Tuesday, March 8, 2011

Siku ya utepe mweupe kitaifa mwaka huu mkoani Ruvuma mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri mkuu

Mke wa Rais mama Salma Kikwete akikabidhi vifaa vya hospitali kwa ajili ya akinamama wajawazito mkoani Ruvuma kwa lengo la kusogeza huduma ya uzazi jirani .
Na Albano Midelo.

SIKU ya utepe mweupe ni siku maalum ya kuwakumbuka akinamama wote waliopoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi na kutafakari ni jinsi gani Tanzania  itaepusha vifo hivyo.

Siku ya utepe mweupe kwa mara ya kwanza ilizinduliwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi Machi 25,2006,tangu wakati huo hadi sasa siku hii huadhimishwa kitaifa kila ifikapo mwezi Machi ili kutia hamasa zaidi kuhusu kutokomeza tatizo hili sugu linalokiuka haki za msingi za binadamu.

Maadhimisho haya ya siku ya Utepe Mweupe kitaifa kwa mara ya kwanza yanafanyika mwaka huu mkoani Ruvuma hapo Machi 15,2011 kwa ushirikiano wa wizara ya afya na ustawi wa jamii,  serikali ya mkoa wa Ruvuma na muungano wa utepe mweupe wa uzazi salama Tanzania  ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri mkuu Mizengo Pinda.

Muungano wa Utepe mweupe wa uzazi salama Tanzania  yaani white Ribbon Alliance for safe motherhood in Tanzania (WRATZ) ni jumuiko la asasi za serikali na zisizo za kiserikali,mashirika,vyuo,vyama na watu binafsi wakiwemo wabunge walioungana kutetea usalama wa mama na mtoto wakati wa ujauzito,wakati wa kujifungua na siku 42 baada ya kujifungua.

Mratibu wa  utepe mweupe mkoani Ruvuma Dk.Helmengild Mayunga anataja sababu ya kuwepo siku ya utepe mweupe Tanzania  kuwa ni kutokana na  Tanzania kuwa ni nchi mojawapo duniani yenye vifo vingi zaidi ya nchi nyingine vinavyotokana na  uzazi.

Utafiti uliofanyika kuanzia mwaka 1996,2004 hadi 2005 na mwaka 2009 hadi 2010 umebaini kuwa kila siku wanawake 20 wanapoteza maisha kutokana na tatizo la ujauzito ambapo watoto wachanga 32  kwa kila vizazi hai 1000 hufa kila mwaka  hapa nchini .

“Jambo la kuhuzunisha ni kwamba vifo hivi vinazuilika kama wataalamu wa afya wangelikuwepo wa kutosha na kufanyakazi katika vituo vya kutolea huduma vyenye vifaa vya  kutosha pamoja na madawa,ni asilimia 46 tu ya akinamama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya na kupata huduma za  kitaalam wakati wa kujifungua”,anasema Dk.Mayunga mratibu wa utepe mweupe mkoa wa Ruvuma.

Hata hivyo Dk.Mayunga anabainisha zaidi kuwa  vifo vya wajawazito vingepungua kwa kiasi kikubwa iwapo akinamama wote wangejifungulia katika vituo vya afya vilivyo na sifa za kuokoa maisha kwa ajili ya unafuu wa rufaa na kwamba takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 47 tu ya akinamama wajawazito wanajifungulia kwenye vituo vya afya.

Mmoja wa akinamama waliojifungua katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma akizungumzia huduma bora za uzazi alizozipata kabla na baada ya kujifungua kwa usalama.



Serikali kitaifa na mashirika mengi wamekuwa wakijishughulisha na uzazi salama, kuunganisha nguvu ni Muhimu hasa ngazi ya mikoa,wilaya na vijiji ,muungano wa utepe mweupe  unachangia katika kushirikisha jamii yote kuunganisha nguvu na kutetea uzazi salama.

Madhumuni ni kuhamasisha jamii katika ngazi zote ili watambue kupanga bajeti kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa makusudi ya kuhakikisha mama anajifungua salama,kujua stadi za kuokoa maisha kuanzia ngazi ya familia,pia kutambua dalili za hatari na kutafuta huduma salama wakati wa kujifungua ambayo ni haki yao.

Malengo mengine ni wanaume kuchukua majukumu thabiti kuhakikisha uzazi salama,wanawake wajawazito kuwa na mpango binafsi wa kujifungua na kuongeza watalaam wa afya ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya Utepe Mweupe  inasema kila mwanamke ana haki kusaidiwa na mtaaalamu wa afya anapokuwa anajifungua.

Dk.Mayunga anasisitiza kauli mbiu hiyo isaidie katika ongezeko la wataalam wa afya ili kila mwanamke ahudumiwe na kunusuru maisha ya mama na mtoto  wakati wa kujifungua na kwamba serikali na jamii iweke vivutio ili kuwavutia watalaamu wa afya kwa wingi  kama vile nyumba bora,vitendeakazi na maslahi bora.

Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Dk.Anselimo Tarimo ameipongeza wizara ya afya kwa kuamua kuadhimisha siku ya utepe mweupe kitaifa mkoani Ruvuma ambapo ameahidi serikali itaendelea  kutoa elimu ya  msingi ya afya kwa wananchi wote katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito katika mkoa wa Ruvuma vimepungua  ambapo takwimu zinaonesha kuwa kila  wajawazito 131 kati ya 100,000 wanakufa kutokana na matatizo ya uzazi ukilinganisha na vifo 175 kati ya 100,000  ambalo ni lengo la milenia hivyo mkoa wa Ruvuma umevuka lengo la milenia kwa idadi ya vifo kupungua .

Takwimu za kitaifa za mwaka 2004 zinaonesha kuwa vifo vya akimama wajawazito vilikuwa ni 578 kwa kila vizazi hai 1000.Kutokana na takwimu hizo inahitajika kuboresha mfumo wa utoaji huduma za uzazi ili kupunguza vifo vya akinamama kwa asilimia 75  kadri ya mpango wa milenia sanjari na kuelimisha jamii ili waweze kutumia huduma bora  za afya na uzazi wa mpango.

Hata hivyo  lengo la wizara ya afya ustawi wa jamii ni kuhakikisha kuwa hakitokei kifo hata kimoja cha mama mjamzito na kwamba takwimu za sasa zinaonesha kuwa asilimia 94 ya akinamama wajawazito ndiyo wanaohudhuria kliniki jambo ambalo ni hatari.
Simu 0766463129


No comments:

Post a Comment