Na Albano Midelo.
Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbuji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500 toka usawa wa bahari ambapo kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750,urefu wake ni karibu kilometa 1000 na upana mkubwa ni kilometa 80 ambapo upana mdogo ni kilometa 15.
Bonde la ziwa Nyasa linajumuisha eneo lote lenye mito ,ambayo inatiririsha maji kuingia katika ziwa Nyasa ,mito hiyo inatoka katika wilaya za Mbeya,Ileje,Rungwe,Kyela na Mbozi mkoani Mbeya.
Ofisa wa maji katika Bonde la ziwa Nyasa mhaidrojia Witgal Nkondora anasema Bonde hilo lina jumla ya wakazi 2,060,000 kutokana na sensa ya mwaka 2002 ambapo wananchi hao walio wengi wanaendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo hali inayosababisha kuharibu mazingira.
Hata hivyo anasema ofisi ya Bonde la maji ziwa Nyasa imeweka mikakati mizuri ya kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa aina yeyote kwa lengo la kufanya rasilimali ya maji haitoweki katika bonde la ziwa Nyasa na hivyo kuathiri viumbehai.
Nkondora anazitaja changamoto zinazolikabili bonde hilo kuwa ni uharibifu mkubwa wa mazingira na uchafuzi wa kutisha katika vyanzo vya maji ambao unafanywa na wananchi wanaozunguka katika bonde hilo kwa kuendesha shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Baadhi ya wachimbaji madini holela wakichafua chanzo cha maji cha mto kata ya Kigonsera wilayani Mbinga 
Kwa mujibu wa Nkondora maji salama huitwa yamechafuliwa endapo viasili vitakavyokuwa ndani ya maji,vinaweza kusababisha madhara ya kifya au kiuchumi kwa binadamu na viumbehai au hata kufanya maji hayo kuonekana hayana muonekano wa asili yaani yanakuwa na rangi au mtibuko au matope.
Njia nyingine za uchafuzi wa mazingira katika Bonde la ziwa Nyasa ni utupaji wa hewa chafu,utupaji holela wa maji taka ya majumbani,uharibifu wa njia asili,ongezeko la mifugo,ongezeko la watu na uchimbaji wa madini kiholela.
“Kama ilivyo katika mabonde mengine ya maji nchini ,Bonde la ziwa Nyasa limeathirika sana katika mazingira yake kutokana na shughuli za kilimo kisichokuwa endelevu na kisichozingatia utaalamu na wachimbaji wadogo wadogo wa madini hasa katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ”,anasema Mkondora.
Nkondora anabainisha zaidi kuwa binadamu na wanyama wanapokunywa maji yaliyochafuliwa na wanapotumia mimea huweza kupata madhara ya kifya ambapo viumbehai kama samaki na viumbe wengine huweza kupoteza maisha kutokana na uchafuzi huo maji na kwamba uchafuzi wa maji unaweza kusababisha binadamu kupata magonjwa mbalimbali kama kuhara,kipindupindu,kichocho,figo na kansa ya ngozi na homa za matumbo.
Akibainisha zaidi uharibifu wa mazingira katika Bonde hilo anasema mmomonyoko wa udongo hutokea pale ambapo udongo unapohamishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kwamba mmomonyoko hufanyika kwa urahisi zaidi kwenye ardhi isiyokuwa na uoto hasa ile iliyo kwenye mwinuko wa maeneo ambayo shughuli za kibinadamu hufanyika kama uchimbaji holela wa madini na kilimo holela.
Hata hivyo anasema vitendo vya binadamu kuharibifu mazingira ndiyo huleta athari mbaya ikiwa ni pamoja na kusababisha mmomonyoko wa udongo ,vitendo hivyo ni kama kukata miti ovyo kwenye vyanzo vya maji,kuchoma moto misitu na mapori na kulima kwenye vyanzo,kandokando ya mito na ndani ya mito.
Vitendo vingine vya uharibifu huo ni kuchimba ovyo mchanga wa mawe kwenye mito,matumizi mabaya ya madawa ya kilimo,utupaji wa maji taka mitoni,uchimbaji holela wa madini na hasa kutumia kemikali za hatari kama zebaki ambazo ni hatari zikiingia kwenye vyanzo vya maji bila kusahau kufuga wanyama wengi kuliko malisho yaliopo.
Iwapo athari za uchafuzi wa maji zitapungua basi umaskini nao utapungua katika kiwango kikubwa kuwa kuwa muda mwingi wananchi watatumia muda wao katika shughuli za uzalishaji mali ,isipokuwa sheria itabaki kuwabana wale wote wanaoharibu kwa makusudi vyanzo vya maji.
Mmoja wa wachimbaji wa madini katika kijiji cha Amani makoro wilayani Mbinga akiibuka kutoka katika shimo refu ambalo linachangia kuharibu mazingira kwenye maeneo ya machimbo 
Mhaidrojia huyo anasisitiza elimu ya kutunza na kuzitumia rasilimali za maji na kwamba wananchi hawana budi kudhibiti uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa aina yeyote,pamoja na kuhakikisha vyanzo vya maji vilivyopo haviharibiwi wala kuchafuliwa kwa njia yeyote ile kama uchimbaji holela wa madini,kulima,kuchoma misitu moto,kukata miti ovyo au kujenga kwenye vyanzo vya maji.
Anakumbusha kuwa uharibifu wa vyanzo vya maji mahali popote ni kinyume cha taratibu,kanuni na sheria za nchi,hivi sasa imefikia wakati kwa vyombo vinavyosimamia sheria kuamka na kuanza kuchukua hatua za haraka kwa wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira ya vyanzo vya maji ili kuwanusuru viumbehai wote ambao wanaishi kwa kutegemea mazingira bora ili kupata maji na mahitaji mengine muhimu kama chakula.
Barua pepe amidelo@yahoo.com
www.maendeleonivita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment