Monday, March 7, 2011

WWK-Kitaifa kanisa la TAG-Galilaya Ruhuwiko Songea yafana




Picha inaonesha wanawake watumishi wa kristo WWK katika kanisa la Galilaya Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma siku ya sikukuu ya WWK Kitaifa  iliyofanyika katika kanisa hilo wakimkabidhi mchungaji wao Gastor Nguya vifaa vya ujenzi aliyekamata microphone ni mke wa mchungaji huyo Rose Nguya picha na Albano Midelo.
-Mchungaji azawadiwa vifaa vya ujenzi
Na Albano Midelo.
WANAWAKE watumishi wa kristo WWK katika kanisa la Tanzania Assembles Of God Galilaya Songea mkoani Ruvuma wameadhimisha sikukuu hiyo kitaifa kwa kujikumbusha majukumu mbalimbali ya wanawake katika kanisa na jamii.

Mchungaji kiongozi wa TAG Galilaya Gastor Nguya ambaye pia ni mwangalizi wa TAG ukanda wa Songea  akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa  sikukuu ya akinamama kitaifa Jumapili hii alisisitiza kuwa wanawake ni watu muhimu katika kanisa na jamii kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa wanaoutoa kimwili na kiroho.

“Kanisa ambalo halina wanawake hilo sio kanisa kwa kuwa litakuwa halina mapambo wala kupendeza, kutokana na umuhimu wa wanawake kanisa la TAG duniani mwaka 1923 kule nchini Marekani liliamua kuanzisha chama cha kwanza kwa ajili ya kuwaangalia na kuwasimamia wanawake ,hapa Tanzania kanisa la TAG liliamua kuanzisha idara ya wanawake ili  wajifunze namna ya kumtumikia Mungu”,alisema.

Naye mwenyekiti wa WWK katika kanisa la Galilaya Evodia Mahay  amewaasa wanawake wote nchini kuwaheshimu waume zao pamoja na kuwahudumia kadri ya uwezo hao ili kulinda ndoa zao na kuwataka wanaume nao siku zote kuhakikisha kuwa wanatoa huduma kwa wake zao pamoja na kujali familia zao.
Mchungaji wa kanisa la TAG-Galilaya Songea Gastor Nguya akiwa na mkewe Rose Nguya ndani ya kanisa  muda mfupi kabla ya kukabidhiwa zawadi na WWK siku ya sikukuu ya WWK kitaifa picha na Albano Midelo.
Hata hivyo Mahay alilitaja lengo la siku ya wanawake watumishi wa kristo ambayo huanzimishwa mara moja kila mwaka kuwa ni kuonesha vipaji mbalimbali walivyonavyo wanawake pamoja na kumtegemeza mchungaji na familia yake sanjari na kutunisha mfuko wa Taifa wa kanisa hilo.

Mwenyekiti huyo aliyataja baadhi ya mafanikio ambayo WWK katika kanisa la Galilaya wameyapata kuwa ni pamoja na  kufanikiwa kumpeleka kiongozi wao kwenye mkutano mkuu wa kanisa hilo Makambako mkoani Njombe,kumtegemeza mchungaji wao vitu mbalimbali pamoja na familia yake na kulitegemeza kanisa kwa kununua vitu mbalimbali.

“Tumefanikiwa kulipa michango mbalimbali yote iliyotakiwa ngazi ya  kitaifa,tumefanikiwa huduma ya kusaidiana sisi kwa sisi ndani ya chama chetu,hata hivyo tumekosa mtaji wa kutosha kuanzisha miradi mbalimbali ndani ya chama,natoa wito kwa akinamama wengi zaidi kujiunga katika chama chetu ili kukiendeleza,pia naomba ushirikiano na mahudhurio mazuri ndani ya chama ’’,alisisitiza.
Mwenyekiti wa WWK katika kanisa la TAG-Galilaya Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma mrs Evodia Midelo akihubiri katika kanisa hilo siku ya WWK-Kitaifa,aliyeketi nyuma yake ni mchungaji  mrsRose Nguya,Mahubiri hayo yaliwagusa wengi ambao walihudhuria maadhimisho hayo 
Changamoto zinazoikabili WWK kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ni pamoja na  kushindwa kuendeleza mradi wa kuuza chakula kutokana na  idadi kubwa ya watu ambao walikopa chakula na kushindwa kulipa,idadi ya wanachama wake imepungua kutoka wanawake 30 mwaka jana hadi kufikia 24 hivi sasa na kwamba chama hicho kinatarajia kuanzisha mradi wa kutengeneza sabuni za kufulia.

Katika maadhimisho ya mwaka huu WWK katika kanisa la Galilaya  limemzawadia mchungaji wake pamoja na familia yake mifuko kumi ya theruji yenye thamani ya shilingi 175,000 pamoja na fedha taslimu shilingi 25 kama sehemu yao ya shukrani kwa mchungaji huyo  kutokana na maombi ambayo amekuwa akiwaombea na kupata Baraka mbalimbali.
  
Wanawake watumishi wa kristo WWK  wa kanisa la TAG-Galilaya wakiwa katika picha ya pamoja na mchungaji wao siku ya sikukuu ya WWK kitaifa iliyofanyika katika kanisa la TAG-Galilaya Ruhuwiko Songea mkoani Ruvuma picha na Albano Midelo.


Kwa upande wake mlezi wa WWK katika kanisa la Galilaya Rose Nguya ambaye pia ni mkurugenzi wa  jimbo la Ruvuma amewapongeza wanawake wa kanisa hilo kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kulihudumia kanisa la Mungu na amewaasa moyo huo wa kujitolea kuuendeleza na kwamba watarajie kupata Baraka nyingi kutokana na huduma zao katika kanisa.
Simu 0766463129



.

No comments:

Post a Comment