Tuesday, March 29, 2011

Nyota iliyoanguka Mbozi sasa kuendelezwa ili kukuza utalii kusini

Picha ya nyota iliyoanguka katika kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi ambayo ni kivutio adimu na cha kipekee ulimwenguni,hata hivyo ni changamoto kwa idara ya mambo ya kale kuiendeleza
Na Albano Midelo.
IDARA ya  mambo ya kale kwa kushirikiana na idara ya makumbusho ya Taifa chini ya wizara ya maliasili na utalii hatimaye  inatarajia kukiendeleza kimondo cha Mbozi mkoani Mbeya ambacho ni kivutio adimu cha utalii  ulimwenguni.

Mkurugenzi msaidizi wa mambo ya kale Dk.Digna Tillya kutoka makao makuu jijini Dar es salaam anasema serikali imedhamiria  kuviendeleza vivutio vyote ambavyo ni vya kihistoria na kiutamaduni ambavyo vimetambuliwa kwa kuwa ni urithi wa Taifa katika kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Dk.Tillya anasema Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii katika mambo ya kale vingi vikiwa katika maeneo ya vijijini,mfano wa vivutio hivyo ni nyayo za binadamu wa kale ambazo zimegundulika sehemu mbalimbali nchini,nyota au vimondo kutoka anga za mbali ambavyo vimeanguka katika sehemu mbalimbali nchini,magofu ya kale,mawe ya ajabu,nyumba za makumbusho pamoja na vivutio vingine.

Picha inaonesha choo ambacho kinatumika kwa watalii ambao wanatembelea kivutio cha utalii cha kimondo cha Mbozi mkoani Mbeya,ni changamoto kwa wizara ya maliasili na utalii


Mkurugenzi huyo wa mambo ya kale amesema nyota ilianguka katika kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi mkoani Mbeya ni moja ya vivutio adimu vya mambo ya kale na kusisitiza kuwa sio kweli kwamba serikali imekisahau kivutio hicho bali ilikuwa inajipanga kuhakikisha kuwa kivutio hicho kinaendelezwa ili kuvutio watalii wa ndani na nje.

“Hatujaisahau nyota iliyoanguka Mbozi,serikali kupitia idara ya mambo ya kale tumejipanga na tunatarajia hivi karibuni kupeleka nguvu kubwa ya kuhakikisha kuwa mandhari ya  eneo ambalo nyota hiyo imeanguka yanaboreshwa na  kuvutia watalii wengi ambao wanakwenda kuangalia nyota hiyo iliyoanguka miaka mingi iliyopita ili wananchi na serikali iweze kupata kipato”,anasisitiza Dk.Tillya.

Awali mwandishi wa makala haya alikwenda kufanya uchunguzi katika eneo ambalo nyota hiyo imeanguka na kubaini kuwa idara ya mambo ya kale imeisahau nyota hiyo ambayo ni kivutio cha utalii licha ya kuwa na vivutio lukuki vya utalii hasa kutokana na kuanguka toka angani mwaka 1840 katika kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi mkoani Mbeya yenye uzito wa tani 12 ikiwa ni ya nane kwa ukubwa duniani kati ya nyota au vimondo zaidi ya 600 vilizoanguka toka angani.

Mwandishi wa makala haya akiwa katika kivutio cha utalii ambacho ni nyota iliyoanguka katika kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi mkoani Mbeya
Uchunguzi huo ulibaini kuwa kivutio hicho licha ya kuwa ni adimu na cha kipekee hakuna jitihada za makusudi ambazo zimefanywa kukihifadhi,kukitangaza na kukiendeleza ili kuvutia idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje hali ambayo ingeweza kuinua kipato kutokana na viingilio ambavyo wangelipia watalii pamoja na kutoa ajira endapo maeneo hayo yangendelezwa kwa kujenga hoteli,usafiri kwa watalii na nyumba za kulala wageni.

 Miongoni mwa wadau muhimu waliotoa maoni yao katika uchunguzi huo ni Keneth Mwazembe  mkazi wa Vwawa Mbozi ambaye   alisema licha ya nyota au kimondo kuanguka kwa miaka mingi katika kijiji cha Ndolezi wilayani humo idara ya mambo ya kale imeshindwa kukiendeleza kimondo hicho ambacho kinaongoza kwa ukubwa kuliko vimondo vyote hapa nchini hivyo kuwa kivutio adimu ulimwenguni.

“Kwa kweli nyota hii licha ya kuwa na sifa nyingi ,mahali kilipo ni pa wazi kabisa,hakijaendelezwa kwa kujengewa uzio,mtu akipita barabarani anakiona hivyo hata haja ya kutoa ada ya kiingilio inaonekana haina sababu,lakini iwapo nyota hiyo ingeendelezwa pamoja na eneo lenyewe kuboreshwa,kujenga hoteli na vivutio vingine serikali ingepata pesa nyingi na wananchi wangepata maendeleo makubwa kiuchumi”,anasisitiza Mwazembe.

.“Wizara ya maliasili na utalii,Bodi ya utalii Tanzania inajua sifa za kimondo hicho lakini mimi nasema bado hatua za kukitangaza na kukiendeleza hazijafanyika ipasavyo kwa mfano hata watalii ambao wanafika hapa kwenye kimondo wanafikia kwanza Iringa kwa kupewa waongoza watalii wa Iringa ili kuwaleta hapa Mbozi kwa kweli hili ni kosa walitakiwa waje moja kwa moja Mbeya ndiyo waongozwe kuletwa hapa Mbozi”anasema.

Mhifadhi msaidizi wa idara ya mambo ya kale katika Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Filmerick Bassange ambaye anahusika na uhifadhi wa kimondo cha Mbozi anasema licha ya kimondo hicho kukabiliwa na changamoto mbalimbali,serikali imeweza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kukiingiza kimondo kwenye sheria ya mambo ya kale mara baada ya uhuru mwaka 1964 hivyo kukitambua na kutoa ulinzi ili kisiendelee kuhujumiwa.

Basange anabainisha zaidi kuwa mwaka 1967 serikali iliamua kuchimba eneo ambalo kimondo hicho kilianguka na kujengea msingi ambapo kabla ya hapo kimondo hicho kilikuwa kinaonekana sehemu ndogo ya juu ambapo robo tatu ya kimondo hicho ilikuwa imezama ardhini wakati kinaanguka toka angani .

“ Uboreshaji wa eneo la kimondo unaenda hatua kwa hatua,historia ya vivutio vya utalii vya kiutamaduni na mambo ya kale vilivyotambuliwa vipo sehemu mbalimbali hapa nchini,ukivitembelea vivutio hivyo bado havijaendelezwa hata kufikia nusu ya uendelezaji wa kimondo,katika mkoa wa Mbeya vivutio vipo  vingi  mfano nyayo wa binadamu wa kale,michoro ya kale,ziwa la Mungu,maji moto hebu nenda ukaangalie hakuna kitu chochote ambacho kimeendelezwa”,anasisitiza.

Philipo Maligisu ni mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa anasema kimondo cha Mbozi ni kivutio adimu ukilinganisha na vimondo vingine vilivyoanguka sehemu mbalimbali ulimwenguni kikiwemo cha nchini   ambacho kilionekana wakati kinaanguka kina asilimia ndogo sana ya madini ya chuma ukilinganisha na kimondo cha Mbozi chenye madini ya chuma kwa zaidi ya asilimia 90.
.
 Maligisu anasema eneo la kimondo likiendelezwa linaweza kuwa chanzo cha kupunguza umaskini wa kipato kwa kuwa  watalii wanapotembelea wanalipa kiingilio,watalipia chakula ambacho kitauzwa kwa watalii na watalipia usafiri pamoja na vifaa mbalimbali vya kiutamaduni kama vinyago na vifaa vingine vya asili ambavyo wanaweza kuviuza kwa watalii hao.

“Kazi kubwa inayotukabili sisi watumishi wa wizara ya maliasili na utalii hasa katika idara ya mambo ya kale na makumbusho kwa ujumla katika nchi nzima kuongeza nguvu za ufahamu  na elimu ya utalii kwa wananchi kuweza kutambua  malikale zilizopo katika maeneo yao kama kimondo,pamoja na kuvitangaza ili vifahamike ndani na nje ya nchi,watalii wengi watamiminika na serikali itaongeza pato lake mara dufu”,anasema.

Simu 0766463129
http://www.maendeleo/nivita.blogspot.com














No comments:

Post a Comment