Na Albano Midelo
SISI wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa katika wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma tuna rasilimali nyingi za kipekee vikiwemo vivutio lukuki vya utalii lakini tumesahaulika kwa kila kitu hali ambayo inasababisha kuendelea kuwa maskini.
Ndivyo anavyoanza kwa kusema mkazi wa kijiji cha Njambe mwambao mwa ziwa Nyasa Mariot Linduti ambaye anashauri serikali pamoja na wadau wa utalii kutembelea eneo hilo na kufanya utafiti kuhusu visiwa vya Puulu pamoja na jiwe la kihistoria la Pomonda ambalo lipo takribani meta 300 ndani ya ziwa Nyasa kutoka ufukwe wa bandari ya Liuli.
Lunduti anasema katika jiwe la Pomonda kuna vivutio vingi vya asili vya utalii ambavyo vikiendelezwa vinaweza kusukuma mbele maendeleo ya wakazi wa kata ya Liuli na Kihagara ambazo zinaongoza kwa kuwa na vivutio vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine yeyote duniani.
“Kisiwa kidogo cha Puulu ambacho kinapakana na jiwe la Pomonda ndani ya ziwa Nyasa kina msitu mnene,wanyama adimu kama pimbi na mazingira tofauti na nchi kavu,kisiwa kipo katika mzunguko wa maji,vitu vingi vya asili,kisiwa cha Puulu kinatakiwa kufanyiwa utafiti na watalaamu ili kiweze kuendelezwa,kwa kuwa mwaka 1917 kisiwa hicho walikuwa wanaishi watu wenye ukoma ambao walitengwa ili kuogopa wasiweze kuambukizwa watu wengine hivyo kuna utalii wa kihistoria”,anasema Linduti.
Joseph Ndomondo ni mwongoza watalii kutoka katika kampuni ya Ntembo Tours ambayo inaundwa na vijana takribani 100 ambao wanatoka katika kata za Liuli na Kihagara mwambao mwa ziwa Nyasa anasema eneo la ziwa Nyasa linaruhusu kufanyika utalii wa aina zote ingawa sekta ya utalii katika eneo hilo bado ilikuwa haujapata mwamko wa kipekee kwa miaka mingi.
Ndomondo anasema mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma Injinia Stella Manyanya ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya utalii katika mkoa wa Ruvuma ndiyo ambaye amesimama imara kwa kuhakikisha kuwa sekta ya utalii mwambao mwa ziwa Nyasa sasa inaboreshwa ambapo kwa kuanzia ameanzia kufufua utalii katika kata mbili za Liuli na Kihagara.
“Sisi huku ziwa Nyasa mazingira yetu yanaruhusu kwa utalii tangu muda mrefu,changamoto kubwa iliyokuwa inatusumbua ni tatizo la usafiri wa barabara ambao wakati wa masika hali inakuwa mbaya zaidi ingawa hivi sasa serikali inajitahidi kuhakikisha kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa karibu 220 kutoka Songea hadi Liuli inapitika wakati wote,pia mawasiliano ya simu yanapatikana”,anasema Ndomondo.
Ndomondo ambaye amepata mafunzo ya Tour Guide kutoka Bodi ya utalii Tanzania anasema mara kwa mara amekuwa anawatembeza watalii wa kigeni kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wanatembelea vivutio mbalimbali vikiwemo kuangalia ngoma za mganda,kioda pamoja na kuwapeleka kwa boti katika jiwe la kihistoria la Pomonda lililopo meta 300 kutoka ufukwe wa ziwa Nyasa.
Jiwe la Pomonda ambalo wajerumani walilipa jina la sphinxhaven kutokana na kuwa na vivutio lukuki lipo katika historia tangu vita vya kwanza vya dunia mwaka 1914 hadi 1918 pamoja na vita vya pili vya dunia mwaka 1939 hadi 1945 ambapo wakoloni wa kijerumani na waingereza walitumia pango kubwa ambalo lipo kama ukumbi wenye kubeba watu kati ya 60 hadi 100 hivyo wanajeshi wa kiingereza na kijerumani walitumia jiwe hilo kama sehemu ya kujificha wakati wa mapambano.
