma unaomilikiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited na Kampuni tanzu ya URMZ ya Urusi unatarajiwa kuanza wakati wowote.

Mradi wa Mto Mkuju upo ndani ya pori la akiba la  Selous (Selous Game Reserve).Eneo hilo ni Sehemu ya Urithi wa Dunia (World Heritage Site) tangu mwaka 1980.

Mwezi Julai, 2012,Tume ya urithi wa Dunia yaani World Heritage Committee iliyoko chini ya UNESCO ilitoa idhini ya kuondoa eneo la Mradi wa Mto Mkuju lenye ukubwa wa kilometa 345 kati ya kilometa 50,000 kwenye Eneo la Urithi wa Dunia ili uchimbaji wa Urani uweze kufanyika.
Hata hivyo mwezi Agosti mwaka 2015 aliyekuwa Naibu waziri wa Nishati na madini Charles Kitwanga alitembelea eneo la mradi la mto mkuju litakalochimbwa madini ya urani katika wilaya ya Namtumbo na kuwaahidi wananchi kuanzia  mwezi Aprili mwaka 2016 mradi wa uchimbaji wa uranium unatarajia kuanza uzalishaji.
Kitwanga alisisitiza wizara ya nishati na madini ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha makubaliano ya kuanza rasmi uzalishaji ifikapo Aprili 2016.
Utafiti wa madini ya urani katika eneo la mto mkuju lenye ukubwa wa kilomita za mraba 20,000 unasimamiwa na kampuni ya Mantra Tanzania, tangu mwaka 2007 tayari umeshafanya uwekezaji wa dola za kimarekani milioni 200.
Kwa muda mrefu wataalam wa mazingira,madaktari pamoja na wanasheria wamekuwa wanaionya serikali kusimamisha mradi wa uchimbaji wa madini ya uranium kutokana na kutajwa kuwa na madhara makubwa kuliko faida. Mradi huo unatarajiwa utadumu kwa miaka 12 tu.
Mradi wa mafunzo ya uelewa wa madini ya urani katika afya na mazingira wilayani Namtumbo yalifanyikwa kwa kuhusisha mashirika matatu yasiyokuwa ya kiserikali ambayo ni CARITAS, TMMTF na MVIWATA.
Mwisho

No comments:

Post a Comment