Tuesday, March 15, 2011

SOUWASA na mkakati wa kuboresha maji katika manispaa ya Songea

Picha inaonesha eneo ambalo umejengwa mtambo wa kisasa wa maji uliogharimu shilingi bilioni 33.2 katika eneo la Matogoro manispaa ya Songea picha na Albano Midelo 











  Na Albano Midelo
MAMLAKA ya  maji safi na maji taka (SOUWASA) katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepiga hatua kubwa katika kufikisha huduma ya maji kwa wananchi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo zaidi ya miaka 11 iliyopita.

Kabla ya kuanzishwa kwa SOUWASA wananchi wa mji wa Songea walikuwa wanahangaika kwa kutembea umbali mrefu kutafuta maji hali iliyosababisha kushindwa kufanya kazi nyingine za maendeleo ili kuinua uchumi wao.

Kaimu meneja wa SOUWASA mhandisi Francis Kapongo  anasema mamlaka hiyo imepata mafanikio makubwa katika kuboresha huduma ya maji kwa wateja wake ikiwemo ukarabati wa vyanzo vya maji vya Ruvuma,Liwoyowoyo,Lipasi na Luhila B.

 Mafanikio mengine ni ujenzi wa mtambo mpya wa kuchuja na kutibu maji uliojengwa katika eneo la Matogoro uliyogharimu sh.bilioni 33.2 wenye urefu wa kilometa 6.2 na kipenyo cha milimita 300 aina ya chuma(DCI) na ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kuchuja,kusafisha na kutibu maji uliopo Matogoro.
                                      

Rais wa Zanzibar Dk.Ally Mohamed Shein akizindua mtambo wa kisasa wa kuzalisha maji katika eneo la Matogoro mjini Songea ambao unazalisha maji yenye viwango vya kimataifa.
Kapongo anayataja mafanikio mengine kuwa ni ukarabati,ubadilishaji na ulazaji wa mabomba ya usambazaji,ufungaji wa dira za maji kwa wateja kutoka dira 29 mwaka 1997/1998 hadi kufikia dira za maji 6240 kufikia mwaka 2009,2010,ukarabati wa matanki ya old treatment plant,maji ya wilaya  na kujenga kituo cha kusukuma maji Luhira Darajani chenye uwezo wa kusukuma maji kiasi cha lita 90 kwa sekunde.

Katika mfumo wa maji taka Kapongo anayataja mafanikio ambayo yamepatikana kuwa ni kujenga sehemu ya kupokea maji kwa wateja kutoka  mtandao wa maji taka yanayotolewa na magari ya kunyonya maji taka,kujenga mabwawa mawili ya uchujaji ambapo hatua ya kwanza ina ujazo wa mita 12,960 kila moja na kujenga mabwawa mawili ya uchujaji wa hatua ya tatu yenye mita za ujazo 4568 kila moja.

Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kujenga sehemu ya kukaushia taka,kujenga jengo la uendeshaji na matengenezo pamoja na kutengeneza mazingira ya mtambo,mabomba makuu ya uondoaji maji taka yenye kipenyo cha DN 400 sawa na nchi 16 na urefu wa kilometa 1.8,kulaza mabomba ya utoaji taka yenye kipenyo kati ya DN 200 na ND 300 sawa na nchi  8.12 na urefu wa kilometa tano.
  
Eneo ambalo maji yaingia kutoka chanzo cha maji cha mto Ruhila kilichopo kwenye milima ya Matogoro ambayo inategemewa na mamlaka ya maji safi na maji taka SOUWASA kuzalisha maji katika mji wa Songea
Mafanikio mengine ni kulaza mabomba madogo ya uondoaji maji taka kwenye mitaa mbalimbali yenye kipenyo cha kati ya DN100 na DN150 sawa na nchi kati ya nne na sita na urefu wa kilometa 22.6 pamoja na ununuzi wa vifaa kama mabomba,gari moja la kunyonya maji taka,toroli na jenerata.
Hata hivyo anazitaja changamoto ambazo zinaikabili SOUWASA kuwa ni pamoja na  uzalishaji mdogo wa maji katika kipindi cha kati ya mwezi wa septemba na Desemba kila mwaka,uharibifu kwenye vyanzo vya maji hususani kwenye vilivyopo milima ya Matogoro pamoja na changamoto ya mtandao mdogo wa uzalishaji maji katika manispaa ya Songea unaofikia asilimia 56.

“Tumeweka mikakati ya kuondokana na changamoto hizo ili kuongeza uzalishaji wa maji kutoka huduma ya sasa ya milimita 6570 hadi kufikia milimita 10280 ifikapo Julai 2010,kusambaza maji maeneo ya Making’inda,Msamala,Ruhuwiko,Mkuzo,Ruvuma,Mshangano na Mateka kwa ajili ya kupandisha kiwango cha usambazaji maji kwa wananchi kutoka asilimia 56 mwaka 2003 hadi 82 hivi sasa”,anasema.

Kwa upande wake ofisa uhusiano wa SOUWASA Silas Bwena anasema tangu mamlaka hiyo iboreshe huduma za maji katika mji wa Songea tayari imetoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na matumizi bora ya maji ili kuhakikisha kuwa wananchi wanatambua kuwa rasilimali ya maji inakuwa endelevu kutokana na ukweli kuwa maji ni uhai.

Baadhi ya maeneo muhimu ya kuchuja maji kwenye mtambo wa kisasa wa Matogoro chini ya SOUWASA
Bwena anabainisha kuwa jumla ya wananchi 276 ambao ni sawa na asilimia 63.48 mwaka jana walitembelea katika banda lka SOUWASA wakati wa wiki ya nanenane   ambao walipewa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kupewa vipeperushi ambavyo pia vilitoa elimu ya namna ya kujiunga na mfumo wa maji taka na faida zake.
 Anaongeza kuwa SOUWASA pia  imekuwa inatoa elimu ya matumizi bora ya maji kwa wanafunzi mbalimbali wa shule za msingi na sekondari katika manispaa ya Songea pamoja na kufanya vikao na madiwani wa Halmashauri ya manispaa ya Songea na wenyeviti wa serikali za mitaa kwa lengo la kutoa elimu ya matumizi bora ya maji na kutunza miundombinu na vyanzo vya maji.

Hili sio ziwa bali ni bwawa la kisasa ambalo limejengwa na SOUWASA ambalo hutumika kupokea maji kutoka vyanzo vya maji kwenye milima ya Matogoro kisha kuyachuja na kuyatibu kabla ya kusambazwa kwa watumiaji,ni sehemu nzuri ya kuvutia hata kwa utalii

Naye kaimu meneja wa ufundi wa SOUWASA mhandisi John Kapinga akizungumzia mitambo ya kisasa ya kuchuja maji taka anasema inapokea maji taka kutoka kwa wateja wao na kupelekwa katika bwawa la pili na la tatu ambako maji huchujwa na kuwauwa bacteria kwa mwanga wa jua na maji hayo kuchujwa tena na kurudi mtoni yakiwa safi na salama kwa matumizi ya kibinadamu.

“Mfumo huu wa SOUWASA wa kuchuja maji taka  ni wa kisasa na wa tatu kwa ubora Tanzania,wa kwanza upo Arusha,wa pili upo Moshi na huu wa tatu upo Songea,ukifika katika eneo ambalo upo mtambo huu linavutia sana ukitembelea utadhani ni ziwa,maji taka yakishachujwa takataka zinatolewa kwenye chujio na kuchomwa moto ambapo jivu lake hutumika kama mbolea ambayo ni bora kuliko ya viwandani”,anasisitiza.
Simu 0766463129






No comments:

Post a Comment