Na Albano Midelo
"Boti
ya doria ilishindwa kuwaokoa waliozama ziwa Nyasa baada ya
wilaya nzima kukosa kituo hata kimoja cha mafuta hivyo boti ilishindwa
kusafiri'' anasema mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa.
Wakazi wa wilaya ya
Nyasa mkoani Ruvuma wameendelea kutoa wito kwa serikali kuharakisha mchakato wa
ujenzi wa kituo cha mafuta ili kusogeza huduma hiyo jirani na wilaya.
Wilaya ya Nyasa yenye
kata 20 haina kituo hata kimoja cha mafuta hali ambayo inasababisha changamoto
kubwa pale inapotokea dharura ya mahitaji ya mafuta ambayo yanapatikana kwenye
vituo vya mafuta vilivyopo wilayani Mbinga takribani umbali wa zaidi ya
kilometa 60.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Jabir Shekimweri amesema mahitaji ya kituo cha
mafuta katika wilaya ya Nyasa na hasa
mji wa Mbambabay ambayo ndiyo makao makuu ya wilaya hiyo ni makubwa kutokana vyombo vya usafiri vya nchi kavu na
majini kuhitaji mafuta ya petroli na dizeli.
“Hivi karibu kutokana
na boti la doria la serikali kukosa mafuta,tumeshindwa kuwaokoa watanzania karibu 11 ambao walipata ajali ya kuzama na
boti wakati wanatoka Mbambabay kwenda nchini Malawi,boti ingekuwa na mafuta
pengine tungeweza kuwaokoa’’,alisema mkurugenzi huyo.
Kuna taarifa kuwa
mwanamke mmoja akiwa katika boti hilo alimpigia simu mumewe kuwa endapo
wangefika katika eneo ambalo walipata ajali kabla ya saa mbili kupita wanaweza
kuokolewa lakini walishindwa kwenda huku baada ya boti la doria kukosa mafuta
hivyo abiria wote ambao walikuwa katika boti hiyo waliangamia katika ziwa
Nyasa.
Kamanda wa polisi wa
mkoa wa Ruvuma kamishina msaidizi wa polisi Zuberi Mwombeji amethibitisha
abiria wote 11 waliokuwa katika boti ya
MV.Mapenza walifariki Dunia ambapo hadi
sasa ni mati wawili tu wamepatikana na kazi ya kutafuta maiti wengine
inaendelea .
Mkurugenzi wa wilaya
ya Nyasa ametoa wito kwa serikali kuharakisha ujenzi wa meli ya kubeba abiria
na mizigo katika bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya kwa kuwa
kukamilika kwa meli hiyo kutawezesha wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa kusafiri
kwa meli badala ya boti ambazo hazina uwezo wa kukabiliana na dhoruba ndani ya
ziwa hilo.
“Watu wanaposafiri au
kusafirisha mizigo kutoka Mbambabay hadi nchini jirani ya Malawi au kusafiri
ndani ya wilaya ya Nyasa wamekuwa wanapata maafa makubwa kutokana na kukithiri
kwa dhoruba katika ziwa Nyasa hasa kuanzia mwezi Mei hadi Agosti kila
mwaka’’,alisema Jabir.
Kuchelewa kufungwa
kituo cha mafuta katika eneo la Kilosa wilaya ya Nyasa kunatokana na taarifa
potofu ambazo zilisambazwa na kituo
kimoja cha luninga kuwa eneo la ujenzi wa kituo hicho lina mgogoro jambo ambalo
limekwamisha mchakato mzima wa ujenzi wa kituo hicho ambao umekwama hadi sasa
huku wananchi wakiendelea kuteseka na kuangamia kwa kukosa huduma ya kituo cha
mafuta.
Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Alto Komba amekemea tabia ya baadhi ya waandishi
wa habari kuandika habari potofu ambazo zinasababisha kudidimiza maendeleo na
amependekeza waandishi wanaoandika habari potofu ili zionekane kuwa sahihi
waache tabia hiyo badala yake wafuate
sheria,kanuni na weledi wa kazi zao.
Halmashauri ya wilaya
ya Nyasa tangu Julai mosi,2013 haina kituo hata kimoja cha mafuta ingawa
Halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kufuata mafuta ya
petroli na dizeli wilaya jirani ya Mbinga kwa ajili ya shughuli za maendeleo
pamoja na huduma kwa wananchi.
Komba anasema wilaya hiyo inakabiliwa na ongezeko kubwa la
watu ambalo linakwenda sanjari na mahitaji makubwa ya mafuta kwa ajili ya
magari,pikipiki na vyombo vya majini hivyo kufungwa kituo cha mafuta walau
kimoja ni jambo ambalo halina mjadala.
“Halmashauri ya Nyasa
inakusudia kutwaa ardhi katika eneo la Kilosa Juu lenye mchoro wa mipango miji wenye namba TP DRG namba 09/NYS/
29/04/2014 kwa ajili ya ujenzi wa kituo
cha mafuta,mfano tarehe 19/9/2013
ulifanyika mkutano na wananchi wa Kilosa kwa ajili ya ushirikishwaji
katika kuandaa mchoro huu’’,alisema.
Kwa mujibu wa Komba
Aprili pili,2014 rasimu ya michoro hiyo iliwasilishwa kwenye kikao cha kamati
ya huduma za uchumi na mazingira
kilichokaa katika ukumbi wa shule ya msingi Mbambambay na hatimaye kwenye
Baraza la madiwani la Aprili 24,2014.
