Wednesday, June 22, 2016

Serikali yahairisha ajira zote kwa muda

Ajira zitarejeshwa baada ya uhakiki wa watumishi hewa kumalizika

Na Albano Midelo

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imehairisha ajira zote kwa muda hadi hapo itakapokamilisha kazi ya uhakiki wa watumishi hewa pamoja na kuwaondoa katika mfumo wa mishahara.
Katibu mkuu Utumishi Dk.Laurean Ndumbaro

Katibu mkuu utumishi Dk.Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya ya Songea kwenye ukumbi wa manispaa ya Songea  amesema zoezi la kuwaondoa watumishi hewa likimalizika taratibu nyingine za utumishi zikiwemo za kupanda madaraja na kutoa ajira mpya zitaendelea.

“Ajira mpya na marekebisho ya mishahara kwa watumishi wa umma havijasitishwa,vimehairishwa (postponed) kwa muda hadi hapo
uhakiki wa kuwaondoa watumishi hewa utakapokamilika ajira na upandishwaji vyeo kwa watumishi wa umma utaendelea kama kawaida’’,alisisitiza Dk Ndumbaro.

Amesema serikali hivi sasa inaweka taarifa za kila mtumishi wa umma katika hali ya usahihi kabla ya kuendelea na mazoezi mengine na kwamba serikali pia imetoa waraka wa kupitia muundo wake mpya wa utumishi ili kuona idara na vitengo vilivyopo iwapo bado vina haja ya kuendelea kuwepo au kupunguzwa hali itakayoboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi kulingana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

Hata hivyo amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya maofisa utumishi  ambao watashindwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria hali ambayo inawasababisha usumbufu watumishi wa umma ambao wanawasimamia katika maeneo yao ya kazi hivyo kuwasababishia kukosa ari ya kufanyakazi baada ya kukosa stahili zao katika utumishi wa umma.

Amewatoa hofu watumishi wa umma kwa changamoto ambazo wanazipata katika kipindi hiki cha mpito na kwamba wizara ya utumishi wa umma ipo tayari kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi na kuzitafutia ufumbuzi wa kuduma.

Katibu mkuu utumishi amefanya ziara ya siku mbili mkoani  Ruvuma akiwa na watendaji wake wa wizara ikiwa ni wiki ya utumishi wa umma ambayo inaanza Juni 16 hadi Juni 23 kila mwaka ikiwa na lengo la kutenga siku moja ya kuwatembelea na kusikiliza kero mbalimbali za watumishi wa umma na kuzitafutia ufumbuzi.

Baadhi ya watumishi wa umma wa wilaya ya Songea wamefarijika na ziara hiyo ya katibu mkuu ambapo wamepata fursa za kutaja changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utumishi wa umma ikiwemo ya kuchelewa kupanda vyeo, kutopata fedha za likizo kwa wakati na kutorekebishiwa mishahara yao kwa wakati.

Baadhi ya changamoto zimeweza kushughulikiwa na katibu mkuu papo hapo kwa kushirikiana na timu yake yote kutoka wizarani jambo ambalo limepongezwa na watumishi wa umma ambao baadhi ya wamehaingaika kwa kati ya miezi sita hadi miaka mitatu bila ufumbuzi.
Baadhi ya watumishi wa umma wa  Songea mjini

Awali mkurugenzi wa manispaa ya Songea Jenifer Omolo akizungumza na watumishi wa umma wa manispaa hiyo katika wiki ya utumishi wa umma amewakumbusha kufanyakazi kwa misingi ya utumishi wa umma.

“Hata kama unakunywa kunywa kama mtumishi wa umma badala ya kuwa mlevi,kuanzia sasa watumishi wote wa umma ambao watakwenda kinywe cha maadili wataitwa katika vikao vya maadili,kama wewe ni mlevi tutatumia evidence ikiwemo kupigwa picha wakati umelewa tafadhali naomba kila kitu mfanye kama watumishi wa umma’’,alisisitiza.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment