Na Albano Midelo.
SEKTA ya utalii katika mkoa wa Ruvuma hivi sasa imepamba moto hasa kutokana na ukanda wa Mtwara korido kuwa katika hatua za kufunguliwa.
Mkoa wa Ruvuma umejiweka tayari kuhakikisha kuwa sekta ya utalii katika vivutio mbalimbali inaimarishwa katika wilaya zote za mkoa huo .
Maeneo muhimu ya mambo ya kale kama vile makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa majimaji yaliopo katika manispaa ya Songea yanaweza kutumika kwa ajili ya utalii wa kiutamaduni au mambo ya kale.
Utalii wa mambo ya kale na kiutamaduni ukifanikiwa mkoa wa Ruvuma utakuwa umeonyesha njia ya kuanzisha utalii wa aina hiyo hapa nchini.
Mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya taifa Majimaji Philipo Maligisu akizungumzia utalii wa kiutamaduni anasema utalii wa aina hiyo ni tofauti kabisa na aina ya utalii ambao umezoeleka na wengi ukiwemo wa kuona wanyama katika hifadhi.
Anasema utalii wa kiutamaduni katika mkoa wa Ruvuma ,utauweka mkoa huo katika mazingira ya kiulimwengu katika historia ya utamaduni wa kishujaa na kuunganisha utalii baada ya kuonekana katika dunia vivutio hivyo adimu na vya kipekee .
“Utalii wa kiutamaduni unahusiana na kitu chochote kinachohusiana na matumizi ya binadamu kama vile sehemu ya kihistoria,mambo ya kale,tukio au eneo la utafiti wa kiekolojia inaweza kuwa kivutio cha utalii”,anasisitiza Maligisu.
Shughuli zinazosababisha watu kufanya utalii kulingana na Maligisu ni kwa ajili ya kujiburudisha,kuhiji,wanandoa kwa ajili ya fungate,kujifunza historian a kufanya utalii wa michezo.
Hata hivyo anasema upo utalii wa mapendekezo ya daktari ambapo mtu hushauriwa kusafiri na kwenda kuishi katika mazingira Fulani katika kipindi Fulani cha mwaka na kwamba kuna utalii wa kidiplomasia na matukio ya kibiashara.
Utafiti uliofanyika kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2005 hadi 2006 umebaini kuwa mkoa wa Ruvuma una aina zote za utalii ambapo katika utafiti huo kuna maeneo ambayo yalichukuliwa kama mfano ikiwemo kwenye milima ya Matogoro,Ruhila game reserve,Boma la mjerumani la mwaka 1902 na Chandamali hill.
Gereza la mkoa wa Ruvuma la mwaka 1902,mahakama ya kwanza, sehemu ambayo walinyongewa mashujaa wa vita vya majimaji,makaburi waliozikwa mashujaa,kaburi la jumla na makumbusho yenyewe ni miongoni mwa vivutio adimu vya kihistoria na mambo ya kale.
Kivutio cha Utalii cha milima Matogoro kulingana na utafiti huo kipo kilometa 25 hivi kutoka mjini Songea na kivutio hicho kilianza tangu wakati wa utawala wa wajerumani na kilitengwa tangu wakati huo kwa ajili ya hifadhi ya msitu ambao unaendelezwe hadi sasa.
Maligisu anabainisha kuwa milima ya Matogoro kama kivutio cha utalii kilianzishwa rasmi kisheria wakati wa utawala wa uingereza ambapo hivi sasa milima ya Matogoro inamilikiwa na wizara ya utalii na maliasili kupitia idara ya misitu na nyuki.
Wajerumani tangu wakati huo walitunza misitu ya milima Matogoro baada ya kufanya utafiti kwa lengo la kutunza chanzo cha mto Ruvuma ambacho kimeanzia katika milima hiyo ambacho kinaendelea na kumwaga maji yake bahari ya Hindi.
Maligisu anasema katika utafiti huo wa wajerumani,ambao maandishi yake yamehifadhiwa hadi sasa,walisema njia sahihi ya kuitunza milima ya Matogoro ni kuweka kisheria ili asitokee yeyote ambaye angeweza kuvamia milima hiyo na kuharibu chanzo cha mto Ruvuma ambao ni miongoni mwa mito mikubwa hapa nchini pia ni chanzo cha maji yanayotumika hivi sasa katika manispaa ya Songea.
Utalii wa mambo ya kale pia umeonekana unafaa katika eneo la Chandamali hill manispaa ya Songea,kilima hicho kipo chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania umbali wa kilometa nne kutoka mjini Songea.
Maligisu ambaye alifanya utafiti katika kilima hicho anasema ndani ya msitu huo wa Chandamali kuna pango la chifu Songea Mbano hivyo kuwa kivutio kikubwa katika utalii wa historia ya vita vya majimaji.
Utafiti huo unaonesha kuwa pango hilo limeanza kutumika tangu kipindi hicho ambapo chifu Songea Mbano alikuwa analitumia kuendeshea mijadala na watu wake ambao walikuwa wanamsaidia katika vita vya majimaji.
Msitu wa Chandamali una utalii wa kihistoria na unalindwa kulingana na kanuni zote za uhifadhi kwa njia ya mila,jeshi na uongozi wa Halmashauri ya manispaa ya Songea kutokana na msitu huo kuwepo katika sera ya maliasili ya ulinzi.
Hata hivyo Maligisu anasema historia ya majimaji inaanzia katika mkoa wa Lindi lakini katika mkoa wa Ruvuma hususani mji wa Songea una historia ya kipekee katika vita hivyo na hasa katika msitu wa Chandamali wenye historia tangu enzi za wajerumani.
Kuhusu Boma la wajerumani lililojengwa mjini Songea mwaka 1902 mhifadhi huyo kutoka makumbusho ya taifa anasema boma hilo lilitumiwa na utawala wa serikali ya uingereza na kuendelea kutumika hadi nchi ilipopata uhuru wake mwaka 1961.
Anasema hadi sasa boma hilo la utalii wa mambo ya kale linatumika na ofisi ya usalama wa taifa mkoa wa Ruvuma tangu lilipojengwa mwaka 1902 na kuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Kuhusu gereza la mkoa wa Ruvuma kama kivutio cha mambo ya kale mhifadhi hiyo anasema gereza hilo lilijengwa wakati wa utawala wa wajerumani kwa kutumia miti na kwamba gereza hilo la mkoa ndimo walikowekwa wahanga walionyongwa katika vita vya Majimaji na walikaa katika gereza hilo kwa miezi miwili wakati wanasubiria hukumu yao ya kunyongwa.
“Wahanga hao walinyongwa Novemba 10 mwaka 1906 na hukumu hiyo ilisubiriwa kutoka Ujerumani bahati mbaya hukumu iliangukia siku ya kuzaliwa Wiliam ambaye alikuwa ni Chancela wa Ujerumani wakati huo ndiyo maana walikaa kipindi kirefu gerezani wakisubiri sherehe hizo zipite na hukumu kutolewa kwamba wote wanyongwe”,anasema Maligisu.
Gereza hilo kwa mara ya mwisho lilifanyiwa ukarabati mwaka 1948 kabla ya hapo lilifanyiwa ukarabati mwaka 1908 na kwamba gereza hilo lilijengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi.
Kivutio kingine cha utalii wa mambo ya kale kutoka katika manispaa ya Songea ni mahakama ya kwanza ya mkoa wa Ruvuma ambayo ilitumiwa na serikali ya wajerumani na katika kipindi hicho hukumu ya wahanga wa vita vya majimaji ilifanyika katika mahakama hiyo baada ya hukumu kutolewa toka Ujerumani.
Watu wengine waliofuata baada ya wahanga hao kunyongwa walihukumiwa katika mahakama hiyo ya kwanza kabisa katika mkoa wa Ruvuma na kwamba serikali ya Uingereza nayo iliendelea kuadhibu kwa kutumia mahakama hiyo.
Mahakama hiyo imekuwa katika historia ya mambo ya kale na hivi sasa haitumiki tena hivyo kuwa kivutio cha utalii wa mambo ya kale.Mahakama hiyo katika kutii sera ya utamaduni haijaharibiwa badala yake pembeni yake imejengwa mahakama nyingine ya kisasa ya mkoa wa Ruvuma .
Utafiti unaonesha kuwa Katika Tanzania maeneo mengi yenye majengo ya kihistoria yameharibiwa kwa kujenga majengo mapya na kubomoa ya zamani,lakini katika mkoa wa Ruvuma majengo hayo yanaendelea kutunzwa na kuingizwa katika utalii wa mambo ya kale.
Makumbusho ya majimaji ndiyo makumbusho pekee nchini ambayo inamiliki vifaa halisi na zana halisi za jadi ambazo zilitumiwa na wazee wa jadi katika mambo mbalimbali.
“Mimi nimefanya kazi katika makumbusho ya taifa Dar es salaam hakuna zana halisi za jadi kama makumbusho ya majimaji,hivyo nadiriki kusema majimaji ni makumbusho pekee nchini yenye zana hizi ukiondoa makumbusho ya Ujerumani ambayo ina vifaa halisi ambavyo vilitumiwa wakati wa vita vya majimaji”,anasisitiza mhifadhi huyo.
Hata hivyo utafiti umebaini kuwa makumbusho nyingi zimekosa vifaa kwa kuwa vilichukuliwa na kuondoka navyo watawala na kwamba katika makumbusho hayo kilichofanyika ni kutafuta vifaa ambavyo vinafanana na sio halisi kama makumbusho ya majimaji.