Amesema baada ya
kupitia mchakato huo Aprili 22,2014 rasimu ya michoro hiyo ilipitishwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa
wa Ruvuma na hatimaye Aprili 30,2016 rasimu ya mchoro huo iliidhinishwa na
mkurugenzi wa mipango miji wizara ya ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi na
kukoma kuwa rasimu na badala yake kuwa
sheria.
Hata hivyo katika
kusudio la kutwaa ardhi ya Kilosa yenye
ukubwa wa ekari moja na nusu kwa ajili ya matumizi ya kituo cha
mafuta,ushirikishwaji wananchi ulikuwepo ambapo Machi tisa mwaka huu ulifanyika
mkutano na wananchi kueleza azma ya Halmashauri kuhitaji kulipa fidia eneo la
Kilosa ili kujenga kituo cha mafuta.
“Wananchi walikubali
lakini Machi 19,2016 wananchi hao walionekana kwenye chombo cha habari cha ITV
kupitia mwandishi wake anayewakilisha Ruvuma wakidai wameingiliwa kwenye maeneo
yao kinguvu na kuwataka wahame ndani ya siku 14 jambo ambalo ulikuwa upotoshaji
mkubwa’’,alisema Komba.
Mwenyekiti huyo wa
Halmashauri ya Nyasa ameyataja madhara ambayo yamesababishwa na taarifa potofu
katika chombo hicho cha habari kuwa ni
hali ambayo inakwamisha mchakato wa kufunga kituo cha mafuta katika eneo
la Kilosa hivyo wananchi wa wilaya ya Nyasa kuendelea kuteseka.
Ametolea mfano
wananchi wa Likwilu juu kata ya Kilosa walikubali eneo lao kuandaliwa ramani ya
mipango miji kwa ajili ya kituo cha mafuta,hata hivyo baada ya habari hiyo
potofu baadhi ya wananchi walishawishika kusema kuwa wataalam wa ramani walifukuzwa Kilosa na
wameamua kukimbilia kitongoji cha Likwilu hivyo wanasambaza taarifa zinazowafanya
wananchi wengine wasikubali maeneo ya kuandaliwa ramani.
Amesisitiza kuwa
taarifa potofu kwa wananchi wa Kilosa
zimesababisha wananchi kukosa imani na serikali yao katika mambo ambayo ni
uzushi.
Kikao cha Baraza la
madiwani katika Halmashauri ya Nyasa kilipitisha maazimio ya kuchukuliwa
hatua na kufikishwa kwenye kamati ya maadili diwani yeyote ambaye
atabainika kushiriki katika uchochezi uliosababisha kuchelewa mchakato wa
kukamilisha eneo la kufungwa kituo cha mafuta Kilosa.
Makamu mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Charles Chawila ameshauri mgogoro huo upatiwe
ufumbuzi haraka ili kituo cha mafuta katika eneo la Kilosa ufanyike haraka kwa
kuwa mchakato ulifikia hatua nzuri ikiwemo ya
kuwalipa fidia wananchi ili kupisha ujenzi wa kituo hicho.
Diwani wa kata ya
Lipingo Halmashauri ya Nyasa Cathbert
Ngwata amesema madiwani wa kata zote
wanaunga mkono ujenzi wa kituo cha mafuta Kilosa ili kukabiliana na kero ya
mafuta inayowakabili wakazi wa wilaya hiyo tangu mwaka 2013.
Kwa upande wake
mbunge wa jimbo la Nyasa na Naibu waziri wa elimu,sayansi,teknolojia na ufundi
Injinia Stella Manyanya amewaasa wenyeji wa wilaya hiyo kuacha kuweka masharti
magumu kwa wawekezaji kama ilivyo kwa mwekezaji wa kituo cha mafuta Kilosa.
“Mazingira ya
uwekezaji katika wilaya ya Nyasa bado ni magumu,nawaomba wakazi wa nyasa kuwapa
ushirikiano wa kutosha wawekezaji wanaojitolea kuwekeza katika mazingira magumu
,serikali itaendelea kutoa mafunzo ya uwekezaji kwa katika vijiji vya kata zote za Nyasa ili
kuepusha migogoro dhidi ya
wawekezaji’’,alisema Manyanya.
Hata hivyo Manyanya
ambaye pia ni diwani alisema taratibu zote zimefuatwa katika mchakato wa ujenzi
wa kituo cha mafuta na kuwaasa wananchi
kutambua kuwa ardhi sio mali ya mtu binafsi hivyo ameshauri hatua za kisheria
zichukuliwe kwa wote wanaokataa kulipwa fidia ili kupitisha ujenzi wa kituo
hicho cha mafuta.
“Natoa mwito kwa
Halmashauri wakati mwingine fanyeni maamuzi magumu ili kusimamia sheria
zilizopo na hasa kuwabana wananchi wanaouza mafuta kwenye ndoo kwa kuwa sheria
ya EWURA hairuhusu kabisa kuuza mafuta kwenye vidumu au ndoo badala yake waunge
mkono mchakato wa kufungua kituo cha mafuta katika wilaya ya Nyasa ambacho
kitakuwa mkombozi wa wananchi wote’’,alisisitiza Manyanya.
Mwisho

No comments:
Post a Comment