Saturday, June 11, 2016

Vipaumbele kumi vitakavyoipaisha manispaa ya Songea

Vipaumbele hivyo vimepitishwa na Baraza la madiwani la manispaa

Na Stephano Mango

Manispaa ya Songea iliyopo mkoani Ruvuma ni miongoni mwa Halmashauri nchini ambazo zimeweka dhamira ya kuhakikisha inaweka mikakati ya kuboresha maisha ili kuendana na kasi ya Rais wa awamu ya tano ya kujenga Tanzania mpya yenye neema.


Afisa habari wa manispaa hiyo Albano Midelo anasema Baraza la madiwani likiongozwa na mstahiki Meya  Abdul Hassani Mshaweji kwa kushirikiana mkurugenzi wa manispaa hiyo Jenifer Omolo pamoja na wataalam katika idara zote  wameweka maeneo kumi ya vipaumbele yatakayoiwezesha manispaa hiyo kupaa.

Kwa mujibu wa afisa habari huyo Halmashauri ya manispaa  imeangalia maeneo
ya msingi katika kuboresha  na kuimarisha utoaji wa huduma kwa kuyapa uzito maeneo hayo ili kukabiliana na  changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Halmashauri.

Vipaumbele ambavyo vimepitishwa na Baraza la madiwani la Halmashauri ya manispaa ya Songea katika bajeti ya mwaka 2016/2017 vimelenga katika Sekta ya Elimu ambapo Halmashauri imejiwekea malengo katika kuboresha huduma za jamii hasa katika kuboresha miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari kwa kukamilisha miradi viporo na kujenga miundombinu mipya.

Katika Baraza la madiwani ambalo mbunge wa jimbo la Songea Leonidas Gama anashiriki kama diwani limeyataja Maeneo yatakayozingatiwa katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa,maabara,mabweni,vyoo, ukarabati wa madarasa ununuzi wa samani pamoja na mishahara ya watumishi.

Sekta ya Afya  ni miongoni mwa vipaumbele vilivyopitishwa na Baraza hilo Lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya Vituo vya Afya na Zahanati kwa kuendeleza ujenzi na upatikanaji wa dawa. Maeneo muhimu ni ujenzi wa zahanati, ukarabati, ujenzi wa chumba cha upasuaji, samani na ununuzi wa madawa.
Jenifer Omolo mkurugenzi wa manispaa ya Songea

Afisa habari huyo amekitaja kipaumbele kingine ambacho kimewekwa na manispaa ya Songea kuwa ni Sekta ya Maji  Lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa maji ya kutosha katika maeneo ya pembezoni ya Manispaa kwa kujenga visima vya maji  virefu na vifupi, kuanzisha uvunaji wa maji ya mvua na kuanzisha mtandao wa maji ya bomba.

Sekta ya ujenzi pia imepewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo manispaa ya Songea imejiwekea lengo la kuboresha miundombinu ya barabara kwa kufanya matengenezo ya mara kwa mara, maeneo korofi na matengenezo ya kawaida.

Bajeti hiyo pia imeadhimia kujenga dampo la kisasa, kujenga kituo kuu ya mabasi ya kwenda mikoani, kujenga maeneo ya maegesho ya malori pikipiki,magari madogo na taksi, kujenga vivuko na Madaraja, kuweka taa za barabara na ujenzi wa masoko kila kata.

Kipaumbele pia kimewekwa katika Sekta ya Kilimo,Uvuvi Mifugo na Ushirika Lengo likiwa  ni kuendeleza kilimo bora na endelevu kwa kutumia pembejeo za kisasa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Manispaa ya Songea imedhamiria kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, mafunzo kwa wakulima huduma za ugani na vituo vya mafunzo na Kuendeleza ufugaji wa ndani hasa Mradi wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe ambao utasaidia kuongeza kipato kwa wananchi.

Sekta ya Mipango Miji, Ardhi na Maliasili  ni miongoni mwa vipaumbele vilivyopitishwa katika bajeti lengo likiwa ni kuboresha makazi ya wananchi kwa kuongeza upimaji wa viwanja, na ulipaji wa fidia kuboresha maeneo yaliyoendelezwa kiholela ambayo yamesababishwa na uhaba wa viwanja vilivyopimwa.

“Manispaa ya Songea imedhamiria kutoa hati miliki za ardhi, kuandaa michoro ya Mipangomiji, upandaji wa miti, utunzaji wa mazingira, utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji na utengaji wa maeneo kwa ajili ya ujasiriamali na kutenga maeneo kwa ajili ya utalii wa ndani na uwekezaji mkubwa’’,alisema afisa habari huyo.
Abdula Hassan Mshaweji mstahiki Meya wa manispaa ya Songea

Kwa kuzingatia kuwa kila kitu kinahitaji Utawala bora,manispaa ya Songea imejiwekea malengo katika kuboresha mazingira ya kufanyia kazi watumishi katika sekta ya Utawala, Mipango na Biashara pamoja na utoaji wa huduma kwa Wananchi wa Manispaa.

Ili kuendana na Ulimwengu wa  Sayansi na teknolojia,Manispaa ya Songea imepanga kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ya teknohama (ICT) kwa kutumia mifumo mipya ya mitandao na kutoa mafunzo ya upangaji mipango bajeti, utunzaji wa takwimu kwa mfumo wa LGMD na  IPSAS.

Manispaa hiyo pia inatoa elimu kuhusu utatuzi wa migogoro sehemu za kazi,utatuzi wa kero wa wananchi, mafunzo ya sheria mbali mbali zinazohusu mikataba, utumishi  elimu ya ujasiriamali na mkataba kwa mteja.

Masuala Mtambuka ambayo yamepewa kipaumbele katika manispaa ya Songea ni pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya maradhi mbalimbali kama UKIMWI, Malaria Kifua Kikuu na kushughulikia masuala ya UKIMWI, magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele,Mazingira na kupambana na Madawa kulevya na rushwa.

Kuhusu kipaumbele cha Uchumi na Biashara manispaa ya Songea imedhamiri kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa bidhaa na kukuza soko, kuanzisha miradi yenye tija, standi na masoko kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia njia ya kielektroniki, kuongeza maeneo ya uzalishaji, biashara na utoaji mikopo mbalimbali kwa mtu mmoja mmoja na vikundi.

Sekta ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto pia ni miongoni mwa vipaumbele katika manispaa ya Songea lengo likiwa ni kutoa elimu ya ujasiliamali na elimu ya kutumia raslimali asilia katika masuala ya maendeleo,kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya mikopo,ujasiriamali,raslimali asili kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Wazee kwa maendeleo.

 Ili kutekeleza vipaumbele vilivyotajwa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, inakadiria kutumia zaidi ya shilingi bilioni. 55.

Hata hivyo kwa Mwaka 2016/2017 Manispaa ya Songea inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi  bilioni  55 kutoka vyanzo mbali mbali vya mapato. Makisio haya ni sawa na ongezeko la zaidi ya  shilingi bilioni 11 sawa na asilimia 21.5 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2015/2016 ambapo lengo  lilikuwa ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni  43.


mwisho

No comments:

Post a Comment