Tuesday, March 15, 2011

Waziri wa mazingira aagiza uvunaji wa miti katika msitu wa Matogoro usimamishwe ili kuunusuru mji wa Songea kugeuka jangwa

Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais mazingira Dk.Terezya Luoga Huvisa akitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa uvunaji usiokuwa endelevu unasimamishwa katika msitu wa serikali wa milima ya Matogoro ili kuunuru mji wa Songea kugeuka jangwa picha na Albano Midelo
Na Albano Midelo.
UVUNAJI wa miti usiokuwa endelevu unaoendelea kufanywa katika msitu wa serikali wa milima ya Matogoro nje kidogo ya mji wa Songea mkoani Ruvuma umemfanya waziri nchi katika ofisi makamu wa Rais mazingira Dk.Terezya Luoga kumuagiza mhifadhi wa msitu huo kusimamisha zoezi  la  kuivuna miti hiyo .

Uvunaji wa miti hiyo umepewa kibali na wizara ya maliasili na utalii kupitia idara ya misitu na nyuki kuhakikisha kuwa miti yote iliyopo katika msitu huo ambao unategemewa na mji wa Songea kwa kuwa una vyanzo vya maji vya mito ya Ruhila pamoja na mto maarufu wa Ruvuma ambao unaanzia katika mlima wa Matogoro na kumwaga maji yake kwenye bahari ya Hindi.

Waziri Dk.Huvisa akiwa katika msitu huo alitamani kutoa machozi kutokana na uvunaji wa miti katika msitu huo hali ambayo ilimlazimu wakati  wote kuwa mkali na kukataa taarifa ambazo zilikuwa zinatolewa na wahifadhi wa msitu huo kutokana na kutozingatia uvunaji endelevu  wa msitu huo  mkongwe ambao ulianzishwa tangu wakati wa serikali ya wakoloni.
Mashine yenye uwezo wa kuvuna miti zaidi ya 150 kwa siku ikitumiwa na wafanyabiashara wa miti katika milima ya misitu ya Matogoro
 Hata hivyo Dk.Huvisa anasema anakubaliana na utafiti ambao umefanywa wa kuhakikisha kuwa miti yote iliyopo hivi sasa inavunwa na kupandwa miti ya asili ambayo ni rafiki wa maji,hata hivyo hakubaliani kabisa na uvunaji wa miti usiokuwa endelevu ambao unafanywa na wafanyabiashara katika msitu huo huku watunzaji wa msitu huo wakiwa hawajapanda miti katika maeneo waliovuna hali ambayo inataharisha usalama wa viumbehai pamoja na wananchi wa mji wa Songea kuwa katika hatari ya kukosa maji miaka michache ijayo.

“Mimi ni mzaliwa wa Songea, miaka yote tumekaa Songea na misitu hii ya Matogoro, hatujawahi kukosa maji,lakini hivi sasa wakati wa kiangazi mji wa Songea unapata upungufu mkubwa wa maji hadi siku nne,kunakuwa na mgawo mkali wa maji hizi ndizo dalili za awali za uharibifu wa mazingira kwenye msitu huu kwa kuwa mnafanya uvunaji usiokuwa endelevu,haiwezekani kuvuna miti wakati hakuna vitalu vya miti ambavyo mmeviandaa kupanda katika maeneo ambayo tayari mmevuna”,anasisitiza waziri huyo wa dhamana ya mazingira nchini.

Mbao ambazo tayari zimevunwa kwenye msitu wa serikali wa milima ya Matogoro ambazo zinasubiriwa kusafirishwa na kuingizwa sokoni
“Mimi nafahamu miti aina ya mikaratusi inaharibu vyanzo vya maji lakini hauwezi kuiondoa miti hiyo bila kuwa na mbadala,ninyi watu wa misitu mnafikiria pesa tu kukitokea uharibifu  sisi wizara ya mazingira tunabebeshwa msalaba mimi siwezi kukubali uharibifu huu uendelee mlima umebakia vipala tu hili jambo tayari limemfikia makamu wa Rais ndiyo maana mimi kama waziri mwenye dhamana ya mazingira nipo hapa sasa  nataka kujua kama wizara inaruhusu watu wavune miti bila kupanda miti mingine  mimi sielewi”,anasisitiza.

Uchunguzi uliofanywa kwa kufanya mahojiano na wavunaji wa misiti katika msitu wa Matogoro umebaini kuwa kwa siku wanavuna miti zaidi ya 150 na kwamba katika eneo hilo wanavuna miti kwa siku 30  ambapo awali wavunaji waliopewa kibali katika msitu huo walikuwa 19 na hivi sasa wavunaji waliobakia wapo sita tu hata hivyo kasi ya uvunaji wa miti hiyo inatishia mji wa Songea kuwa jangwa endapo uvunaji endelevu hautapewa kipaumbele. 