Kulingana na Maligisu katika makumbusho ya taifa kuna document pekee na sio nyala halisi na kwamba katika makumbusho ya mashujaa wa majimaji vifaa halisi ambavyo vilitumika mwaka 1905 vipo hadi leo.
“Hili ni jambo la kihistoria na ni utalii wa kiutamaduni ambao watalii wengi wa ndani na nje ya nchi watapenda kuja katika makumbusho haya na kujifunza,kuona vifaa na zana halisi zilizotumika ambavyo vimehifadhimiwa katika majengo ya makumbusho hayo”,anasisitiza.
Makumbusho ya mashujaa wa vita vya majimaji yalijengwa mwaka 1980 lengo lilikuwa ni kutunza hadhi ya sehemu ya makumbusho ya majimaji, shinikizo la ujenzi wa majengo hayo lilitolewa na kauli ya Baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere kwenye mkutano wea TANU mwaka 1958.
Nyerere aliagiza ijengwe minara katika mikoa yote nchini kwa ajili ya heshima ya kuwaenzi mashujaa wa ukoloni ambao ndiyo chimbuko la kupigania uhuru, katika mikoa yote ni Songea pekee ndiyo iliyobahatika kuwa na makumbusho .
Utafiti unaonesha kuwa katika maeneo mengine ya nchi walishindwa hata kujenga minara ya mashujaa ambapo Baba wa taifa mwaka 1965 alisisitiza na kukumbushia kile alichoahidi kujenga minara mwaka 1958 sasa kila mkoa ujenge minara hiyo ya mashujaa.
“Mkoa wa Lindi umejenga mnara mwaka 2008 tena kwa shinikizo la chuo kikuu cha Dar es salaam ambapo mnara huo umejengwa katika eneo la Nandete ndiyo maana nasema Songea ndiyo pekee ambapo katika makumbusho ya Songea zimejengwa sanamu mbalimbali za wapiganaji ambao alikuwa nao chifu Songea Mbano kwenye Baraza lake kupambana na wakoloni’,anasema mhifadhi wa makumbusho ya taifa.
Sanamu hizo zipo 12 na wote hao walikuwa ni washauri wake wa karibu wa chifu Songea ,pia katika makumbusho hayo kuna sanamu ya askari waliotoka kupigana vita vya kumg’oa Idd Amini mwaka 1978.
Sanamu hiyo imekusudia kuwakumbuka askari walitoka katika mkoa wa Ruvuma ambao walikwenda kupigana vita vya Uganda ambapo kwa bahati mbaya wakati askari hao wanarudi nyumbani walipata ajari katika milima ya lukumbule na wote walikufa hivyo serikali iliamua kujenga sanamu hiyo katika eneo hilo lililoitwa mashujaa kwa lengo la kutambua mchango wao kwa taifa.
Hayati Baba wa taifa pia ndiyo aliyefungua makumbusho ya mashujaa na kuamuru mnara wa mashujaa ujengwe katika eneo hilo ,hivyo kutokana na hali hiyo mkoa wa Ruvuma umekidhi vigezo vyote vya kuingia katika makumbusho ya taifa kulingana na sera ya taifa ya utamaduni ya mwaka 1997.
Sera hiyo inasema kuwa vitu vyote ambavyo vinahusiana na historia ya mwanadamu baada ya miaka 100 haina mjadala bali vinaingia moja kwa moja katika urithi wa taifa.Sera ya maliasili na utalii na sera ya utamaduni imetamka wazi kwamba sheria za mambo ya kale bado hazifahamiki sawasawa na wadau wengi hivyo hivyo hawajui waanzie wapi na waishie wapi katika kuimarisha utalii wa mambo ya kale.
Ipo sheria ya mambo ya kale iliyo chini ya wizara ya malisili na utalii ya mwaka 1964 na 1979 ambayo inatamka bayana kuwa waziri mwenye dhamana ya maliasili na utalii anatangaza katika gazeti la serikali kuwa eneo lenye vivutio vya mambo ya kale ni sehemu ya urithi wa taifa,sehemu yeyote ya kihistoria kama makumbusho ya majimaji ili jamii iweze kutambua badala ya kuendelea kufanya kimila pekee.
Wananchi wa mkoa wa Ruvuma ingawa hawajachelewa katika kuanzisha utalii wa mambo ya kale,wangejua tangu mapema sera za sheria ya mambo ya kale wangekuwa mbali katika utalii wa aina hiyo. Ili kuokoa urithi huo uliopo Ruvuma , inafaaa kuifanya dunia na ulimwengu ujue Songea kuna makumbusho ya kipekee ya mambo ya kale.
Simu 0766463129
baruapepe amidelo@yahoo.com,simu
Tovuti;www.maendeleo ni vita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment