Wednesday, February 2, 2011

Kihagara kitovu cha utalii mwambao mwa ziwa Nyasa

Picha inaonyesha samaki aina ya ngogo ambaye hajai hata kwenye kiganja cha mkono lakini ana maajabu mengi ikiwa ni pamoja na uwezo wa kumuua mamba pamoja na kukausha mti mkubwa kwa siku saba tu,samaki huyu ambaye ni kivutio cha utalii anapatikana kwa wingi eneo la Kihagara ziwa Nyasa
samaki mwenye uwezo wa kuuwa mamba  na kukausha miti mikubwa
Na Albano Midelo.
KATA ya Kihagara inapatikana kilometa karibu 250 kutoka makao makuu ya mkoa wa Ruvuma Songea,ipo mwambao mwa ziwa Nyasa,kata hiyo ina vijiji vitano ambavyo ni Kihagara,Mango,Ngehe,Tumbi na Njambe.

Kata ya Kihagara ina wakazi zaidi ya 6000 huku shughuli kuu za kiuchumi ikiwa ni uvuvi wa samaki katika ziwa Nyasa pamoja na kilimo, zao kuu ni Muhogo,Unga wa muhogo unapendwa na wakazi walio wengi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ukilinganisha na unga wa mahindi hali ambayo inasababisha wakazi hao kulima zao la mahindi katika kiwango kidogo .

Katika makala yangu lengo sio kuzungumzia shughuli za kiuchumi ukiwemo uvuvi na kilimo,bali katika makala haya lengo ni kuonyesha utajiri wa maliasili ambazo zinapatikana katika kata ya Kihagara  na endapo zitatambuliwa na kutangazwa zinaweza kuwa vivutio adimu vya kitalii hivyo kuboresha sekta hiyo kwa haraka na kuchangia maendeleo ya wakazi wa mwambao walio wengi wanakabiliwa na umaskini mkubwa.

Utakubaliana na mimi kuwa Kihagara ni kitovu cha utalii mwambao mwa ziwa Nyasa kwanza ni kutokana na eneo hilo kuongoza kwa kuwa na samaki wa aina mbalimbali kupatikana kwa wingi wakiwemo samaki wa mapambo ambao licha ya kuwa kivutio cha utalii pia wanaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi endapo wakazi hao watatafutiwa soko la uhakika badala ya hali inayoendelea hivi sasa watu wachache wajanja wanawavua samaki hao na kwenda kuwauza kwa bei kubwa huku kata hiyo ikendelea kuwa masikini.

Martin Ndomba mkazi wa kijiji cha Kihagara anasema katika kijiji hicho kuna vivutio lukuki na vya kipekee vya utalii kikiwemo cha aina ya samaki wa pekee mwenye umbo dogo anayeitwa ngogo lakini ni mfalme  katika ziwa Nyasa kutokana na kuwa na uwezo wa kuuwa samaki wakubwa kama bogobogo ambaye ana mwili mkubwa sawa na binadamu mtu mzima.

“Sisi wavuvi tunamwita samaki huyu mfalme katika ziwa Nyasa kwa kuwa hakuna samaki anayeweza kupambana naye wote wanamkimbia,samaki huyu ana maajabu kwa kuwa samaki mkubwa akifika jirani na samaki huyo kwa lengo la kummeza,samaki ngogo anaficha miba zake ambazo zipo pande zote baada ya kumezwa akiwa tumboni samaki huyo hukunjua miba zake ambazo zina sumu kali  na kumsababishia samaki mkubwa kufa hivyo yeye baada ya samaki huyo kuoza anatoka ingawa anakuwa amekonda na kuendelea na maisha kama kawaida na kuendelea kupambana na samaki wengine”,anasema Martin Ndomba mvuvi mzoefu ziwa Nyasa.

Thomas Komba mzee mkongwe  na mvuvi ziwa Nyasa anasema samaki huyo ambaye hata kwenye kiganja cha mkono hajai,ana uwezo wa kumuua mamba ambaye ambaye ni adui mkubwa wa binadamu kwa kuwa mamba anakula binadamu hali ambayo inaleta hofu kubwa kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa baadhi yao kuogopa kuoga ziwani kutokana na historia ya mamba wa ziwa hilo kupenda kula watu.

“Samaki ngogo  akimezwa na mamba akiwa tumboni anachomoa miba yake ambayo ipo mitatu tu na kuanza kumchoma mamba ambaye kutokana na sumu ya miba ya samaki huyo mamba huanza kudhoofika na hatimaye kufa,kwa kweli samaki huyu ni wa maajabu makubwa ,ingefaa wizara ya utalii na maliasili itangaze maajabu yake ili watalii wengi waweze kufika ziwa Nyasa kumuona na kuingiza fedha za kigeni”,anasisitiza.

Maajabu mengine ya samaki ngogo kwa mujibu wa wavuvi hao wa ziwa Nyasa ni kwamba endapo samaki huyo atashikwa vibaya wakati anavuliwa na kumchoma mvuvi kwenye mguu au mkono wake anaweza kusababisha mguu au mkono uliochomwa kwa mwiba wake wenye sumu kali kukatwa  hali ambayo inawafanya wavuvi kuwa waangalifu wanapokuwa ziwani endapo wanakutana na samaki huyo.

Uchunguzi mwingine ambao umethibitishwa na baadhi ya wavuvi na wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa umebaini kuwa samaki huyo anatumiwa kwa ajili ya kukausha miti mikubwa mibichi kwa ajili ya kupata kuni kama anavyoeleza Martini Ndomba “Tangu enzi za zamani wazee wetu walikuwa wanamchukua samaki ngogo akiwa hai na kwenda kumchomeka mwiba wake kwenye mti mkubwa mbichi ,wakati samaki huyo anachomekwa mwimba wake uliochongoka,mnene na mgumu kwenye mti mbichi anatoa sauti ambao ni ishara kuwa sumu yake imeingia kwenye mti ambao baada ya siku saba hadi 14 unakauka kabisa”

Wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa katika mila zao tangu zamani wanakataza mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kula samaki aina ngogo kwa madai kuwa analeta ugonjwa wa degedege  yaani malaria kali,hata hivyo samaki huyo mwenye radha ya kipekee wakazi wa mwambao wanamtumia zaidi kula wakati wanakunywa pombe za kienyeji badala ya kutumika kama kitoweo kwa ajili ua ugali au wali,pia samaki huyo ni moja ya aina za samaki wa mapambo.

Maajabu mengine ambayo yapo katika kata ya kihagara ambayo ni kivutio cha kipekee ni samaki aina ya mkunga anayepatikana katika ziwa Nyasa pekee hususani kwenye kata ya Kihagara,samaki huyu anafanana na nyoka kwa kila kitu,kinachowatofautisha ni kwamba samaki huyu hana meno na sumu.

John Vumu mvuvi  katika kata ya Kihagara anasema mkunga au samaki nyoka unapomwona kwa mara ya kwanza huwezi kumtofautisha na nyoka aina ya chatu,hata hivyo anasema ni samaki mtamu mwenye mafuta mengi na anapatikana kwa nadra sana ukilinganisha na aina nyingine za samaki na kwamba siku za nyuma samaki huyu alikuwa anapatikana kirahisi ukilinganisha na sasa sehemu nyingi za mazalia yake zimeharibiwa hali iliyosababisha kuanza kutoweka.

“Maajabu ya samaki huyu ambaye anakuwa na urefu wa karibu mita mbili endapo mmemvua na jirani akakutana na jiwe anaviriga mkia wake kwenye jiwe hali ambayo inasababisha kuwa vigumu kumvuta hata kama mkiwa wavuvi kumi hamuwezi hadi samaki huyo ajikunjui kwenye jiwe ndipo mnaweza kuendelea kumvuta hivyo inatakiwa muwe na subira ya kumsubiri ajisahau na kuamini kuwa yupo salama hali ambayo inachukua hadi dakika 30 au 45”,anasema Vumu mvuvi mkongwe ziwa Nyasa.

Martin Ndomba anasema samaki mkunga kila kitu anafanana na nyoka isipokuwa mkia wake unafanana na samaki na kwamba mdomoni hana meno isipokuwa ana vitu vinavyofanana na msasa wa kusafishia mbao  ambavyo anaweza kukuchubua au hata kukujeruhi lakini hana meno wala sumu.

Kivutio kingine ambacho kinapatikana Kihagara ni eneo oevu ambalo lina ukubwa wa karibu meta 300 ambalo linajaa maji na kuwa kivutio cha wanyama mbalimbali wakiwemo ndege aina ya nyangenyange pamoja na chura wenye uwezo wa kuimba nyimbo nzuri kwa sauti tamu na tofauti na chura ambao unawafahamu.

Felician Komba mkazi wa kijiji cha Kihagara anasema  eneo hilo ambalo linafanana na ziwa au bwawa ambalo lipo umbali wa kilometa moja na nusu kutoka kijiji cha Kihagara, miaka ya nyuma lilikuwa na maji muda wote hali ambayo ilisababisha idadi kubwa ya samaki wa aina mbalimbali kuzaliana kwa wingi na kulisha karibu kata nzima ya Kihagara ambayo ina vijiji vitano ambavyo ni Kihagara,Mango,Tumbi,Njambe,Ngehe ambapo baada ya kutokea uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji umesababisha  bwawa hilo kuanza kukauka na kujaa maji kwa msimu.

Komba anasema mwezi wa tatu hadi wa tano kila mwaka bwawa hilo ujaa maji ambayo yanatoka kwenye mto Mbuchi ambapo maji yanapopungua watu hufika katika bwawa hilo kukamata maelfu ya samaki na kwamba bwawa hilo linapojaa  maji linakuwa kivutio cha viumbehai wengi wakiwemo,mamba, maelfu ya ndege aina ya nyangenyage,bata maji wanafika kwa wingi na kuzaliana katika eneo hilo pamoja na bata maji wenye umbo dogo ambao wanamilio ya kuvutia na kupendeza.

“Katika hali ya kustaajabisha bwawa hili likijaa maji lina aina Fulani ya chura  warefu,wana ngozi laini weusi kidogo wana uwezo wa kuimba nyimbo nzuri ambazo huwezi kuamini kama wanaoimba chura,nyimbo hizo zinasikika umbali hata wa kilometa tano,chura hao huimba kwa pamoja katika sauti ya kwanza na ya pili,ukiwasogolea wanaendelea kuimba lakini akipita mnyama ambao wanadhani kuwa ni adui wote kwa pamoja wananyamaza”,anasema Komba na kusisitiza kuwa hayo ni maajabu ya  bwawa hilo.

Hata hivyo Komba  anasema chura hao uendelea kuimba nyimbo hizo hadi mwezi wa nne kila mwaka wakati ambao maji yanakuwa yameanza kukauka katika eneo hilo na kutoweka tena hadi kipindi kingine ambacho maji yanaanza kujaa kwenye bwawa hilo na kwamba katika kipindi ambacho chura hao wanazaana hawaendelei kuimba tena nyimbo hizo.

Anamtaja adui mkubwa wa chura hao kuwa ni ndege aina ya nyangenyage wenye shingo ndefu  ambao wanakula chura hao kwa kuwadonoa wanapowaona katika bwawa hilo  anasisitiza umuhimu wa kuhifadhi bwawa hilo ili viumbe hai waweze kupatikana wakati wote na kuwa kivutio kikubwa cha watalii.

Anasema bata maji ambao wanapatikana katika bwawa hilo nyama yake ni laini yenye radha tamu,pia nyama hiyo haishiki kwenye meno kama ilivyo kwa wanyama wengine ambao humlazimisha mlaji kutafuta kijiti cha kutolea nyama ambazo zimekwama kwenye meno na kuleta kero kubwa kwa walaji.


Komba anasema hivi sasa kijiji cha Kihagara kwa kushirikiana na mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Injinia Stella Manyanya wameweka mikakati kuanzia mwaka huu kuhakikisha kuwa bwawa hilo ambalo ni kivutio cha utalii halikauki badala yake linakuwa na maji wakati wote kama ilivyokuwa zamani na kwamba hilo linawezekana kwa kuhifadhi vyanzo vya maji pamoja na kupanda miti na nyasi ili kuhifadhi ene hilo.

Komba anabainisha zaidi kuwa kijiji hicho kimekusudia kujenga vibanda vya asili katika eneo la bwawa hilo ili kuwawezesha watalii kukaa wakati wanaona vivutio vilivyopo katika bwawa hilo hali ambayo itaongeza pato kwa kijiji litakalotokana na kodi watakazolipia watalii
0766463129
Tovuti:www.maendeleonivita.blogspot.com





No comments:

Post a Comment