 Uchunguzi umebaini kuwa mgogoro wa kiutendaji unaoendelea katika msitu wa serikali wa milima ya Matogoro uliopo ambao bila shaka unazikabili wizara tatu sasa ambazo ni wizara ya maliasili na utalii,wizara ya maji na wizara ya mazingira ambapo kila wizara inafanyakazi kulingana na taratibu zao kitaaluma bila kujali athari za kimazingira ambazo zinaweza kutokea iwapo wizara hizo hazitakaa meza moja na kutafutia ufumbuzi wa kina suala hilo..

 Msitu wa serikali wa Matogoro unamilikiwa na kuhifadhiwa na wizara ya maliasili na utalii tangu miaka 1960 ambapo wizara ya maji  kupitia mamlaka ya maji safi na maji taka Songea SOUWASA pia  wanatumia vyanzo vya maji vilivyopo kwenye msitu wa Matogoro kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi wa mji wa Songea wakati wizara ya mazingira ambayo ipo chini ya makamu wa Rais inasimamia mazingira.

Milima ya Matogoro licha ya kukabiliwa na uvunaji wa miti usiokuwa endelevu pia unakabiliwa na changamoto ya uchomaji moto holela ambapo karibu kila mwaka maelfu ya hekta za miti huteketea kwa moto na kusababisha uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji vya mito ya Ruhila na Ruvuma hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe hai waliopo kwenye milima hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa watalaamu kutoka wizara ya maliasili na utalii  utafiti uliofanywa na watalaamu wa mazingira kutoka nchini Ujerumani mwaka 2000 umebaini kuwa miti aina ya mikaratusi na mibani iliyopandwa kwenye msitu huo inapunguza maji kwenye vyanzo, kuchafua maji  na kusababisha kupoteza rangi yake ya asili  pamoja na kusababisha mmomonyoko wa udongo kutokana na maji mengi kushindwa kuzama ardhini.

 Ofisa wa maliasili wa mkoa wa Ruvuma Enock Buja anasema shamba la miti la serikali la milima ya Matogoro lilianzishwa miaka ya 1950 likiwa na  hekari 2259 aina ya mikaratusi na mibani ambapo kutokana na utafiti uliofanywa na Wajerumani mwaka 2000 ulibaini kuwa miti hiyo sio rafiki ya vyanzo vya maji hivyo hivyo serikali ilitoa kibali kwa uongozi wa hifadhi ya msitu wa milima ya Matogoro kuvuna miti hiyo na kupanda miti ya asili.

“Mkataba wa kuvuna miti hiyo unatakiwa ukamilike mwaka 2012 kwa kuhakikisha miti yote ya kupanda  inavunwa na kupanda miti ya asili   ili kuepusha vyanzo vya maji katika milima hiyo visikauke kutokana na athari za miti hiyo kuonekana kuathiri vyanzo vya maji katika milima ya Matogoro ambavyo vinategemewa na Mamlaka ya maji safi na maji taka Songea SOUWASA kuzalisha maji kwa wananchi wa mji wa Songea”,anasisitiza.

Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais mazingira Dk.Terezya Luoga Huvisa akikagua msitu wa serikali wa matogoro ambao umefanyiwa uharibifu mkubwa wa mazingira
Msitu wa serikali wa milima ya Matogoro unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uchomaji holela wa moto karibu kila mwaka hali ambayo inasababisha maelfu ya miti ya asili  kuteketea kwa moto,pia wananchi wanaozunguka msitu huo bado wanaendelea  kulima mbogamboga katika vyanzo vya maji  pamoja na kupulizia dawa za kuulia wadudu kwenye mbogamboga hizo zenye kemikali zenye sumu zinazochuruzika na kuingia kwenye vyanzo vya maji hali ambayo inahatarisha maisha ya viumbehai wakiwemo binadamu.

Mkurugenzi wa misitu na nyuki wa wizara ya maliasili na utalii  Dk.Felician Kilahama anasema anasema wavunaji wa miti katika msitu huo  walikuwa wanavuna miti hiyo kwa kuzingatia utaratibu ambao uliwekwa na serikali kulingana na maagizo ya wizara ya maliasili na utalii.

Anabainisha kuwa wizara iliagiza kuvunwa miti yote aina ya  mikaratusi na misonobari iliyopandwa  kwenye msitu huo katika shamba lenye ukubwa wa hekta 3.8 kutokana na utafiti kubaini kuwa miti hiyo sio rafiki ya vyanzo vya maji na kwamba wizara ya maliasili katika idara ya misitu na nyuki  mwaka 1978  mwaka 1978 kwenye msitu huo ilipanda hekta 867.2 za miti aina ya mikaratusi na misonobari kwa ajili ya kupata nguzo na mbao laini.
Mkoa wa Ruvuma una misitu 15 iliyohifadhiwa kisheria kwa ajili ya vyanzo vya maji na bioanuai mbalimbali yenye ukubwa wa hekta 680,000 ambapo msitu wa Matogoro pekee unakadiriwa kuwa na  ukubwa wa hekta 4800.
Simu:0766463129.
Website;www.maendeleonivita.blogspot.com
              
                                           



No comments:

Post a Comment