Na
DUNIA imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia,ni wale tu ambao wana elimu ndio watakaoweza kufaidi matunda ya sayansi na teknolojia na wale ambao hawana elimu watabakia kuwa watazamaji tu hivyo basi kundi kubwa ambalo halijui kusoma,kuandika na kuhesabu lililopo hapa nchini lina kila sababu ya kujikomboa kutoka katika hali hiyo ili hatimaye waweze kufaidi matunda ya kuwa na elimu katika ulimwengu huu wa utandawazi.
Hivi sasa kuna mabadiliko au mapinduzi makubwa katika elimu ya sekondari,hasa kutokana na jitihada za serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa kila kata katika nchi nzima inakuwa na shule yake ya sekondari hali iliyowezesha vijana wengi kupata fursa ya kujiunga na elimu ya sekondari,ingawa tatizo la wajinga linaendelea kuongezeka.
Ili kufikia malengo ya milenia ya kupunguza umaskini, kukuza uchumi na kufikia dira ya taifa ya 2025 wadau wa elimu wanashauri hakuna budi kupanua utoaji wa elimu ya sekondari ikiwezekana kwa uwiano sawa yaani mfumo rasmi na ule usio rasmi,hali ambayo wanasema italeta ufanisi na tija katika sekta zote za maendeleo na uchumi.
Taasisi ya elimu ya watu wazima Tanzania(TEWW) ni moja ya mkombozi wa watu wa makundi mbalimbali wenye umri tofauti ambao wamekosa nafasi ya mfumo wa elimu rasmi hivyo wanalazimika kujiendeleza ili wafikie elimu ya sekondari.
Lazima ikumbukwe kuwa sio rahisi watu waliopo makazini ,katika biashara,mitaani,magerezani au katika shughuli zozote za kujiajiri kwenda kujiendeleza katika mfumo rasmi badala yake mfumo usio rasmi umeonekana kuwa ndiyo njia pekee mbadala ya watu wa jinsi hiyo
Mkufunzi mkazi wa Taasisi ya elimu ya watu wazima mkoani Ruvuma Bonifas Chipeta anasema TEWW inatoa elimu kupitia mfumo usio kuwa rasmi iliyoanzishwa mwaka 1960 kama sehemu ya kitengo cha mafunzo ya ziada ya chuo kikuu cha Makerere cha nchini Uganda .
Anabainisha kuwa TEWW ilipewa hadhi ya kuwa Taasisi ya idara ya elimu ya watu wazima chini ya chuo kikuu cha Dar es salaam mwaka 1975 na kwamba TEWW ilipata hadhi na kuwa Taasisi chini ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kwa sheria ya Bunge namba 12 ya mwaka 1975 na kupewa majukumu mengi ambayo yalilenga kuikwamua jamii.
Walengwa ni wanafunzi waliomaliza darasa la saba na waliofanya vibaya mitihani ya kidato cha nne na kutaka kurudia,wanafunzi wanaohitaji kujiendeleza na masomo ya kidato cha tano na sita,wanafunzi waliomaliza na kufaulu masomo ya elimu ya msingi kwa walioikosa(MEMKWA) na watu wazima waliopo maofisini au katika shughuli za kujiajiri.
Chipeta anabainisha kuwa katika mkoa wa Ruvuma vipo vituo vya elimu ya watu wazima katika wilaya tatu ambapo wilayani Mbinga kuna vituo vinne,katika wilaya ya Songea kuna vituo vitatu, Tunduru kuna kituo kimoja mjini Songea kuna vituo viwili ambapo wilaya ya Namtumbo haina kituo hata kimoja hadi sasa na kwamba vituo hivyo vina wanafunzi zaidi ya 600.
Hata hivyo mkufunzi mkazi huyo wa elimu ya watu wazima katika mkoa wa Ruvuma anaelezea masikitiko yake kuhusiana na vituo vya mitaani vinavyotoa elimu nje ya mfumo rasmi bila kufuata utaratibu wa serikali na ametoa wito kwa wamiliki wa vituo hivyo kujisajiri chini ya chombo kinachosimamia shughuli hizo ambacho ni Taasisi ya elimu ya watu wazima Tanzania.
Amezitaja faida za kujiendeleza kupitia vituo vya Taasisi ya elimu ya watu wazima ambavyo vinatambulika na serikali kuwa ni pamoja na wanafunzi kufundishwa kwa kutumia miongozo(syllabus) maalum na moduli za masomo yote zinapatikana,wanafunzi hufundishwa na walimu wenye sifa.
Pamoja na mafanikio hayo Taasisi ya elimu ya watu wazima katika mkoa wa Ruvuma inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kukithiri kwa vituo vya mitaani vinavyoendesha masomo ya sekondari na vyuo bila utaratibu .
Albano Midelo ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu huria cha Tanzania katika shahada ya uandishi wa habari, anapatikana kwa simu 0766463129,barua pepe amidelo@yahoo.com
Asante sana kwa taarifa hii. Mimi mwalimu na mdau wa elimu nimevutiwa na yote uliyoandika. Kuhusu elimu katika dunia hii ya utandawazi wa leo ni jambo ambalo nami nimekuwa nikisema tena na tena kwenye maandishi mbali mbali. Nimejifunza kutokana na taarifa ya Bwana Chipeta. Kila la heri.
ReplyDelete