Sunday, October 9, 2016

Kituo cha Afya Mjimwema kuwa Hospitali ya Wilaya


Majengo mengi yamekamilika
HALMASHAURI ya manispaa ya Songea  imepitisha ombi la kituo cha afya cha mji mwema kupandisha hadhi kuwa hospitali ya Halmashauri ya manispaa hiyo.
Afisa habari wa manispaa hiyo Albano Midelo alisema Ombi hilo liliwasilishwa katika Baraza la madiwani ili Halmashauri iridhie hatua nyingine ziendelee  hatimaye Halmashauri ya manispaa hiyo iwe na Hospitali ya Wilaya.
Hata hivyo alisema ombi  la kupandisha hadhi Kituo hicho cha afya lilikuwa ni  agizo la waziri wa afya,ustawi wa jamii,jinsia,watoto na wazee Ummy
Mwalimu alipotembelea kituo hicho Januari 11 mwaka huu.

Alisema Waziri Mwalimu aliagiza Ombi la kupandisha hadhi Kituo cha Afya Mjimwema kuwa Hospitali ya Wilaya liwasilishwe Wizara  ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee  ili kupata idhini ya Wizara yenye dhamana.

Afisa habari huyo alisema kikao cha Baraza la madiwani kikiongozwa na Mstahiki Meya Abdul Hassan Mshaweji kilipokea w taarifa na kikao kiliidhinisha  upandishaji hadhi Kituo cha Afya Mjimwema kuwa Hospitali ya Halmashauri ya manispaa.

Amelitaja lengo la kuwa Hospitali ya Wilaya ni kuboresha huduma mbalimbali za afya ambazo hazipatikani kwenye Kituo cha Afya na sababu za msingi kuomba kuwa Hospitali ya Wilaya ni kuiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuwa na Hospitali ya Wilaya ambayo itaweza kuhudumia wananchi wa Manispaa na wale wanaotoka Kata na Wilaya za pembezoni

Kituo cha Afya Mjimwema kilianzishwa Aprili 8,2002 ambapo Kituo hicho kinahudumia wakazi wanaokadiriwa kufikia 31,091 kati ya hao 1213 ni watoto chini ya mwaka mmoja, 5845 ni watoto chini ya miaka mitano, 1275 ni wajawazito wanaotegemewa na 7586 ni wanawake walio na umri wa kuzaa.

Alisema Kituo cha afya cha Mjimwema kina majengo nane  yakiwemo Jengo la wagonjwa wa nje, Wodi ya Watoto na Wanawake, Wodi ya Wazazi na huduma za kujifungua, jengo la kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto na wodi ya Wanaume, jengo la Utawala, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba mbili za watumishi na jengo la upasuaji.

Kulingana na ofisa habari huyo,Kituo cha Afya Mjimwema kina jumla ya watumishi 110 wa kada mbalimbali na kwamba Kituo kinatoa huduma mbalimbali za afya.

Hata hivyo alizitaja huduma ambazo hazitolewi katika kituo hicho cha afya kuwa ni pamoja na  Huduma ya upasuaji licha ya kwamba jengo limekamilika lakini vifaa bado havitoshelezi kuanza huduma hiyo,huduma nyingine ambazo hazitolewi ni huduma za macho, huduma za kuongeza damu, huduma za pua, masikio na koo na huduma ya mionzi yaani ultrasound.

Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina vituo 30 vinavyotoa huduma za afya ambavyo ni Hospitali moja, Vituo vya Afya vitatu vikiwepo viwili vya Serikali na kimoja cha Shirika la Dini na Zahanati 26 Kati ya hizo Zahanati 19 zinamilikiwa na Serikali, zahanati mbili zinamilikiwa na Mashirika ya Dini, na zahanati nne  zinamilikiwa na watu binafsi ambapo Zahanati moja inamilikiwa na UMATI.
Mwisho

1 comment:

  1. Udah punya Asuransi belum? Pasti belum, iya kan. Yuk baca artikel berikut Asuransi Kendaraan MSIG, Berkendara Tanpa Cemas kali aja setelah baca artikel berikut langsung kepincut beli asuransi. Asuransi itu penting loh.

    ReplyDelete