Wednesday, February 2, 2011

Kilimo cha ngoro kinavyoweza kuwa kivutio cha utalii

Picha inaonyesha kilimo cha Ngoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ambacho ni kivutio cha utalii wa kiutamaduni

Na Albano Midelo.
NGORO ni aina ya kilimo ambacho kinaaminika kilianza kutumika na wakulima wa kabila la wamatengo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma zaidi ya miaka 300 iliyopita.

Kilimo cha ngoro kilianzishwa na wazee maarufu wa kabila la wamatengo waliotokea nchini Malawi katika karne ya 17 ambapo tayari vizazi zaidi ya 10 vimepita hivi sasa tangu kilimo cha ngoro kilipoanzishwa wilayani Mbinga.
 Moja ya madhumuni ya kuanzisha kilimo hiki ni kuudhibiti udongo wa juu wa ardhi  ambao kwa kawaida huondolewa na maji au upepo  kutokana na mmomonyoko wa ardhi ya juu ambayo ina rutuba nyingi ya kuifanya mimea iweze kustawi vizuri na hatimaye kutoa mavuno mengi na bora.

Tunajua kuwa udongo ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi vizuri, Kutoweka kwa udongo wa juu toka shambani au bustani kwa njia ya mmomonyoko ni hasara kubwa , kwa vile kunasababisha upungufu wa mavuno. Hivi basi lazima kuzingatia hifadhi ya ardhi ili mkulima aweze kupata mazao bora.

Njia za kuhifadhi ardhi zinaweza kutumiwa kwa kutegemea hali ya hewa, mazingira ya eneo kama ni maeneo ya mwinuko au tambarare. Hata hivyo zinaweza kutumika njia mbili au tatu katika shamba moja. Ziko njia kuu mbili za kuhifadhi ardhi ambazo ni njia za asili au za kienyeji na njia ya kisasa ambazo zimefanyiwa utafiti yakinifu na wataalamu.

 Wataalamu wakongwe kama akina Bike  mwaka 1938, Stenhouse  mwaka 1994,  Temu na Bisanda  mwaka 1966 wanaeleza kuwa Wamatengo walilazimika kutumia kilimo cha ngoro  ili kuhifadhi udongo mzuri ulio katika miteremko hiyo. Ngoro hulimwa kwa kuchimba mashimo madogo madogo katika miteremko hiyo.

Katika mashimo hayo hupandwa mazao kama maharage,mahindi na ngano kwenye kingo za mashimo hayo. Mkulima hufyeka shamba  lake  na kuzipanga nyasi zilizokatwa katika mistari kwenda juu mpaka chini na toka upande wa kushoto kwenda kulia.

 Mkulima akipindua udongo wa chini kuwa juu na chini ya udongo wa juu kukaa, nyasi na udongo wenye rutuba zilizofunikwa hugeuka kuwa mboji na polepole udongo wenye rutuba huongezeka. Maji ya mvua yakisimama katika mashimo hayo  madogo hulinda unyevu wa ardhi na kukinga mmomonyoko wa ardhi.

Inaaminika kuwa kilimo cha ngoro ambacho tunaweza kukiita draft agriculture kinahusishwa na shughuli za kuwepo kwa mapango ya kuishi.Hapo zamani wananchi wa wilaya ya Mbinga walikuwa na tabia ya kufanya kilimo cha kuhamahama.

Wakulima wakilima sehemu moja na wanapogundua sehemu hiyo rutuba imemalizika walikuwa wanahamia sehemu nyingine yenye rutuba na kuendesha kilimo bila kujali athari za kimazingira ambazo zilikuwa zinajitokeza kutokana na aina hiyo ya kilimo.

Kutokana na kuwepo kwa mapango, wazee hao wa kabila la wamatengo waliamua kaunzisha kilimo cha kulima ,kufukia majani  ili kupata mbolea ya asili kulima na kufukia hivyo kuendesha kilimo walichokiita ngoro katika sehemu moja bila kuhama huku wakirutubisha ardhi na kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na ardhi ya Mbinga kuwa milimani.

Mbunge mstaafu wa Mbinga mashariki Ngwatura Ndunguru anasema wamatengo tangu wameanza kutumia kilimo cha ngoro miaka 300 iliyopita hadi sasa wamekuwa wanazalisha vyakula kwa wingi pamoja na kuhifadhi mazingira kwa njia ya asili kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokea kwenye mitelemko ya milima ya umatengo wilayani Mbinga.

Anabainisha kuwa kilimo cha ngoro ni sawa na mchanganyiko wa kilimo cha umwagiliaji  mvua zinaponyesha maji huingia taratibu kuingia kwenye mmea na kuzuia udongo usiharibiwe na kwamba yale majani yaliyowekwa chini yanaoza ambapo katika msimu mwingine wa kilimo majani yaliota kwenye shimo  yatafyekwa mazao yaliosalia yatavunwa na kutandazwa kwenye shimo na kufukuliwa majani ya mwaka jana ambayo tayari yanakuwa mboji.

Elia Hyera(60),John Mbunda(80),Zuberi Kapinga(90) wakazi wa kijiji cha Kilanga Juu wilayani Mbinga wanasema wamatengo walianzisha mfumo  maalumu ya kilimo cha ngoro uliyowasaidia uliyojulikana kwa jina la “Ingoro,” mfumo ambao uliwawezesha kuendelea kulima kwenye maporomoko ya milima bila ya kusababisha mmomonyoko wa udongo au kuathiri vibaya rutuba kwenye mashamba yao.

 Utafiti wa kina umeonyesha wazi kwamba  teknolojia ya ngoro ni bora zaidi katika kilimo,ambapo wakulima kutoka  maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakifika katika wilaya ya Mbinga kujionea wenyewe na kujifunza teknolojia hiyo ya kilimo cha ngoro.


Moja ya faida ya kilimo cha ngoro ni kwamba hata kama mvua hazitanyesha, bado shamba litaendelea kuwa na unyevunyevu kutokana na maji yaliyomo ndani ya mashimo hayo,isitoshe wakati wa mavuno, mabaki ya nafaka huwa yakitupwa kwenye mashimo hayo,husababisha shamba kustawi vizuri zaidi kutokana na mbolea iliyowekwa.

Mbunge  mstaafu wa Mbinga magharibi Ngwatura Ndunguru ambaye ni mtumishi mstaafu wa wizara ya maliasili na utalii anasema tayari wameanza kukitangaza kilimo hicho na kukiingiza kuwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana katika wilaya ya Mbinga pekee na hakuna sehemu nyingine yeyote duniani inayoendesha kilimo cha aina hiyo.

Baadhi ya wageni  ambao wamekuwa wakitembea kwenye magari kupitia barabara ya Mbinga hadi bandari ya Mbambabay pamoja na maeneo mengine ya milima ya umatengo wamekuwa wakisimama mara kwa mara kwenye milima hiyo na kuchukua picha za kawaida na video kwenye kilimo cha ngoro ambacho kimeonekana kuwavutia  watalii wengi wa  ndani na nje ya nchi hasa mimea  inayochomoza na kuonekana mfano wa mapambo fulani yaliopambwa milimani.

Simu:0766463129






No comments:

Post a Comment