“Jiwe la Pomonda pia katika kilele chake ambacho kina urefu wa takribani meta 40 kwenda juu ipo taa maalum kubwa yenye rangi nyekundu ambayo ilikuwa itatumiwa na nchi tatu za Tanzania,Malawi na Msumbuji wakati wa wakoloni wa kijerumani,kireno na waingereza kwa ajili ya alama ya kuongozea meli katika ziwa Nyasa ili wasiweze kupotea wanapotaka kutia nanga kwenye bandari ya Liuli,taa hiyo walikuwa wanaweza kuiona hata wakiwa katika nchi za Malawi na Msumbuji”,anasema Ndomondo.
Vivutio vingine ambavyo vinapatikana kwenye jiwe hilo la kihistoria ndani ya ziwa Nyasa ni kwamba kuna mawe matatu makubwa ambayo wakazi wa eneo hilo wanaamini yamepangwa na mwenyezi Mungu ,huku mpangilio wake ukiwa ni kivutio cha ajabu utadhani yamejengwa na mafundi ujenzi huku yakiwa yameacha njia maalum ambayo unaweza kupita kutokea upande wa pili hali ambayo inawashangaza na kuwavutia wengi.
Jiwe la kihistoria la Pomonda pia ni sehemu muhimu ambayo inafaa kufanya utalii wa kupiga mbizi yaani adventure raping rock kuruka toka juu ya jiwe hadi ziwani umbali wa karibu mita 20 hali ambayo inawavutia watalii wengi kutoka nje ya nchi kwenda mara kwa mara katika jiwe hilo hali ambayo inawafanya wajisikie kana kwamba wapo katika nchi zao ambazo zina maeneo ambayo wameyatengeneza tofauti na eneo hilo la jiwe la Pomonda ambalo ni la asili.
Ndomondo anasema ana vifaa maalum kwa ajili ya kufanya utalii wa kuruka toka juu ya jiwe la kihistoria hadi ziwani,hata hivyo anasema ili kumudu kufanya aina hiyo ya michezo ya kitalii inahitajika kufanya mazoezi ya kutosha ambapo watalii kutoka nje ya nchi walio wengi wanapenda kufanya mchezo huo ukilinganisha na idadi ya watanzania .
Kivutio kingine cha utalii katika jiwe la Pomonda ni kupatikana kwa wingi kwa samaki wa mapambo katika eneo hilo inakadiriwa eneo hilo lina aina zaidi ya 120 wa samaki wa mapambo hivyo mtalii akifika katika jiwe hilo kuna eneo maalumu ambalo anaweza kuvua samaki hao yeye mwenyewe pia anaweza kupika au kupikiwa ugali wa asili wa mhogo ambao ni chakula maalum kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa kuna makampuni ambayo wanaendelea kuwavua samaki hao wa mapambo kama shamba la bibi katika ziwa Nyasa na kwenda kuwauza Ulaya na Marekani kwa bei kubwa huku wenyeji wa kata ya Liuli na maeneo mengine ambako samaki hao wanavuliwa wakibakia mikono mitupu pia serikali inapoteza ushuru halali wa kodi ya samaki hao ambao wanauzwa ulaya kwa bei ya kati ya shilingi za kitanzania 30,000 hadi 40,000 kwa samaki mmoja.
Jiwe la Pomonda ni eneo ambalo linafaa kwa ajili ya kufanyia picnic kwa kuwa lina ukumbi mkubwa ambao umefunikwa vizuri na mwenyezi Mungu tngu kuumbwa kwa dunia kwa mawe hata wakati wa mvua mtalii anaweza kukaa na kuwa salama,pia kuna eneo maalum ambalo linafaa kwa kupigia picha huku mtalii akipata upepo mwananana wa ziwa Nyasa pamoja na kufanya utalii wa kuzunguka maeneo yote ya jiwe hilo kwa kutumia boti maalum.
Martin Ndomba kutoka kikundi cha Ntembo Tours anashauri watalaamu kutoka wizara ya utalii na maliasili kutembelea katika jiwe la kihistoria la Pomonda ili kufanya utafiti zaidi na kubaini vivutio vingine zaidi na hata umri wa jiwe hilo ambalo linafanana na lile lililopo ziwa Viktoria ,pia anasema kuna vivutio vingine ambavyo ni adimu mwambao mwa ziwa Nyasa.
0766463129
http://www.maendeleo/ ni vita.blogspot.com
nimefurahi sana bwana amidelo jinsi unavyojitahidi kuitangaza nyasa kwaujumla hasahasa jiwe la pomonda,kaza buti nasi tupo nyuma yako........james nyiriri
ReplyDeletepia tutangazie milima ya livingstone na maporomoko yake....james nyiriri
ReplyDelete