uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na uchimbaji wa madini katika eneo la Ngembambili wilayani Mbinga 
Na ZIWA Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbuji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500 toka usawa wa bahari ambapo kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750,urefu wake ni karibu kilometa 1000 na upana mkubwa ni kilometa 80 ambapo upana mdogo ni kilometa 15.
Bonde la ziwa Nyasa linajumuisha eneo lote lenye mito ,ambayo inatiririsha maji kuingia katika ziwa Nyasa, mito hiyo inatoka katika wilaya 11 za mikoa ya Mbeya,Iringa na Ruvuma .
Wilaya zinazounda Bonde la maji la ziwa Nyasa ni pamoja na wilaya za Songea,Mbinga na Namtumbo mkoani Ruvuma,wilaya za Ileje,Mbozi,Kyela,Mbeya na Rungwe mkoani Mbeya na wilaya za Ludewa,Njombe na Makete mkoani Iringa.
Ofisa wa Maji katika Bonde la ziwa Nyasa Witgal Nkondola anasema Bonde hilo lina jumla ya wakazi 2,060,000 kutokana na sensa ya mwaka 2002 ambapo wananchi hao walio wengi wanaendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo hali inayosababisha kuharibu mazingira.
Nkondola anabainisha zaidi kuwa maeneo hayo kuzunguka Bonde la ziwa Nyasa yanapata mvua nyingi kwa wastani kati ya milimita 1000 na 2500 kwa mwaka, mito yote sehemu ya Tanzania inachangia zaidi ya asilimia 53 ya maji yote ya ziwa Nyasa.
Pia jamii inatakiwa kutunza mazingira yanayozunguka vyanzo vya maji na kuvifanya kuwa endelevu na safi kwa kupanda miti rafiki ya maji na kuepuka kufanya shughuli za kilimo na mifugo na kazi nyingine ambazo zinachangia kuharibu mazingira.
Ofisi ya Bonde la maji ziwa Nyasa imeweka mikakati ya kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa aina yeyote kwa lengo la kufanya rasilimali ya maji haitoweki katika bonde la ziwa Nyasa na hivyo kuathiri viumbehai.
Hata hivyo kuna changamoto mbalimbali katika Bonde la ziwa Nyasa ambapo Afisa wa maji Bonde la ziwa Nyasa anazitaja changamoto hizo kuwa ni uharibifu mkubwa wa mazingira na uchafuzi wa kutisha katika vyanzo vya maji ambao unafanywa na wananchi wanaozunguka katika bonde hilo kwa kuendesha shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Hata hivyo Nkondola anasema maji salama huitwa yamechafuliwa endapo viasili vitakavyokuwa ndani ya maji,vinaweza kusababisha madhara ya kiafya au kiuchumi kwa binadamu na viumbehai au hata kufanya maji hayo kuonekana hayana muonekano wa asili yaani yanakuwa na rangi au mtibuko au matope.
Anabainisha kuwa kuna njia mbalimbali zinazoweza kusababisha uchafuzi wa maji ambazo anazitaja kuwa ni pamoja na uchafu toka viwandani,kemikali za kilimo,matumizi holela ya ardhi na kilimo cha kuhamahama.
Njia nyingine za uchafuzi wa mazingira kulingana na Kaimu Afisa huyo wa maji Bonde la ziwa Nyasa ni utupaji wa hewa chafu,utupaji holela wa maji taka ya majumbani,uharibifu wa njia asili,ongezeko la mifugo,ongezeko la watu na uchimbaji wa madini kiholela.
“Kama ilivyo katika mabonde mengine ya maji nchini, Bonde la ziwa Nyasa limeathirika sana katika mazingira yake kutokana na shughuli za kilimo kisichokuwa endelevu na kisichozingatia utaalamu na wachimbaji wadogo wadogo wa madini hasa katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ”,alisema.
Anasisitiza kuwa kwa ujumla shughuli za kujitafutia riziki kwa wananchi waishio na wasioishi katika bonde la ziwa Nyasa kumeathiri hali ya mazingira ya bonde la ziwa Nyasa katika kiwango cha kutisha.
