Monday, June 6, 2016

Mkakati wa manispaa ya Songea kuwa jiji waiva

Ni mpango wa miaka mitatu ijayo

Na Kwirinus Mapunda

HALMASHAURI ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeweka mpango mkakati wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2019/2020 ili kuwa na mwelekeo wa utoaji wa huduma za msingi za kuanzishwa kwa Halmashauri ya  jiji la Songea.


Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo anasema mpango mkakati wa miaka mitatu katika manispaa hiyo umetolewa na  Baraza la madiwani  kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali wa manispaa hiyo.

Lengo la manispaa hiyo  ni kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Halmashauri ambayo yameainishwa katika sheria namba nane ya uanzishwaji wa serikali za mitaa, miji, manispaa na jiji ili
kutekeleza azma yake ya safari ya kuelekea jiji la Songea kutoka manispaa.

Dira ya Halmashauri ya manispaa ya Songea ni  kuwa mji uliopangika miundombinu ya kisasa na ongezeko la kipato pamoja na kuwa na wananchi wenye maisha bora na endelevu kwa kudumisha ulinzi,usalama,usafi wa mji,uadilifu,uwazi,uzalishaji bora  hivyo kukuza manispaa ya Songea  na kuwa jiji la Songea.

Mwelekeo wa Halmashauri ya manispaa ya Songea ni kutoa huduma bora za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wake kwa kutumia fursa na rasilimali,kuhamasisha, kuendeleza, kuimarisha na kusajirisha wananchi katika mazingira ya ushindani na ubadilishaji rasilimali na huduma endelevu.

Mstahiki meya wa Manispaa ya Songea Abdul Hassan Mshaweji anabainisha kuwa manispaa inatarajia kufikia malengo ya kuwa jiji kwa kuzingatia Sayansi,teknolojia,utawandawazi na soko huru kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu na kuongeza ufanisi mkubwa kwa kutumia utawala bora ili kuinua na kuboresha maisha ya wakazi wa manispaa hiyo.

Ili kuhakikisha uchumi wa Halmashauri ya manispaa inakua,Mshaweji ameutaja mwelekeo ni kuongeza uzalishaji na mauzo ya bidhaa, kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki pamoja na kuwa na miradi ya uzalishaji yenye tija na utendaji wenye maadili na nidhamu kwa kuzingatia kauli mbiu ya Hapa kazi tu ifikapo mwaka 2017.


“Manispaa ya Songea imejiwekea malengo makuu na malengo mahususi ambayo yanatekelezwa kwa kufuata shabaha zilizopangwa ili kufikia malengo shughuli mbalimbali zimepangwa kwa kuzingatia ukomo wa  bajeti na vipaumbele vya kitaifa,hususuani kufuata ilani ya Chama tawala’’,anasema Mshaweji.

Malengo makuu yatakayohakikisha manispaa inatekeleza mpango mkakati kikamilifu ni pamoja na kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI,kupambana na rushwa na kuboresha huduma za kiuchumi  pamoja na kuimarisha miundombinu ya mji uliopangika ili uweze kuwa na hadhi ya jiji.

Malengo mengine ni kuimarisha masuala ya utawala bora, elimu, afya,maji na ukusanyaji wa mapato,kuwepo kwa usawa wa kijamii,kusimamia maliasili na mazingira,kuwepo miundombinu bora na ya kisasa,kuwepo zana bora  za kufanyia kazi mbalimbali ili kuongeza mapato.

Manispaa pia imelenga kuongeza ufanisi katika utendaji na kuacha kufanyakazi kwa mazoea,kuondoa kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wananchi,kupitia kero zote zinazosubiri maamuzi husuasn sekta ya ardhi na kuendeleza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wakiwemo walimu,waganga na wafanyabiashara ndogondogo.

Ili kuhakikisha manispaa inakamilisha safari yake ya kuwa jiji Mstahiki Meya ameitaja moja ya mikakati iliyopitishwa na manispaa hiyo kuwa ni kufungua barabara zote za mtaa kwa mtaa, barabara za kata kwa kata na barabara zote za muingiliano na Halmashauri jirani pamoja na kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika unapatikana katika mji wa Songea.

Katika kuhakikisha huduma za msingi zinatolewa kwa wananchi  Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeweka mikakati na Malengo maalum ili kuboresha huduma hizo.Mikakati hiyo ni pamoja na  Kuchangia na kuhamasisha miradi inayoibuliwa na kutekelezwa na jamii yenyewe na Kuendeleza kilimo masoko na  kuboresha miundo mbinu ya kilimo na mifugo sanjari na kutoa elimu kwa wakulima.

Manispaa ya Songea inatarajia Kujenga miundo mbinu ya miradi ya maji safi na salama kwa wananchi,Kusimamia utoaji taaluma katika shule za msingi na sekondari na kuwawezesha wanafunzi wa darasa la saba kufaulu mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza.


Kuboresha huduma za afya kwa kukarabati na kujenga majengo ya kutolea huduma za afya, kuboresha upatikanaji wa madawa na kuongeza wataalam wa kutoa huduma ni miongoni mwa mikakati iliyowekwa na manispaa hiyo.

Mikakati mingine itakayokamilisha safari ya manispaa ya Songea kuwa jiji ni Kuboresha miundo mbinu ya barabara kwa kufanyia matengenezo na kujenga madaraja ya kudumu na kuimarisha shughuli za kiuchumi za wanawake, vijana  wazee na sekta isiyo rasmi.

Katika kipindi safari ya kutoka manispaa hadi kuwa jiji la Songea manispaa hiyo imepanga kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo (NGO),Mashirika ya dini na vyama na vikundi vya kijamii (CBOs) na Kuhamasisha walipa kodi umuhimu wa kulipa kodi,Kuimarisha na kuendeleza Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo na vyama vya huduma za kifedha vingine.

Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina zaidi ya watu 203,309 kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.Manispaa ya Songea ina kata 21 na mitaa 95 ikiwa ndiyo makao makuu ya mkoa wa Ruvuma.

Halmashauri nyingine ambazo zinaunda mkoa wa Ruvuma ni Halmashauri ya wilaya ya Songea, Namtumbo, Tunduru, Nyasa,Halmashauri ya wilaya ya Mbinga na Halmashauri ya mji Mbinga.

kwirinusmapunda@yahoo.com

No comments:

Post a Comment