Monday, March 14, 2011

Kutana na mtoto mwenye vipaji vya ajabu,ana uwezo wa kukariri Biblia na kuisoma kwa kichwa

Mtoto Aloyce Milinga mkazi wa kijiji cha Mgazini wilayani Songea mkoani Ruvuma mwenye kipaji cha kukariri kitabu kitakatifu yaani Biblia na kusoma neno kwa neno mstari na mstari bila kukosea.pia ana kipaji cha kuimba na ametunga nyimbo za kiroho na kimwili ambazo baadhi zinarushwa kwenye vituo vya redio,kanisani amekuwa anasoma masomo siku ya Jumapili,anahitaji msaada wa kusaidiwa ada katika shule ya sekondari baada ya kudaiwa kufelishwa kwa makusudi darasa la saba mwaka jana licha ya kuongoza kila mwaka tangu akiwa darasa la kwanza picha na maelezo na Albano Midelo.
Na Albano Midelo.

Mtoto Aloyce  Milinga(14) ambaye amemaliza darasa la saba mwaka jana katika shule ya Msingi Mgazini Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma amebainika kuwa na vipaji mbalimbali kikiwemo cha kusoma Biblia kwa kichwa.

Mtoto akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa amebainika kuwa na uwezo wa kusoma kitabu kitakatifu kwa kichwa bila kukosea mstari wala neno ambalo lipo kwenye kitabu hicho.

“Nimekuwa nasoma masomo kanisani tangu nikiwa darasa la nne,nikishapitia Biblia takatifu nina uwezo wa kuisoma toka kichwani mstari kwa mstari na neno kwa neno bila hata kukosea watu wengi huwa wanashangaa lakini ni kipaji ambacho nimepewa na mwenyezi Mungu ili nimtumikie”,alisema mtoto huyo kwa akujiamini.

Licha ya kuwa na kipaji  hicho ,mtoto huyo pia anakipaji cha kuimba ambapo ametunga nyimbo mbalimbali za kiroho na za kijamii zenye ujumbe mzito kiasi kwamba unaweza kudhani kuwa ametungiwa ambapo tayari kuna nyimbo mbili amerekodi na hivi sasa zinasikika kwenye vituo vya redio Maria pamoja na Redio Jogoo ya mjini hapa.

“Nimeshatunga nyimbo nyingi,naweza hata kujaza albamu moja iwapo nitazirekodi,lakini kwanza nimemua kwanza nisome halafu mambo ya kuimba yatafuata baadaye kwa kuwa elimu ni jambo la kwanza katika maisha”,alisema.

Hata hivyo mtoto huyo ambaye alikuwa anaongoza kwenye mitihani yake tangu darasa la kwanza hadi la saba mwaka jana katika hali ya kushangaza licha ya darasa lake kufaulisha wanafunzi zaidi ya 20 yeye alifeli mtihani huo jambo ambalo anadai kuwa alichakachuliwa na mwalimu mkuu wake ili afeli.

Pichani ni Mtoto Aloyce Milinga mwenye vipaji vya ajabu,akiendelezwa anaweza kutoa mchango mkubwa katika taifa hili.

Hivi sasa mtoto huyo amepata shule ya sekondari binafsi wilayani Tunduru lakini hadi sasa anashindwa kwenda kujiunga na masomo ya sekondari kutokana na kukosa fedha za kutosha za ada,matumizi na nauli kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo ambapo analelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama yake .

Ametoa mwito kwa watu wote wenye mapenzi mema kumsaidia kwa kuwa bado shilingi 100,000 ili kutosheleza ada pamoja na fedha za matumizi na sare za shule ili aweze kwenda shule ambayo imefungua tangu mwanzoni mwa mwezi huu.
Simu 0766463129



No comments:

Post a Comment