Monday, May 16, 2011

Askofu awachongea watendaji serikalini kwa kunyanyasa wachungaji

 Askofu wa kanisa TAG jimbo la Ruvuma mchungaji Johakimu Mhagama
 Na Albano Midelo,Songea.
KANISA la Tanzania Assembles Of God TAG jimbo la Ruvuma limetoa lawama nzito kutokana na unyanyasaji mkubwa ambao unafanywa na viongozi wa serikali ngazi ya vijiji,mitaa na kata dhidi ya wachungaji wa kanisa hilo .

Askofu wa TAG jimbo la Ruvuma mchungaji Joakimu Mhagama alimweleza mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma kuwa viongozi hao wa  serikali  wamekuwa  na tabia ya kuwakamata wachungaji na kuwatoza fedha ya mgambo isiyokuwa na risiti kwa madai kuwa hawakwenda kujitolea siku ya Jumapili.

Baadhi ya wachungaji wa kanisa la TAG jimbo la Ruvuma


“Mhemishimiwa mkuu wa mkoa  naomba nikupe baadhi ya mifano ambayo imetokea,mchungaji wetu Longinus Haule wa kijiji cha Mdunduwalo kata ya Maposeni wilayani Songea aliwekwa ndani na kutozwa fedha  ya mgambo kwa kuwa eti hakwenda kujitolea  siku ya Jumapili,tunaomba ufafanuzi juu ya viongozi wa dini kuhusu kazi za kujitolea”,alisema.

Hata hivyo Askofu Mhagama alibainisha zaidi kuwa mazoea ya viongozi wa  serikali za vijiji,kata,mitaa na wilaya kuitisha mikutano siku za Jumapili kitu ambacho alisema kimekuwa kinasababisha makanisa kuvunja ibada na waamini kushindwa kutumia uhuru wao wa kuabudu ambao ni haki yao ya msingi kikatiba.

Aliongeza kuwa iwapo wachungaji wanaamua kuwazuia waumini wasiende kwenye mikutano hiyo au shughuli za kujitolea viongozi hao wa serikali huwatoza faini kwa madai kuwa wanaonekana kuwa ni wapinzani wa serikali hivyo kusababisha migogoro katika maeneo husika.

Changamoto nyingine ambazo zinalikabili kanisa la TAG jimbo la Ruvuma ni  matukio ya kiuharifu ambayo yamekuwa yanatokea kwenye majengo ya kuabudia ambapo waumini wamekuwa  wanashambuliwa na watu wenye chuki za kidini.

“Kanisa letu la Kihagara lililopo wilayani Nyasa hivi karibuni lilichomwa moto kwa ajili ya chuki za kidini,huko katika kijiji cha Lukalasi wilayani Mbinga motto mmoja aliuwawa kwa kupigwa jiwe kanisani wakati wa mkesha pia huko Kindimba Juu wilayani Mbinga mchungaji wetu Agutino Mtewele alipigwa rungu kwa sababu ya kutaka kunyang’anywa kiwanja cha kanisa”,alisema.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma akiwa ofisini kwake mjini Songea



Akitoa kauli ya serikali baada ya kusikiliza lawama hizo dhidi ya viongozi wa serikali ngazi za vijiji afisa ushirika wa mkoa wa Ruvuma Watson Nganiwa ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma alisema serikali imepokea kero hizo na itazifanyia kazi ili haki itendeke.

Hata hivyo ametoa mwito kwa wananchi wanapoona kuna kiongozi wa umma anafanya unyanyasaji  wa aina yeyote kuripoti haraka polisi au ofisi ya mkuu wa mkoa ambayo ipo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wote bila kujali wadhifa au cheo cha mtu na kuhakikisha kuwa haki inatendeka.

Kwa upande wake Askofu mkuu wa TAG nchini Dk.Barnabas Mtokambali akitoa maoni yake kuhusu vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji kwa wachungaji na waumini wa kanisa hilo jimboni Ruvuma,ametoa rai kwa serikali ya mkoa wa Ruvuma kutumia mamlaka yake kuwadhibiti viongozi hao miungu watu.

“TAG inafanyakazi bega kwa bega  na serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo,viongozi wa serikali katika ngazi zote wanatakiwa kutenda haki kwa wananchi wote,wananchi wakinyimwa haki ni sawa na kukosa pumzi,serikali ya mkoa na Taifa itumie mamlaka yake kuwadhibiti viongozi wanaowanyanyasa wananchi”,alisisitiza Dk.Mtokambali.
Simu 0766463129,baruapepe amidelo@yahoo.com


           


No comments:

Post a Comment