Monday, June 13, 2011

Askofu mstaafu wa Bukoba avunja rekodi ya maaskofuTanzania


Askofu mstaafu wa jimbo la Bukoba mhashamu Gervas Nkalanga siku ya jubilei yake ya miaka 50 ya uaskofu katika abasia ya Hanga wilayani Namtumbo.Askofu huyo amevunja rekodi ya kuwa askofu wa kwanza nchini kufanya jubilei ya miaka 50 akiwa hai.Picha na Albano Midelo

Na Albano Midelo,Natumbo
ASKOFU mstaafu wa jimbo la Bukoba Mhashamu Gervas Nkalanga amevunja rekodi kwa maaskofu wa kanisa katoliki nchini baada ya kuwa Askofu pekee kuadhimisha jubilee ya miaka 50 ya uaskofu akiwa hai.

Askofu Nkalanga ameadhimisha jubilee ya miaka 50 katika Abasia ya Hanga jimbo kuu katoliki ya Songea Juni 7 mwaka huu ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa.

Rais wa Baraza la maaskofu katoliki Tanzania TEC mhashamu Yuda Thadei Ruwaichi akitoa salamu za Baraza hilo kwenye jubilee hiyo iliyohudhuriwa na maaskofu  karibu wote wa kanisa katoliki nchini alisema askofu mstaafu Nkalanga mwenye umri wa miaka 92 anakuwa ni askofu wa kwanza nchini kufanya jubilee ya miaka 50 akiwa hai.

Rais huyo alibainisha kuwa TEC inatambua mchango mkubwa ambao ulifanywa na Askofu mstaafu Nkaranga katika kipindi chake chote cha uaskofu akiwa madarakani na baada ya kustaafu  na kutoa rai kwa maaskofu wengine kuiga mema yote ya askofu huyo.
Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea akimpokea Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkpa akiwa na mkewe Anna Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi siku ya maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya askofu mstaafu wa jimbo la Bukoba Gervas Nkalanga katika abasi ya Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma


Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa akizungumza kwenye maadhimisho hayo alimpongeza Askofu mstaafu Gervas Nkaranga kwa kufanya jubilee ya miaka 50 akiwa hai na kusisitiza kuwa ni jambo jema mtu kupongezwa akiwa hai kwa kuwa imezoelea watu wengi wanasifiwa baada ya kufa.

Rais mstaafu Mkapa ambaye anajiita kuwa ni mseminari mshindwa kutokana na ukweli kuwa alisoma katika seminari ya Kigonsera wilayani Mbinga,alikiri kuwa nafasi zote ambazo amepewa hapa nchini zimetokana na malezi mazuri  ya kiroho na kimwili ambayo alipewa na shirika la watawa wabenedikitini  akiwa Kigonsera na Ndanda chini ya kanisa katoliki jimbo kuu la Songea.

“Shirika la wabenedikitini siku zote wanazingatia kauli mbiu yao ya sala na kazi,bila kazi hakuna maisha wala heshima, vijana wetu siku hizi hawataki kufanyakazi wanataka kufanyiwa kazi na sisi wazee tusisahau sala na kazi”,alisisitiza Rais mstaafu Mkapa.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa akiwa na mkewe Anna Mkapa katika picha ya pamoja na maaskofu wapatao 38 wa kanisa katoliki siku ya jubilei ya askofu mstaafu w Gervas Nkalanga abasia ya Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma



Hata hivyo Rais mstaafu mkapa alisema watu wengi wanapenda kuonekana kwa jamii pale wanapofanya mambo mbalimbali  ambapo alibainisha kuwa Askofu mstaafu Nkalanga  kuacha jimbo lake la Bukoba na   kuamua kuishi katika Abasia ya Hanga jimbo kuu la Songea ni jambo la kupongezwa.

“Mimi binafsi hivi sasa sipendi kuoneka onekana ndiyo maana hata mliponialika kuja kuwa mgeni rasmi katika jubilee hii nilitafakari sana na nilisita,kwa kweli nimeguswa sana na ucha Mungu na uongozi wa Askofu mstaafu Nkalanga naomba mwenyezi Mungu amzidishie maisha marefu Askofu mstaafu Nkalanga”,alisisitiza Mkapa.





No comments:

Post a Comment