Thursday, March 17, 2011

Uharibifu wa mazingira migodini unavyoathiri barabara ya Songea-Mbinga

Athari za uharibifu wa mazingira kutokana na uchimbaji holela wa madini katika kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoani Ruvuma picha zote na Albano Midelo
-Barabara ya Songea-Mbinga ipo katika hatari ya kumeguka
Na Albano Midelo.
MOJA ya maeneo ambayo uharibifu wa mazingira umekithiri na kuleta hofu kubwa kwa wanaharakati wa mazingira ni katika  kata ya Kigonsera wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kwenye maeneo ya gereza la Kitai,Ngembambili na Amanimakoro ambapo wachimbaji wa madini katika maeneo hayo wameharibu mazingira katika kiwango kinachotishia usalama wa viumbehai.

Wachimbaji hao wamevamia katika eneo la gereza la Kilimo Kitai ambalo lina hekta zaidi ya 3000 ambapo  inadaiwa zaidi ya hekta 1200 zimeharibiwa na kusababisha uharibifu mkubwa wa ardhi pamoja na kuchafua vyanzo vya maji vilivyopo katika eneo hilo.

Uchunguzi uliofanywa katika maeneo ya Ngembambili na Kitai  umeonesha kuwa  wachimbaji hao wa madini kiholela wamechimba mashimo marefu chini kwa chini ambayo  yamevuka barabara kuu ya Songea –Mbinga na kuingia upande wa gereza la Kitai ambako kunadaiwa kuna mkondo wa madini mengi aina ya safaya na kisheria hairuhusiwi kuchimba madini katika eneo hilo la jeshi la magereza .

Hali hiyo ya uharibifu wa kutisha wa mazingira isipodhibitiwa mapema inatishia usalama wa barabara hiyo inayounganisha mikoa ya kusini ambapo hivi sasa ukifika karibu na daraja la Ngembambili mpakani na gereza la Kitai, dalili za kuanza kutitia  kwa barabara hiyo zimeanza kujitokeza  hali inayoleta wasiwasi katika barabara hiyo kubomoka na kusababisha athari za kimazingira na kiuchumi.
 katika picha inaonesha uharibifu wa mazingira  eneo la Kitai unavyotishia mazingira ya viumbe hai wakiwemo binadamu
Ikumbukwe kuwa barabara hiyo ya Songea-Mbinga ndiyo inaunganisha ukanda wa Mtwara korido kutoka Mtwara hadi bandari ya Mbambabay iliyopo ziwa Nyasa hivyo basi uharibifu huo unaoendelea kufanywa na wachimbaji holela wa madini jirani kabisa na hifadhi ya barabara unatakiwa udhibitiwe mapema ikiwa ni pamoja na kutoa elimu sahihi ya uchimbaji wa madini pamoja na kuwakamata wale wote wanaokiuka sheria hizo.

Ofisa wa bonde la ziwa Nyasa  Witigal  Mkondora ambaye anasimamia pia wilaya za Songea na Mbinga anasema Uchimbaji huo  wa madini ni miongoni mwa  shughuli za kibinadamu zinazoharibu sana mazingira na hasa katika vyanzo vya maji ambapo maeneo yote yaliovamiwa kwa ajili ya kuchimba madini yameathirika na inakuwa vigumu kuendesha shughuli nyingine zenye manufaa kwa binadamu.

“Uharibifu wa mazingira migodini na uchafuzi vyanzo vya maji huyaacha maeneo hayo yakiwa mashimo wazi,miti huteketezwa na kemikali hatari huchuruzika na kuathiri vyanzo vya maji na hivyo kuhatarisha maisha ya viumbehai”,anasisitiza Mkondora.

 Baadhi ya wachimbaji madini katika eneo la Ngembmbili wakisafishia madini kwenye mto na kuathiri chanzo cha mto pamoja na watumiaji wa mto huo

Mwenyekiti wa asasi inayoendesha shughuli za kijamii katika maeneo ya migodi inayoitwa Tanzania Mineral Mining Fund(TMMTF) Wilbert Mahundi  anabainisha  kuwa wachimbaji wa madini hawazitii serikali za vijiji badala yake wanawaheshimu maafisa wa madini pekee hivyo kutokana na changamoto hiyo ameshauri wizara ya madini kuiga mfumo wa wizara ya maliasili na utalii ambao unatoa fursa kwa kila kijiji kuweza kumiliki rasilimali hivyo kumpa hamasa za kuzitunza,kuzisimamia na kuzilinda.

“Mimi nimeshuhudia wachimbaji haramu wa madini wanakaa nje ya mipaka ya jeshi la magereza Kitai na wanachimba chini kwa kwa chini kuvuka barabara ya Songea Mbinga ili kujaribu kutafuta madini wakiwa chini bila kuonekana na askari juu,wachimbaji hao wanapiga fonka yaani kuzamia chini kwa chini  na kufanya wizi wa madini kwa sababu ya eneo la kambi la magereza Kitai ambalo linadaiwa na madini aina ya safaya lina mipaka yake na hairuhusiwi kufanya chochote ndani ya mipaka ya jeshi”,anasisitiza.

Uchimbaji wa madini kwa njia ya fonka ambao unafanywa kwa wachimbaji kuchimba chini kwa chini kuvuka barabara ya Songea-Mbinga  na kuiba madini huku athari za mazingira ya zikiwa zimeanza kujitokeza

Mahundi amelitaja tatizo liliosababisha kuendelea kwa uchimbaji holela wa madini katika kata ya Kigonsera kuwa  mfumko wa wachimbaji wasiokuwa na leseni ambao wanakadiriwa kufikia zaidi ya 4000 katika kata ya Kigonsera hivyo kuchimba madini katika maeneo ambayo sio rasmi na kwamba watu  wanachimba kiholela kutokana na serikali za vijiji kushindwa kusaidia kusimamia uchimbaji katika maeneo yao.

Anadai kuwa viongozi wa vijiji wanahitaji zaidi kushirikishwa ili kuepukana na wachimbaji holela ambao wanavamia hata maeneo ambayo kijiji kilipanga kwa ajili ya matumizi mengine na kwamba tatizo bado lipo kwenye wizara ya madini kuwashirikisha viongozi wa vijiji ili kuleta mfumo wa pamoja  utakaowezesha kusimamia shughuli za uchimbaji wa madini,ardhi na mazingira Tanzania.

 Kwa upande wake ofisa wa madini katika mkoa wa Ruvuma Stanislaus Mtalemwa anasema uharibifu wa mazingira katika maeneo ya machimbo kata ya Kigonsera  unatokana na wachimbaji haramu ambao wamekuwa  wanapuuzia hasa kuacha kufukia mashimo mara baada ya kuchimba mashimo ingawa  wanapewa elimu ya mazingira.

Anaongeza kuwa elimu hiyo ya udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika maeneo ya madini kwa kiwango kikubwa imeweza kuwabadilisha baadhi ya wachimbaji hata hivyo kutokana na maeneo hayo kufikiwa na wageni mbalimbali ambao wanatoka mikoa mingine  ili kuendesha kazi ya uchimbaji wa madini,uharibifu huo umekuwa unaendelea.

 Wachimbaji wa madini kutoka maeneo ya Ngembambili na Amanimakoro ambao ni Said Juma,Isack Salum,Manji Isack na John Kamwene wanadai kuwa wanafanyakazi ya uchimbaji katika mazingira magumu hasa kutokana na ukosefu wa vitendeakazi ambapo kuchimba shimo moja huwachukua siku hadi 60 na kufanya uharibifu mkubwa kutokana na mashimo marefu.

Wanadai kuwa wamekuwa wanachimba madini kwa kutumia uzoefu walioupata katika maeneo mbalimbali ikiwemo nje ya nchi na hawajawahi kupata elimu ya mazingira na kwamba hawapati ushirikiano wowote kutoka katika serikali za vijiji na kwamba wao wakichimba na kufanikiwa kupata madini wanaondoka bila kufukia mashimo.

Athari za kutitia kwa barabara ya Songea-Mbinga zimeanza kujitokeza katika daraja la Ngembambili wilayani Mbinga ambapo  uchunguzi umebaini kuwa barabara imeanza kutitia na endapo hatua hazitachukuliwa kuna hatari ya barabara hiyo kubomoka.

Afisa maliasili wa wilaya ya Mbinga Peter Mdaki  anasema katika maeneo ya Kitai,Ngembambili,Amani makoro,Dapori na Masuguru vijana wengi kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi wanafanya kazi ya uchimbaji wa madini kiholela na cha kusikitisha ni kwamba katika maeneo hayo vyanzo vya maji vimevamiwa na kutumika kusafishia madini bila kujali uharibifu  mkubwa wa mazingira unaotokea.

Kwa mujibu wa kanuni ya madini ya mwaka 1999 inamtaka mwenye leseni ya kuchimba madini  atumie mawe yasiyohitajika kujaza mashimo yalichimbwa au kuyajengea uzio mashimo yote ambayo shughuli za uchimbaji hazifanyiki na kwamba mwenye leseni ya biashara ya madini  anatakiwa kujenga  mabwawa ya kuoshea na kwamba mabwawa hayo yasiwe karibu na mito,vijito,visima au sehemu nyingine za maji  na ufyekaji miti kamwe  usifanyike kabisa kwenye eneo la mita 20 kutoka ukingo wa mito.

Serikali ya mkoa wa Ruvuma imewaagiza wakuu wa wilaya zote kusimamia na kufuatilia uharibifu huo wa mazingira migodini na wahusika wote kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.
Simu 0766463129
                            








No comments:

Post a Comment