Sunday, June 19, 2016

Songea yafikia zaidi ya asilimia 95 utengenezaji madawati

Hadi Juni 25 hakutakuwa na mwanafunzi anayekaa chini

NA KWIRINUS MAPUNDA,SONGEA

Halmashauri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imefikia asilimia 95 katika utengenezaji wa madawati hadi kufikia Juni 8 mwaka huu.
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa George Mbijima

Ofisa habari wa manispaa hiyo Albano Midelo amesema manispaa hiyo katika kutekeleza agizo  la Rais John Magufuli la kumaliza kero ya madawati inaendelea kutengeneza na kukamilisha madawati 5,130 yenye thamani ya  zaidi ya shilingi milioni 333.45 ambayo yanahitajika katika manispaa ya Songea.

Hata hivyo amesema hadi kufikia wiki ya kwanza ya mwezi Juni  Madawati yote yaliyokwisha tengenezwa ni 4830 kati ya madawati 5130 ambayo
sawa na asilimia 94.2 ya mahitaji  ya madawati yote.

Amesema Juni 8 mwaka huu kiongozi wa  mbio za mwenge kitaifa  George Mbijima alikabidhi madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 6.5 katika Shule ya msingi Luhira mchanganyiko ambayo ni miongoni mwa shule 81 za Serikali na binafsi zilizopo katika Manispaa ya Songea.

“Shule  hiyo ni ya Mchanganyiko ina Wanafunzi wa kawaida 2031 kati yao Wanaume 991,wanawake 1040. Shule ina Wanafunzi  wenye ulemavu wa macho wapatao 40 kati yao wanaume 18,wanawake 22 hivyo madawati hayo yamemaliza kero ya madawati katika shule hiyo ilioanzishwa mwaka 1928 ambayo pia waziri mkuu mstaafu hayati Rashid Kawawa alisoma’’,alisema.

Kaimu afisa elimu wa manispaa ya Songea Sunday Wahyungi amesema Mradi wa madawati katika manispaa hiyo ulianza tangu mwezi wa Desemba mwaka 2015  ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania iliyowataka  Wakuu wa Mkoa,Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha kuwa hakuna wanafunzi wanaokaa chini hadi kufikia Juni 30 mwaka huu.

Wahyungi amesisitiza kuwa kabla ya Juni 30 hakuna mwanafunzi ambaye atakaa chini katika shule za msingi za manispaa hiyo kwa kuwa madawati yote yaliopangwa kukamilisha mradi wa madawati yatakuwa yametengezwa hivyo uhaba wa madawati katika manispaa ya Songea kubakia kuwa historia.



Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Songea Benson Mpesya amesisitiza kuwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu miradi yote ya madawati katika wilaya hiyo itakuwa imekamilika hivyo kumaliza kabisa tatizo la baadhi ya wanafunzi katika shule kukaa chini kutokana na upungufu wa madawati.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri zote tatu zinazounda wilaya ya Songea ambazo ni Songea manispaa,Halmashauri ya Songea pamoja na Halmashauri ya Madaba amewaagiza watendaji katika ngazi zote kusimamia zoezi la utengenezaji wa madawati yaliobakia  kabla ya Juni 25 ambayo  inatarajiwa kuwa siku maalum ya kutoa taarifa ya kumaliza utengenezaji wa madawati katika wilaya ya Songea.

Mwisho


No comments:

Post a Comment