Sunday, October 9, 2016

Maji ya Ziwa Nyasa yanaendelea kuchafuliwa

Na Albano Midelo

Mito inayomwaga maji imechafuliwa

MADINI ya mkaa wa mawe yaliolundikwa na Kampuni ya TANCOAL katika Kijiji cha Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoa wa  Ruvuma bado  yanaendelea kuingia ziwa Nyasa hali ambayo inasababisha uchafuzi wa maji katika ziwa hilo.

Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ndumbi Rajabu Abdallah anasema licha ya kampuni hiyo binafsi ya uchimbaji madini kuyaweka madini hayo mbali na eneo la ziwa bado wakati wa mvua za masika chembechembe za madini hayo zinasombwa na maji kupitia mfereji uliopo jirani na  kuingia hadi ziwa Nyasa.


Abdallah anasisitiza kuwa bado wananchi zaidi ya 2000
wa kijiji hicho wanatumia maji ya ziwa Nyasa licha ya kwamba serikali imeanza mchakato wa kuchimba visima viwili ambavyo bado havijaanza kutumika na wakazi hao wa mwambao mwa ziwa.

Anasema Kampuni hiyo iliahidi kuweka bomba ili wananchi wa Kijiji cha Ndumbi wasiendelee kutumia maji ya ziwa Nyasa,hata hivyo mchakato wa kuweka maji ya bomba umeshindikana baada ya  utafiti kubaini vyanzo vya maji vilivyopo havina maji ya kutosha.

Hata hivyo Abdallah anasema serikali ya Kijiji hicho inaendelea kufanya mawasiliano na uongozi wa Kampuni  ya TANCOAL ambayo imeahidi kuwachimbia visima  wananchi ili wasiendelee kutumia maji ya ziwa Nyasa.

Afisa Mazingira wa Wilaya ya Mbinga Gordon Nkondora anasema Halmashauri iliuagiza uongozi wa Kampuni ya TANCOAL  kuondoa madini yote ya mkaa wa mawe katika kijiji cha Ndumbi na kusisitiza kuwa iwapo bado hawajaondoa,wanafanya makosa kwa kuwa muda waliopewa kuyaondoa ulimalizika na eneo hilo linatakiwa kuwa wazi.



Kampuni hiyo imekuwa ikitumia bandari ya Ndumbi kusafirishia mkaa wa mawe   kupitia ziwa Nyasa kwenda Malawi,Afrika ya kusini na bandari ya Itungi iliyopo Kyela mkoani Mbeya tangu kipindi cha utafiti hadi uchimbaji wa madini hayo.

“Kwa miaka minne mfululizo kuanzia 2011 hadi 2014 maelfu ya tani za mkaa wa mawe umekuwa unasombwa na maji  toka katika eneo jirani na bandari ya Ndumbi hadi ndani ya ziwa Nyasa…’’,anasema mwenyekiti  mstaafu wa Kijiji cha Ndumbi, James Mbawala.

Mary Komba,Jeska Haule na Magreth Challe ni wakazi wa Kijiji cha Ndumbi,wanasema katika kijiji hicho hawana huduma ya maji ya bomba,hivyo wanatumia maji ya ziwa Nyasa kwa matumizi mbalimbali.

Msimamizi wa Kampuni ya TANCOAL katika bandari ya Ndumbi Deo Mapunda  anasema mwaka 2015,Kampuni hiyo iliondoa madini hayo kutoka kando mwa bandari ya Ndumbi na kuyaweka mbali kidogo  na eneo la ziwa ili kukabiliana na mvua za masika ambazo zimekuwa zinayasomba madini hayo hadi ndani ya ziwa na kuleta uchafuzi wa maji.



Baadhi ya wavuvi katika Kijiji cha Ndumbi wanasema kuwa mwaka 2013 kulitokea vifo vya samaki ambavyo wanaamini vilisababishwa na athari za madini ya mkaa wa mawe kuingia katika ziwa Nyasa kupitia bandari ya Ndumbi.



Frank Challe mvuvi wa Kijiji cha Ndumbi anasema samaki wana tabia ya kula takataka zikiwemo chembechembe za madini ya  mkaa wa mawe ambazo zinaingia ndani ya ziwa Nyasa na kwamba anaamini samaki waliokufa waliathirika na  sumu za mabaki ya madini hayo.



Fransis Chuwi mvuvi wa Ndumbi anasema wavuvi walibaini kuwa vifo vya samaki vilivyotokea mwaka 2013 vilianzia  ukanda wa Ndumbi ambako maji ya ziwa yalikuwa yamechafuliwa na madini ya mkaa wa mawe kisha kuenea eneo la Lituhi na maeneo mengine ya mwambao mwa ziwa Nyasa.



Afisa Uvuvi Tarafa ya Ruhuhu Wilaya ya Nyasa  Joseph Mwingira anasema utafiti wa awali ulibaini kuwa samaki waliokufa  na kuelea juu ya maji walionekana kuwa na majeraha ya kubabuka katika sehemu za mwili zikiwemo usoni,tumboni,kichwani,mkiani na mgongoni.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dk.Benjamin Ngatunga  alipinga madai ya wavuvi hao kwamba vumbi na chembechembe za madini ya mkaa wa mawe husababisha vifo vya samaki.