Hata hivyo anakiri kuwa ni kazi ngumu kuwathibiti wananchi wajasiriamali wasifanye shughuli za kuwaingizia kipato katika maeneo yao na kwamba ambacho kinawezekana kufanyika hivi sasa ni kutoa elimu na njia bora za kitaalamu za uchimbaji wa madini bila kuharibu vyanzo vya maji na mazingira yake kwa ujumla.
Changamoto nyingine katika Bonde la ziwa Nyasa kwa mujibu wa Nkondola ni athari za uchafuzi wa maji ambapo binadamu na wanyama wanapokunywa maji yaliyochafuliwa na wanapotumia mimea huweza kupata madhara ya kifya ambapo viumbe kama samaki na viumbe wengine huweza hata kupoteza maisha kutokana na uchafuzi huo wa maji.
Uchafuzi wa maji unaweza kusababisha binadamu kupata magonjwa mbalimbali kama kuhara, kipindupindu, kichocho, figo na kansa ya ngozi na homa za matumbo.
Licha ya umuhimu mkubwa wa maji,vitendo vya binadamu katika mazingira vinaweza kufanya maji kuwa na athari katika mazingira zikwemo mmomonyoko wa udongo,upotevu wa rutuba,mafuriko na kutuama kwa maji.
Mmomonyoko wa udongo hutokea pale ambapo udongo unapohamishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kwamba mmomonyoko hufanyika kwa urahisi zaidi kwenye ardhi isiyokuwa na uoto hasa ile iliyo kwenye mwinuko wa maeneo ambayo shughuli za kibinadamu hufanyika kama uchimbaji holela wa madini na kilimo holela.
Vitendo vya binadamu kuharibifu mazingira ndiyo huleta athari mbaya ikiwa ni pamoja na kusababisha mmomonyoko wa udongo ,vitendo hivyo ni kama kukata miti ovyo kwenye vyanzo vya maji,kuchoma moto misitu na mapori na kulima kwenye vyanzo,kandokando ya mito na ndani ya mito.
Vitendo vingine vya uharibifu huo ni kuchimba ovyo mchanga na mawe kwenye mito,matumizi mabaya ya madawa ya kilimo,utupaji wa maji taka mitoni,uchimbaji holela wa madini na hasa kutumia kemikali za hatari kama zebaki ambazo ni hatari zikiingia kwenye vyanzo vya maji bila kusahau kufuga wanyama wengi kuliko malisho yaliopo.
Utunzwaji na ulinzi wa vyanzo vya maji ni jukumu la kila mwenye haki ya kutumia maji,uhamasishaji jamii ufanyike,ukishirikisha wadau wote ambao utasaidia kuleta mabadiliko ya kitabia katika utunzaji wa mazingira.
Iwapo athari za uchafuzi wa maji zitapungua basi umaskini nao utapungua katika kiwango kikubwa kwa kuwa muda mwingi wananchi watatumia katika shughuli za uzalishaji mali ,isipokuwa sheria itabaki kuwabana wale wote wanaoharibu kwa makusudi vyanzo vya maji.
Jambo la kuzingatia hapa ni elimu ya namna ya kutunza na kuzitumia rasilimali za maji na kwamba wananchi hawana budi kudhibiti uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa aina yeyote.
Ni lazima kuhakikisha vyanzo vya maji vilivyopo haviharibiwi wala kuchafuliwa kwa njia yeyote ile kama uchimbaji holela wa madini,kulima,kuchoma misitu moto,kukata miti ovyo au kujenga kwenye vyanzo vya maji.
Ikumbukwe kuwa uharibifu wa vyanzo vya maji mahali popote ni kinyume cha taratibu, kanuni na sheria za nchi,hivi sasa imefikia wakati kwa vyombo vinavyosimamia sheria kuamka na kuanza kuchukua hatua za haraka kwa wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira ya vyanzo vya maji ili kuwanusuru viumbehai wote ambao wanaishi kwa kutegemea mazingira bora ili kupata maji na mahitaji mengine muhimu kama chakula.
Viumbehai vyote vinavyoonekana na visivyoonekana haviwezi kuishi bila mazingira endelevu,kuhifadhi na kuyatunza mazingira ni jambo la lazima kwa wadau wote kushirikiana kwa pamoja ili dunia iendelee kubakia mahali salama kwa binadamu, wanyama na viumbe hai wengine.
Tovuti:www.maendeleonivita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment