Halmashauri ya
manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imefikia asilimia 98 katika utengenezaji wa
madawati hadi kufikia Juni 20 mwaka huu.
Ofisa habari wa
manispaa hiyo Albano Midelo amesema manispaa hiyo katika kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kumaliza kero ya
madawati inaendelea kutengeneza na kukamilisha madawati 5,130 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 333.45 ambayo
yanahitajika katika manispaa ya Songea.
Hata hivyo amesema hadi
kufikia mwezi Juni Madawati yote
yaliyokwisha tengenezwa ni zaidi ya 5000 kati ya madawati 5130 ambayo sawa na
zaidi ya asilimia 98 ya mahitaji ya
madawati yote katika manispaa hiyo.
Kaimu afisa elimu wa manispaa ya Songea Sunday Wahyungi amesema Mradi
wa madawati katika manispaa hiyo ulianza tangu mwezi wa Desemba mwaka 2015 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania iliyowataka
Wakuu wa Mkoa,Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha kuwa hakuna
wanafunzi wanaokaa chini hadi kufikia Juni 30 mwaka huu.
Wahyungi
amesisitiza kuwa kabla ya Juni 30 hakuna mwanafunzi ambaye atakaa chini katika
shule za msingi za manispaa hiyo kwa kuwa madawati yote yaliopangwa kukamilisha
mradi wa madawati yatakuwa yametengezwa hivyo uhaba wa madawati katika manispaa
ya Songea kubakia kuwa historia.
Kwa upande wake mkuu
wa wilaya ya Songea Benson Mpesya amesisitiza kuwa hadi kufikia Juni 25 mwaka
huu miradi yote ya madawati katika wilaya hiyo itakuwa imekamilika hivyo
kumaliza kabisa tatizo la baadhi ya wanafunzi katika shule kukaa chini kutokana
na upungufu wa madawati.
Mpesya ambaye pia ni
kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma amesema wilaya ya Songea imefikia hatua nzuri ya
utengenezaji wa madawati ambapo hati kufikia Juni 22 miradi yote ya madawati itakuwa
imekamilika katika manispaa ya Songea.
Amezitaja wilaya
nyingine za mkoa wa Ruvuma ambazo utengenezaji wa madawati umefikia zaidi ya
asilimia 80 kuwa pamoja na
Namtumbo,Mbinga,Nyasa na Tunduru na kwamba taarifa alizonazo ni kwamba hadi
kufikia Juni 28 miradi ya madawati katika wilaya zote itakuwa imekamilika.
Amewaagiza watendaji
katika ngazi zote katika mkoa wa Ruvuma kusimamia zoezi la utengenezaji wa
madawati yaliobakia kabla ya Juni
30 ili kuhakikisha kuwa kuanzia mwezi
Julai mwaka huu tatizo la madawati katika shule za mkoa wa Ruvuma ibakie kuwa
historia.
Mwisho


No comments:
Post a Comment