Na Albano Midelo
TATIZO la mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kanda ya kusini ikijumuisha mikoa ya Ruvuma ,Lindi na Mtwara linaonekana kuwa ni tatizo sugu licha ya hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa na wadau kukabiliana na tatizo hilo.
Uchunguzi ambao umefanywa katika wilaya za Tunduru mkoani Ruvuma,Masasi mkoani Mtwara na Lindi vijijini mkoani Lindi umebaini kuwa asilimia 49 ya watoto wanapata mimba za utotoni.
Takwimu zinaonesha mwaka jana katika mkoa wa Ruvuma pekee jumla ya wanafunzi 400 wa shule za msingi na sekondari walipewa ujauzito na kukatishwa masomo yao huku wilaya ya Tunduru ikiongoza kwa idadi kubwa zaidi ukilinganisha na wilaya nyingine.
Katika uchunguzi huo imebainika sababu mbalimbali zinazosababisha mimba za utotoni zikiwemo mila na desturi za maeneo hayo kurahisisha tatizo hilo la mimba za utotoni kutokea kutokana na mila za ngoma za unyago na jando kwa watoto chini ya miaka saba.
Baadhi ya maeneo wazazi na walezi hawaoni kuwa mimba za utotoni ni tatizo hali iliyosababisha baadhi ya wazazi kuwaficha wanaume waliowapa mimba watoto wao pale sheria inapotaka kuchukua mkondo wake hivyo kukwamisha azma ya serikali ya kupambana na wanaowatia mimba watoto wa shule.
mila za jando na unyago kwa watoto chini ya miaka saba ni mbaya na zinasaidia mimba za utotoni kuongezeka katika maeneo hayo matokeo yake vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi kuongezeka hivyo tatizo la ugonjwa wa Fistula kuendelea hapa nchini.
Hata hivyo sheria ya ndoa inasema mzazi anaweza kutoa ruhusa kwa mtoto wake mwenye umri wa miaka 14 kuolewa hivyo hii ni changamoto na kwamba katika maeneo hayo kiwango cha umasikini ni kikubwa hivyo mzazi akiona mtoto wake amepata mume mwenye uwezo fulani anamruhusu aweze kumuoa.
Uchunguzi ambao umefanywa katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma umebaini athari nyingi za kijamii na kiuchumi za mimba za utotoni hasa kwa wanafunzi wenyewe ambao walikatishwa masomo kwa kupewa mimba na sasa wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa huku wakiendelea kuwatunza watoto waliowazaa bila ya msaada wowote.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Madaha anasema mimba za utotoni katika wilaya hiyo zinachangia kuongeza umaskini wa kipato kuanzia ngazi ya familia kwa kuwa wanafunzi ambao wamejifungua walio wengi wanawalea watoto wao wenyewe kutokana na wanaume waliokuwa wamewapatia ujauzito kukimbia.
Wanafunzi 855 kati ya 3122 waliofaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wilayani Tunduru hawajiunga katika sekondari walizopangiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mimba,kuolewa na mwamko duni wa wazazi na walezi wao.
Madaha anabainisha kuwa kati ya wanafunzi hao 478 ni wavulana na wasichana 375 na kwamba serikali hivi sasa inawasaka nyumba hadi nyumba na kwamba hadi kufikia Septemba mwaka huu watoto wa kike wengi waliofaulu walikuwa wameolewa ambapo takwimu sahihi bado zinaendelea kutafutwa kupitia maofisa tarafa.
“Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai mwaka 2010 wanafunzi 42 wametiwa mimba kabla hawajaripoti katika sekondari walizopangiwa kati ya mimba hizo mimba 16 kesi zipo mahakamani na kesi nyingine zipo polisi,pia mimba 21 zimetokea kabla wanafunzi hawakaripoti shuleni”,anasema.
