NA
KWIRINUS MAPUNDA,SONGEA
HALMASHAURI ya
manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imetoa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 52
katika vikundi 107 vya wajasiriamali ili kuendeleza miradi yao.
![]() |
| Jenifer Omolo mkurugenzi wa manispaa ya Songea |
Akizungumza wakati
anafungua mafunzo hayo,mkurugenzi wa manispaa ya Songea Jenifer Omolo amewaasa
wanakikundi kukopo fedha hizo zenye riba nafuu na kuacha kwenda kukopa katika
asasi za kibenki ambazo zinatoza riba kubwa kwa mkopaji.
“Sisi manispaa
tunatoa riba ya asilimia kumi tu kwa mkopo wa mwaka mmoja
,asasi nyingi za
kifedha zinatoa riba kubwa yenye makato mengi hali inayosababisha wakopaji
kushindwa kufikia malengo yao,hata hivyo ili mfuko uimarike ni lazima mrejeshe
mikopo tunayowapatia kwa wakati’’,alisisitiza Omolo.
Kwa mujibu wa
mkurugenzi huyo mwaka jana wakopaji hawajarejesha shilingi milioni 30 ambazo
walikopeshwa na Halmashauri hiyo na kuwaagiza wote ambao hawajarejesha
warudishe mikopo hiyo na kwamba katika urejeshaji wa fedha za serikali au mkopo
hakuna hadithi zaidi ya kurudisha mikopo kabla ya hatua kuchukuliwa.
Kwa upande wake
mchumi wa manispaa hiyo Raphael Kimary aliwaasa wajasiriamli hao kuwa na
nidhamu katika mikopo na kuhakikisha
wanarejesha kwa wakati.
Kimary alibainisha
kuwa mkopo huo wa fedha umetolewa na manispaa kwa lengo kusaidia vikundi vya
wajasirimali katika shughuli za
uwekezaji na kuhakikisha wanarejesha ili
kusaidia vikundi vingine vya
wajasirimali katika manispaa hiyo.
“Zingatieni taratibu
zote za mafunzo ambayo mmepewa kabla ya kupewa mkopo,fedha hizo zisifanye mambo
ambayo hayapo katika mradi huo,muwe wajasirimali wa kweli ili muweze kuondokana
na umaskini,kumbukeni fedha tunazowakopesha
zitafuatiliwa na mnatakiwa kurejesha
mkopo kwa wakati ili tuendelee kuwakopesha wajasirimali wengine’’,alisisitiza
Kimary.
![]() |
| Baadhi ya vikundi vya wajasirimali wakipata mafunzo |
Kwa upande wake afisa
maendeleo ya jamii wa manispaa hiyo Naftali Saiyoloi
alisema
mkopo huo unatolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana na kwamba lengo ni kuinua
hali ya uchumi katika makundi hayo mawili.
Kwa mujibu wa afisa
maendeleo huyo,mfuko wa kukopesha wanawake na vijana ulianzishwa mwaka 1993 na
kwamba mfuko huo licha ya kuwa na fedha kidogo ,umelenga kuongeza ajira,kuinua
uchumi wa mwananchi wa kawaida na hasa vijana na wanawake.
“Masharti
yanayomwezesha mjasiriamali kupata mkopo huo,awe mwanamke au kijana mwenye umri wa kuanzia
miaka 18 na kuendelea,awe amejiunga kwenye vikundi vya kuanzia watu
watano,kikundi kiwe na katiba,mkopo unalipwa ndani ya mwaka mmoja kwa riba ya
asilimia 10 tu’’,alisema.
Akitoa mada ya kanuni
za kikundi,akiba ya pamoja na umuhimu wake,afisa maendeleo ya jamii Scholastica
Gowele aliwatahadharisha wajasirimali hao kuwa lengo la mkopo huo sio kuanzisha
mradi au biashara mpya badala yake ni kuendeleza biashara ambazo wamezianzisha
ili ziweze kuwaletea faida zaidi.
Naye afisa biashara
wa manispaa hiyo Raymund Raphael aliwataka wanavikundi kuhakikisha kuwa
wanafanya biashara ambayo itawapatia faida hivyo kabla ya kuendeleza biashara
zao ni vema kwanza kufanya utafiti wa
ili kufahamu wateja wao na masoko ya biashara zao.
Mada ambazo
zimefundishwa katika mafunzo hayo ni
historia fupi ya mfuko wa maendeleo ya wanawake na vijana,taratibu na
masharti ya mkopo,usimamizi na ulipaji wa mikopo,namna ya kuunda
vikundi,uendeshaji na usimamizi wa miradi ya vikundi,soko la biashara,mahusiano
ya biashara,utunzaji wa kumbukumbu na ujazaji wa mikataba.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment