Wednesday, February 2, 2011

Selous hifadhi ya wanyama inayoongoza kwa viumbe adimu duniani



Na Albano Midelo.
PORI la akiba la Selous ni moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii hapa nchini na endapo lingetangazwa kwa nguvu zote lingeweza kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni na kuongeza pato la taifa.

Changamoto iliyopo hivi sasa ni pori hilo kutofahamika vilivyo licha ya kuwa kubwa,lenye vivutio lukuki na limeanzishwa miaka mingi iliyopita. Pori la akiba la Selous linapatikana katika mikoa minne ikiwemo Ruvuma,Lindi,Pwani na Morogoro.

Selous ni moja kati ya mapori mengi yaliopo hapa nchini likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 50,000 likijumuisha maeneo ya ardhi oevu,misitu ya miombo,tambarare ,nyasi za kuvutia,maziwa na mito inayotiririka na kuwa kivutio.

Pori la akiba la Selous lilianzishwa  mwaka 1896 na wajerumani likiwa pori la kwanza kutengwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori barani Afrika na la pili duniani baada ya pori la Marekani ambalo linaitwa Yellowstone National Park.

Meneja mkuu wa pori la akiba la Selous John Mbwilizi  anasema jina la Selous limetokana na askari ambaye alikuwa ni mvumbuzi wa kiingereza aliyeitwa kapteni Fredrick Selous aliyefariki Januari 4, mwaka 1917 wakati anapigana vita vya pili vya dunia na kuzikwa katika eneo la Behobeho .

Pori la akiba Selous Pori la Selous lina utajiri wa viumbe adimu katika sura ya dunia kama vile nyani aina ya sanje,mbega mwekundu na faru mweusi yupo hatarini kutoweka pamoja na wanyama wengine wakiwemo ndege na wadudu.

Ndege waliopo katika pori la Selous mara kwa mara wamekuwa wakisafiri katika pori hilo ambapo wakifika katika pori la Selous  katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma hupumzika na kuendelea na safari hadi nchini Afrika ya kusini.

Kwa ujumla pori la Selous linapakana na wilaya tisa katika mikoa minne kati ya hizo mkoa wa Ruvuma pori hilo linapita katika wilaya za Namtumbo na Tunduru.

 Katika kuonesha kuwa Pori la akiba la Selous ni kubwa  linapita katika vijiji 83 vilivyopo katika mikoa ya Pwani,Ruvuma,Lindi na Morogoro hivyo wananchi hao wanaoishi karibu na pori hilo wananufaika na utalii shirikishi unaofanywa.

Selous ndiyo pori linalosifika kuwa na uoto wa kuvutia wa miombo pamoja na idadi kubwa ya wayama tembo ambayo inakadiriwa kuwa zaidi ya 70,000 hali inayosababisha wakati mwingine wanyama hao kutoka nje ya pori na kwenda katika makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mali.

Tembo zaidi ya 70,000 waliopo katika pori hilo kitakwimu ni idadi ambayo ni kubwa kuliko idadi ya tembo iliyopo katika hifadhi nyingine yeyote ulimwenguni,ambapo idadi ya mamba katika pori hilo inafikia zaidi ya 80,000,mbwamwitu zaidi ya 3000 na viboko zaidi ya 40,000.

Kutokana na umuhimu wa pori la Selous shirika la umoja wa  mataifa linaloshughulikia utamaduni na sayansi UNESCO  limelihorodhesha pori hilo kuwa ni  moja ya maeneo ya asili ya urithi wa dunia tangu mwaka 1982.

 Pori hilo linakabiliwa na ujangili wa nyara mbalimbali za serikali,uwindaji haramu kwa kutumia silaha haramu za aina mbalimbali na za sumu,uvuvi haramu na uvunaji haramu wa miti ya mbao ni baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kutokea licha ya kufanyika doria mara kwa mara.

Mafanikio ambayo tayari yamepatikana katika uwindaji wa kitalii kupitia pori hilo ni pamoja na  Tanzania kufikiwa na watalii wawindaji 662 katika pori hilo mwaka 2005,mwaka 2006 watalii 437 na mwaka 2007 watalii 549.

Kulingana meneja  wa pori hilo idadi ya watalii wa picha 55,197  waliotembelea katika pori hilo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka jana na kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.Pori la akiba la Selous lina viwanja vya ndege 22 vinavyotumika na kutoa huduma kwa watalii wa picha,wawindaji wa kitalii na kazi za utawala.

Pamoja na mafanikio hayo pori la akiba la Selous linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo baadhi ya barabara zake kutopitika kutokana na kutofanyiwa matengenezo wakati muafaka kunakosababishwa na ufinyu wa bajeti ya wizara ya maliasili na utalii.

Pori hil linakabiliwa na ulimaji wa mashamba,uchungaji wa mifugo ndani ya hifadhi,wananchi kuanzisha makazi karibu na mipaka ya hifadhi na ukataji wa miti kwa ajili ya majengo,kuni na mkaa.

Mikakati iliyopo katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinalikabili pori hilo ni pamoja na kuimarisha doria katika maeneo yenye ujangili mkubwa  ndani na nje ya pori kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kama polisi ili kukabiliana na ujangili na kutoa elimu ya utalii shirikishi kwa wananchi.

Tovuti:www.maendeleonivita.blospot.com

                   








No comments:

Post a Comment