Madaha anayataja maeneo ambayo yameathirika na vitendo vya mimba za utotoni wilayani humo kuwa ni Mbesa,Nandembo,Malumba,Lukumbule na Muhuwesi na kwamba serikali ya wilaya hiyo imejipanga vizuri kukabiliana na tatizo hilo la mimba ambalo ni tatizo sugu wilayani humuo.
“Unakuta binti aliyetiwa mimba ametoka katika familia masikini na hata mwanaume aliyempatia mimba pia anatoka katika familia duni,hana kipato chochote zaidi ya kulima vibarua hali ambayo inazidisha umaskini zaidi kwa wananchi”,anasema.
Hata hivyo Madaha anasema wengi wanaopewa mimba pamoja na wanaume waliowatia ujauzito hawana mtaji hivyo wanaendelea kuzunguka kwenye wimbi la umaskini mkubwa na kwamba katika mazingira ya namna hiyo mtu hawezi kujikomboa kiuchumi hivyo mume,mke na mtoto waliomzaa wanaendelea kuwa duni.
Abdalah Ally mwanaharakati katika kijiji cha Mataka wilayani Tunduru anasema mabinti wengi waliochishwa masomo kwa kupata mimba wanaishi maisha duni wanafanya vibarua vinavyowaingizia kipato cha kula kwa siku huku wakiwa hawana uhakika wa kesho endapo watakosa kibarua cha kuwaingizia japo shilingi 500 tu.
Anasisitiza kuwa mimba za utotoni wilayani Tunduru zimechangia kuongeza umaskini wa kipato kwa kuwa hivi sasa mabinti wengi waliojifungua wamewaachia mama zao wanawalelea watoto wao na wao wamekimbilia maeneo ya mijini ikiwemo Tunduru,Masasi,Mtwara na Songea wakitafuta kazi za ndani ,kuuza bar na wengine wakijiuza ili kupata riziki.
Ameitaja sababu kuu ambayo inachangia tatizo la mimba za utotoni katika wilaya hiyo kuwa ni ngoma za unyago na jando ambapo serikali ya wilaya hiyo imeagiza ngoma hizo sasa kuchezwa mara moja tu kwa mwaka wakati wa likizo ya mwezi wa sita na kwamba yeyote ambaye atakwenda kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia wanafunzi waliopata mimba na kuacha masomo katika wilaya hiyo anasema suala hilo ni la kisera zaidi ambapo ametoa rai kwa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kutoa sera kwa maeneo yenye matatizo makubwa ya mimba za utotoni kama wilaya ya Tunduru kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi waliacha masomo kutokana na mimba.
Hata hivyo anasema watendaji wa vijiji,kata na maafisa tarafa wamepewa sheria ya elimu namba 25 ya mwaka 1978 na waraka namba sita wa elimu ambao unasisitiza kuhusu mahudhurio ya lazima kwa wanafunzi na kuagiza kila mtoto lazima awepo shuleni na mzazi atakayeshindwa anachukuliwa hatua za kisheria.
Anasema ufaulu wa watoto wa kike katika shule za msingi wilayani Tunduru hasa katika mitihani ya mocko unakuwa ni wa juu sana ukilinganisha na wavulana na kwamba kwenye mtihani wa mwisho ufaulu wa wanafunzi wa kike unakuwa ni wa chini sana na kwamba uchunguzi umebaini kuwa tatizo hilo linaanzia ngazi ya familia ambapo wazazi wanawaambia watoto wao wa kike wasifanye vizuri katika mitihani hiyo ili waolewe na mzazi asipate shida ya kumlipia ada.
Anabainisha kuwa asilimia 90 ya wakazi wa wilaya ya Tunduru ni wa dini ya kiislamu na wanaongozwa na mashehe,maimamu na masultani ambao ni viongozi wasiokuwa rasmi lakini wanaaminika na jamii hiyo na kwamba viongozi hao wakikubaliana na serikali wanaweza kusaidia katika suala la elimu hasa kwa watoto wa kike ili wasiendelee kupata mimba za utotoni.
Baruapepe amidelo@yahoo.com,simu 0766463129.
No comments:
Post a Comment