Monday, March 14, 2011

Waziri mwenye dhamana ya mazingira aendesha operesheni kabambe ya usafi mjini Songea

Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais mazingira Dk.Terezya Luoga Huvisa akiwa mstari wa mbele katika operesheni ya kusitukiza ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga ambao wamejaza bidhaa zao kila upande kando kando ya barabara kuu ya Sokoine mjini Songea na kusababisha barabara kuwa finyu hivyo kuhatarisha maisha ya watembea kwa miguu pia ni uchafuzi wa mazingira.

Na Albano Midelo.
WAZIRI wa nchi ofisi ya makamu wa Rais Mazingira Dk.Terezya Luoga Huvisa  ameendesha operesheni kabambe ya kusafisha mji wa Songea kwa kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo yaani wamachinga katika barabara kuu ya Sokoine ya mjini hapa.

Waziri Dk.Huvisa Jumapili amefanya ziara ya kushitukiza katika barabara kuu ya Sokoine  ambayo ndiyo kioo cha mji wa Songea ambayo alikuta kila upande wamejaa wamachinga ambao walitandaza bidhaa zao hadi hifadhi ya barabara kuu na kuhatarisha maisha ya wananchi pamoja na kuleta kero kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo mjini Songea.
Kutokana na hali hiyo waziri  huyo akiwa ameongozana na mstahiki Meya wa manispaa ya Songea Ally Manya,mkurugenzi wa manispaa hiyo,pamoja na mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Ruvuma walianza operesheni kabambe iliyodumu kwa dakika 80 ya kuwasimamia wafanyabiashara hao kuondoa bidhaa zao zote walizopanga barabarani.

“Nakuagiza mkurugenzi wa manispaa ya Songea kwa kushirikiana na mstahiki meya hakikisheni kuanzia kesho meza zote za biashara ziondolewe pia hakikisheni kuwa wafanyabiashara hawa harudi tena kufanya biashara kando kando ya barabara kuu kwa kuwa licha ya kuwa hatari katika maisha lakini pia ni uchafuzi wa mazingira,waelekezeni waende sehemu ambazo zimeandaliwa rasmi kwa ajili yao”,alisisitiza.

Picha  wafanyabiashara ndogo ndogo wakiondoa bidhaa zao ambazo wamezipanga chini katika barabara kuu ya Sokoine mjini Songea  picha na Albano Midelo
Hata hivyo  waziri huyo anayeshughulikia mazingira ambaye pia ni mwenyeji wa Songea, anabainisha kuwa zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo wadogo kando kando mwa barabara kuu linafanyika katika nchi nzima hivyo amewaagiza wakurugenzi kusimamia usafi wa mazingira ili kuboresha mandhari ya miji yote nchini .

Waziri Dk.Huvisa anainua meza ya kupangia viatu akishiriki moja kwa moja katika operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo katika barabara kuu ya Sokoine mjini Songea,aliyebeba ubao ni mkurugenzi wa manispaa ya Songea.
“Mstahiki meya pamoja na Baraza zima la madiwani simamieni sheria za barabarani kuwabana wote ambao wataendelea kufanyabiashara katika barabara kuu hii ili wananchi  wanaotumia  wasiwe hatarini kwa kuwa wanaweza kugongwa  na vyombo vya moto,serikali inapenda wananchi wafanye biashara lakini katika maeneo yaliotengwa,tunafanya hivi kwa nia njema kabisa”,anasema.

Mstahiki Meya wa manispaa ya Songea Ally Manya ameahidi kusimamia suala hilo pamoja na usafi wa mazingira katika mji wa Songea ili mji huo uweze kurudi katika sifa ya kuongoza kwa usafi kitaifa pamoja na kuhakikisha kuwa afya za wananchi wa mji huo zinakuwa salama bila kupata magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu kutokana na uchafu uliokithiri.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wamempongeza waziri huyo wa mazingira kwa hatua ambazo amezichukua kuusafisha mji wa Songea  ambapo kwa kuanzia amewaondoa wafanyabiashara wa barabarani ambao walikuwa wametanda barabara kuu ya Sokoine mjini hapa wakifanyabiashara zao bila kuchukuliwa hatua zozote.

Gari la kubebea takataka katika manispaa ya Songea likiwa katika operesheni hiyo mahusus ya kusafisha mji wa Songea,aliyesimama ni bwana afya wa manispaa hiyo akitoa maelekezo kwa dereva.

Hata hivyo wananchi hao Mhamed Kudeka,John Mapunda na Ezabela Komba wametoa ombi kwa waziri huyo kutoa agizo la kuyaondoa pia magari makubwa na madogo ambayo yamekuwa yakiegeshwa kila siku katika barabara kuu hiyo na kuhatarisha maisha ya wananchi .

Waziri wa mazingira Dk.Huvisa anatoa maagizo kwa uongozi wa Halmashauri ya manispaa ya Songea kuhakikisha kuwa wamachinga hawarudi tena katika barabara kuu ya Sokoine mjini Songea.
Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo TCCI mkoani Ruvuma Mays Mkwembe alisema kuwa mji wa Songea una pikipiki zaidi ya 4000 ambazo zinatumia katika barabara kuu hiyo hali ambayo imesababisha wananchi kugongwa na wengine kupoteza maisha kutokana na ufinyu wa barabara unaochangiwa na magari kuegeshwa kando kando hivyo ameshauri wahusika kuchukua hatua za kumuunga mkono waziri wa mazingira kwa kuyaondoa magari hayo na kwenda kuyaegesha katika maeneo maalum kisheria.

Naye  Joseph Mbano mkazi wa mjini hapa alimwomba waziri huyo wa mazingira kutembelea katika stendi kuu ya mabasi ya Songea ambayo walidai kuwa haina hadhi ya kuwa stendi ya mkoa ambapo hivi sasa katika maeneo ya kuegesha mabasi wamejitokeza wafanyabiashara ndogo ndogo ambao wamekuwa wakiweka bidhaa zao kama samaki chini hali ambayo inataharisha afya kutokana na mazingira machafu kwa kuwa vumbi za magari yanayoingia katika stendi hiyo zinaishia kwenye vyakula hivyo ambavyo vinaliwa na walaji na kuhatarisha afya zao.

Simu 0766463129


No comments:

Post a Comment