Na Albano Midelo,Songea.
ASKOFU mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega ametoa rai vyombo ambavyo vinasimamia sheria kutenda haki kwa watu wote ili ipatikane haki na amani ya kweli alioicha Yesu Kristu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake.
Askofu mkuu Mtega alitoa rai hiyo wakati anahubiri kwa nyakati tofauti katika kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba la mjini hapa pamoja na kanisa la parokia ya Bombambili jimbo kuu la Songea.
Mhashamu Mtega alibainisha kuwa misingi ya sheria isipofuatwa kikamilifu na vyombo vinavyotoa haki kama mahakama vinaweza kuumiza jamii kwa kuwa haki itashindwa kupatikana matokea yake amani inaweza kuvunjika na kusababisha migogoro katika jamii.
“ Amani haiwezi kuwepo endapo haki haiwezi kutendeka ,natoa wito kwa wenye mamlaka na vyombo vya haki viache kupindisha sheria‘pasiwepo na upendeleo kwa sababu ya ukabila,kufahamiana,uwezo wa mtu,rangi ya mtu au kwa namna yeyote ile ,Yesu kristo alihukumiwa adhabu ya kifo bila ya kuwa na hatia yeyote ,Yesu alikuwa hana mtetezi yeyote,hata hivyo alishinda mauti na kutuletea amani ya kweli”,alisisitiza.
Aliongeza kuwa sheria zimewekwa kwa ajili ya kutenda haki bila upendeleo pamoja na kupatikana kwa ulinzi kwa watu wote pamoja na mali zao,hivyo ametaka vyombo vyote vinavyosimamia haki na sheria kutimiza wajibu wao bila upendeleo ili viweze kuaminika katika jamii.
Hata hivyo Askofu mkuu Mtega amewaasa waumini kuwaombea viongozi waliopo madarakani hivi sasa ili waweze kuliongoza Taifa katika misingi ya umoja,amani,utulivu na haki pamoja na kuviombea vyombo vya sheria ili viweze kutenda haki katika jamii inayowazunguka.
Askofu mkuu Mtega amerudia wito wake kwa watanzania kuhusu mchakato wa katiba mpya ambayo inatakiwa kuandikwa nchini ambapo ametahadharisha kuwa katiba iwe ile ambayo Mungu ataonekana ndani yake na itakayowanufaisha watanzania wote .
“ Tumeshuhudia yaliotokea Bungeni Dodoma hivi karibuni,ndugu zangu hivi sasa tunalilia kuandikwa katiba mpya ,lakini tunataka katiba ambayo ndani yake Mungu ataonekana ili tuunde taifa ambalo linatembea na Mungu, tunapofikisha ya jubilei miaka 50 ya uhuru wa Taifa letu hapo Desemba 9,2011 ni vema tuzaliwe upya ”anasema.
Alibainisha zaidi kuwa Taifa linapotimiza Jubilei ya miaka 50 linatakiwa kuzaliwa upya kwa kuandikwa katiba ambayo itatenda haki kwa watanzania wote,vyama vyote vya siasa ,rasilimali za taifa kama vile madini na maliasili zote ziwanufaishe watanzania wote na pasiwepo upendeleo wa aina yeyote.
Baruapepe amidelo@yahoo.com
No comments:
Post a Comment