Dk.Ngatunga alisisitiza kuwa wavuvi wanaongea jambo ambalo halijafanyiwa utafiti wa kisayansi ambao TAFIRI imechunguza katika nchi mbili za Tanzania na Malawi na kubaini tatizo la vifo vya samaki katika ziwa Nyasa ni mabadiliko ya mkondo wa maji katika ziwa hilo ambayo hujitokeza kila baada ya miaka kadhaa na sio vinginevyo.

Afisa wa Maji wa Bonde la Ziwa Nyasa Mhaidrojia Witgal Nkondora anasema ziwa Nyasa linapokea tope, udongo na mchanga kutoka katika mito iliyochafuliwa na shughuli za kibinadamu na kusababisha uchafuzi wa mazingira kwa viumbe waliomo kwenye mito na ziwa hilo.

Utafiti umebaini aina mbalimbali za Samaki katika mto Ruhuhu na  ziwa Nyasa wameanza kupungua kwa kuwa samaki hawezi kutaga mayai na kuzaliana kwenye tope  au maji yaliochafuliwa na kemikali za madini yenye sumu.

Kwa mujibu wa Afisa huyo,utafiti uliofanyika mwaka 2007 katika mto Songwe, unaonesha kuwa zaidi ya tani 700,000 za mchanga,udongo na tope zilisombwa na kuingia katika ziwa Nyasa hali ambayo inatishia usalama wa ziwa hilo.

“Ninaamini mwaka huu utafiti  mwingine ukifanyika katika mito inayomwaga maji ziwa Nyasa ukiwemo mto Ruhuhu huenda mchanga na udongo ulioingia katika ziwa Nyasa utafikia mamilioni ya tani,ikumbukwe utafiti wa awali ulifanyika katika mto mmoja tu bado hatujui katika mito mingine mikubwa zaidi ya minane inayoingiza maji katika ziwa hilo ”,anasisitiza Nkondora.

Nkondora anaitaja   mito mitano  inayoongoza kwa kusomba taka zenye sumu,mchanga na tope na kumwaga ndani ya Ziwa Nyasa kuwa ni mto Ruhuhu wenye ukubwa wa mita za mraba13,490,mto Songwe  mita 3,550, mto Rufirio  mita1,350, mto Kiwira mita 1,660 na mto Lumbira mita 1,414.

“Mto Chiwindi uliopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ndiyo unaoongoza kwa kuingiza takataka zenye sumu katika ziwa Nyasa kutokana na uchimbaji wa madini hasa dhahabu ambao unaendelea kufanywa kwenye maeneo ya wilaya za Nyasa na Mbinga’’,anasema Nkondora.

Kulingana na Nkondora, mto Ruhuhu ambao chanzo chake ni mkoa wa Ruvuma na  Njombe umechafuliwa katika kiwango cha kutisha  na maji yake yanaonekana kuwa na tope kwa mwaka mzima kutokana na shughuli za kibinadamu.

Anabainisha uchafuzi wa maji ya mito na ziwa umechangia kuharibu mazalia ya samaki,kuua viumbehai wa majini  na baadhi ya aina za samaki wameanza kutoweka.

Ili kuvitunza na kuvilinda vyanzo vya maji,Nkondora anashauri Baraza la Taifa la Kusimamia Mazingira(NEMC) kutumia sheria mama ya mazingira kukabiliana na Wachimbaji madini  wanaozalisha taka kwenye maji na kutumia kemikali za sumu kusafishia madini.

Julai 28,2010,Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulitoa mkataba ambao ulitamka wazi kwa nchi wanachama ikiwemo Tanzania kuhakikisha inatoa maji safi na salama katika kiwango cha juu kwa wananchi wake ili kulinda afya za watu wake.



Mwanasheria na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira Tanzania (LEAT) Dk.Nshala Rugemeleza anasema sheria mama ya mazingira ya mwaka 2004  kifungu cha 21 inaonesha wazi miradi yote mikubwa inatakiwa kufanyiwa tathmini ya mazingira (EIA) ili kukabiliana na athari za kimazingira.

Hata hivyo Dk.Nshala anasema utafiti umebaini katika maeneo mengi kampuni za uwekezaji zinashindwa kuzishirikisha serikali za vijiji katika hatua zote za tathmini ya mazingira, utafutaji na uchimbaji wa rasilimali kama madini,gesi na mafuta ambapo kisheria wanafanya makosa.

“Sheria inasema wazi wawekezaji hawaruhusiwi kuingia katika eneo la kijiji hata kama wamepewa leseni na wizara, bila kibali cha serikali ya kijiji husika,mwenyekiti wa serikali ya kijiji anatakiwa kutoa ruhusu kwa kampuni  au mwekezaji kwa niaba ya wanajiji’’,anasisitiza Dk.Nshala.

Anazitaja sheria ambazo zinampa uwezo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji kutoa kibali kwa mwekezaji anapofika kutafuta,kuchimba au kuwekeza kuwa ni sheria ya madini ya mwaka 2010,sheria ya serikali za mitaa na mamlaka ya wilaya sura ya 287 na sheria ya ardhi namba nne na tano ya mwaka 1999.

Albano Midelo ni Mwanahabari anayeandikia zaidi masuala ya mazingira


No comments:

Post a Comment