Sunday, June 5, 2011

Mfahamu mzee aliyeuwa mamba wala watu 640 ziwa Nyasa

Baadhi ya wakazi wa mji wa Songea mkoani Ruvuma wakimiminika kwenye uwanja wa michezo wa Majimaji kuangalia banda la wizara ya maliasili na utalii ambalo lilikuwa limewekwa mnyama aina ya mamba ili kumtazama mnyama huyo aliyewavutia wengi waliomuona.
 Na Albano Midelo.

 MAMBA ni mnyama ambaye anatisha kutokana na kuwa na tabia ya kula binadamu pale anapofanya mawindo yake majini ambako ndiyo makazi makuu ya mnyama huyu.

Nimewahi kuishi mwambao mwa ziwa Nyasa kwa takribani miaka minne wakati nasoma katika shule moja ya Sekondari inayoitwa  shule ya mtakatifu Paulo iliyopo katika mji mdogo wa Liuli ziwa Nyasa.Nikiwa nasoma katika shule hiyo nimewahi kushuhudia matukio kadhaa ya mamba kukamata watu ndani ya ziwa Nyasa hali ambayo ilinifanya kumuogapa sana mnyama huyu.

Mtoto wa mamba ambaye aliwekwa kwa siku saba kwenye maonyesho ya wiki ya mazingira duniani ambazo kitaifa zilifanyika mkoani Ruvuma kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea ,sherehe hizo zilifunguliwa na makamu wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal na kuhitimishwa na waziri mkuu Mizengo Pinda ambaye aliwakilishwa na waziri wa ardhi,nyumba na makazi profesa Anna Tibaijuka.


Kwa kweli kwa miaka minne ambayo niliishi Nyasa sijawahi kuoga katika ziwa Nyasa kuhofia kukamatwa na mamba.Mamba katika ziwa Nyasa walidiriki kuwakamata raia wa kigeni yaani wazungu ambao walikuwa wanafanya uvuvi wa samaki wa mapambo katika ziwa hilo,licha ya uvumi ambao ulikuwa umeenea awali kwamba mamba hawezi kukamata mzungu.

Kutokana na mamba wala watu katika eneo la Liuli  kuwa kero  ,walijitokeza wanaharakati ambao waliamua kutafuta mbinu za kukabiliana na mamba hao ambao walianza kurudisha nyuma shughuli za kiuchumi ndani ya ziwa Nyasa  pamoja na wawekezaji kuanza kuogopa.

Miongoni mwa  wazee ambao walijitokeza kupambana na mamba ni mzee mstaafu wa jeshi la wanaunchi wa Tanzania JWTZ ambaye kutokana na uhodari wake katika vita dhidi ya mamba wananchi wa mwambao mwa ziwa Nyasa waliamua kumpa jina la Mrema ambaye alifanikiwa kuangamiza mamba wapatao 640 baada ya kuwatega kwa kutumia ndoani maalum.

Mwandishi wa makala haya Albano Midelo akizungumza na mzee maarufu kwa jina la Mrema  katika kijiji cha Liuli ziw Nyasa mwenye shati jeupe muda mfupi kabla ya kufariki ghafla mzee huyo mwaka huu ambaye ameweza kuuwa mamba wala watu 640 ndani ya ziwa Nyasa 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mzee Mrema ambaye hivi sasa ni marehemu ,alisema alifanikiwa katika vita hivyo kwa kumuomba mwen yezi Mungu kabla ya kuanza kuwatega mamba hao,ambao ilidaiwa walikuwa ni mamba wa watu ambao walikuwa wanatumika katika mambo ya kishirikina na kwamba alifanikiwa kuwamaliza kwa kuwatega kwa ndoana maalum iliyowekwa nyama ya mbwa.

“Nyama ya mbwa ni chakula ambacho mamba anakipenda sana,mkiwa wawili binadamu na mamba majini,mamba anaanza kumkata kwanza mbwa,hivyo mimi nilifanikiwa kuwanasa mamba wengi kwa kutumia nyama ya mbwa na kufanya idadi ambao niliwauwa walifikia 640 na tatizo la mamba wala watu ziwa Nyasa likabakia kuwa ni historia,ingawa hivi nimeanza kusikia wameanza kuonekana lakini hawajawahi kukamata tena mtu”,alidai mzee Mrema.
 Baadhi ya wazi wa mji wa Songea wakiangalia banda ambalo aliwekwa mamba ,fuvu ambalo unaliona juu ya meza ni la mnyama aina ya tembo ambalo nalo lilivutia wengi waliotembelea katika banda hilo la maliasili.


Katika sherehe za siku ya mazingira duniani ambazo kitaifa zimefanyika mkoani Ruvuma wizara ya maliasili na utalii katika mabanda yao ya maonyesho kulikuwa na vivutio vingi vya wanyama,lakini kubwa ambalo wakazi wa mji wa Songea walivutika ni  kwenda kumuangalia mamba  katika banda la mamba  ambaye aliwavutia wengi ingawa pia kulikuwa na wanyama wengine kama nyungunyungu,nyani,ngozi za wanyama mbalimbali  na mafuvu ya wanyama kama vile tembo.

Metson Mwakanyamale ni mkuu wa kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kusini ambaye alizitaja faida za mamba kuwa ni pamoja na utalii,chakula na mazao yake kama vile mayai na ngozi   vina thamani kubwa kutokana kutumika kutengenezea mikanda,mabegi na viatu.
Mkuu wa kikosi dhidi ya ujangili kanda ya kusini ambaye pia ni msimamizi wa hifadhi ya wanyamapori ya asili ya Luhira ya mjini Songea akitoa elimu ya wanyamapori kwenye banda la maliasili

“Nyama ya mamba ni chakula ambacho kinapendwa na watu wengi ,baadhi ya makabila hapa nchini yanapenda kula nyama ya  mamba,hata hivyo katika ulimwengu nchi ambayo inaongoza kwa ulaji wa nyama ya mamba ni Ujerumani,wageni ambao wanatoka katika nchi ambazo hazina mamba wananunua  mayai na kwenda kutotoresha ili kupata mamba na kukuza utalii katika nchi zao”,anasisitiza Mwakanyamale.

Pamoja na  faida ambazo zinatokana na mamba ,Mwakanyamale anayataja madhara ya mamba kuwa ni pamoja na  mamba kuwa ni miongoni mwa wanyama hatari kwa binadamu na mifugo iwapo atapatikana mahali ambako sio hifadhi ya Taifa au majini.

Kutokana na hali hiyo Mwakanyamale anasema serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii inafanya doria  katika maeneo yaliotengwa na hasa majini ili kuhakikisha kuwa  mamba hawaleti madhara ambapo ametahadharisha kuwa hairuhusiwi kuwauwa au kuwamiliki  mazao ya wanyamapori kama vile ngozi na pembe bila kibali  toka serikalini.

Baruapepe amidelo@yahoo.com





No comments:

Post a Comment