Tuesday, June 21, 2016

Songea mfano wa kuigwa usafi wa mazingira

Usafi unafanyika kila siku

 Na Stephano Mango
Usafi wa Mazingira unaofanyika kila siku  katika manispaa ya Songea kuanzia mwaka huu umeufanya mji huo kuwa kuvutia wengi na kuwa msafi  kuliko kipindi kingine chochote cha uhai wa manispaa hiyo.

Utafiti umebaini kuwa manispaa ya Songea ambayo ndiyo kioo cha mkoa wa Ruvuma inaongoza kwa usafi ukilinganisha na Halmashauri nyingine za mkoa huo ambazo ni Halmashauri za Songea manispaa, Halmashauri ya wilaya ya Songea, Tunduru, Namtumbo, Madaba, Nyasa,Halmashauri ya Mbinga  na Mbinga mji.

Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo amesema tangu kutolewa kwa agizo la usafi wa mazingira na sasa sheria ya usafi  wa mazingira katika nchi nzima kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi  kumeongeza moyo wa kujituma kwa wakaziwa manispaa hiyo hivyo kuweka viunga vya mji  huo katika hali ya usafi wakati wote.Amesema licha ya manispaa ya Songea kukabiliwa na changamoto ya uzalishaji taka nyingi kutokana na ongezeko kubwa la watu ambao ni zaidi
ya watu 203,309,,idara ya afya inafanya kazi ya ziada kuhakikisha mji huo unaendelea kuwa safi hasa kutokana na ukweli kuwa Songea ndiyo kioo cha mkoa wa Ruvuma.

Midelo amesema uongozi wa Halmashauri ya manispaa ya Songea umesikitishwa na upotoshaji uliofanywa hivi karibuni na televisheni moja binafsi kupitia mwandishi wake wa mkoa wa Ruvuma akidai kuwa uchafu umekithiri katika manispaa ya Songea jambo ambalo sio taarifa sahihi.

“Kila mmoja ni shahidi ukitembelea katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea,mazingira yake ni ya kuvutia,usafi unafanyika kila siku,magari ya takataka yanasomba,ukisema mji wa Songea ni mchafu ni udanganyifu wa hali ya juu’’,alisisitiza Midelo.

Ametoa wito kwa wanahabari nchini kufanya kazi zao kwa mujibu wa maadili,kanuni na sheria za uandishi wa habari kwa kuwa ni kosa kubwa kwa mwandishi kuandika habari ambazo za upotoshaji kwa kuwa wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Manispaa ya Songea katika kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi,Midelo anasema Halmashauri imeamua kutumia makampuni kwa ajili ya kusimamia shughuli za usafi wa mazingira ili kuhakikisha kuwa mji wa Songea unaendelea kuwa safi wakati wote.

Amesema tayari Baraza la madiwani la manispaa hiyo kwa pamoja wameunga mkono na kuidhinisha shughuli za usafi wa mazingira ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea zifanywe kwa kutumia makampuni ili kuongeza kasi ya usafi wa mazingira.

Hata hivyo amesema Baraza hilo limekubali viwango vya adhabu itakayotokana na wachafuzi wa mazingira  iwe kwa mujibu wa Sheria ndogo ya usafi wa mazingira ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ya mwaka 2015.

Kulingana na tangazo la serikali Namba 308 la mwaka 2015, viwango vya utozaji faini kwa kila mkosaji vitafuata Sheria ndogo ya mwaka 2015 ambayo inatamka mkosaji kulipa faini ya papo kwa papo isiyopungua Shilingi 50,000 na akifikishwa mahakamani atalipa faini isiyopungua Shilingi 100,000.

Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas  Gama ambaye amewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro alieleza kuwa Manispaa ya Moshi imefanikiwa kwenye zoezi la usafi baada ya kutumia Kampuni ambayo ndiyo inawajibika kwa Halmashauri.

Baraza la madiwani la manispaa ya Songea limeshauri uwekwe mkakati wa kuwadhibiti wachafuzi wa mazingira kwa kutumia kikundi cha askari wa usafi wa mazingira ambao watatoza faini za papo kwa papo mara wamkamatapo aliyechafua eneo lolote.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Songea akiwemo Anna Komba na Joseph Ngonyani wamefurahia hatua iliyochukuliwa na Baraza la madiwani wa manispaa ya Songea ambapo wamesema  imebadilisha mji wa Songea kuonekana msafi na kuvutia wakati wote ukilinganisha na hali ya miaka ya nyuma.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment