Monday, June 13, 2011

Mwanamke abubujika machozi akimlilia Rais mstaafu Mkapa kanisani


 Baadhi ya wakazi wa mji wa Songea  wakiwemo waumini wa kanisa katoliki jimbo kuu la Songea  wakiwa wamejitokeza kwa wingi kumlaki Askofu mkuu Norbert Mtega siku ya  Jubilei miaka 25 ya askofu huyo  katika kanisa kuu la kiaskofu mjini Songea.

 Picha hapa chini inamuonesha Askofu mkuu Mtega akilakiwa na maelfu ya waumini wa kanisa katoliki jimbo kuu la Songea siku  ya jubilei ya miaka 25 ya askofu mkuu Mtega. 
Na Albano Midelo,Songea

MKAZI mmoja wa mjini Songea mkoani Teresia Komba(50) alilibubujika machozi  huku akimuomba  Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kuacha kukaa kimya badala yake asaidie kutoa ushauri wa kukabiliana na maisha magumu yanayowakabili watanzania hivi sasa.

Mwanamke huyo alikuwa amejipanga katika lango la kuingilia kanisa kuu katoliki la Songea ambapo baada ya kumuona Rais Mkapa anatoka kanisa kuu katoliki la Songea  ambako alikuwa mgeni rasmi katika Jubilei ya  miaka 25 ya Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega alipaza sauti huku akibubujika na machozi  na kumuomba Rais mstaafu kuliokoa taifa.
“Baba Benjamin Mkapa tafadhali rudi,mbona hauonekani,watanzania tunakufa,maisha magumu kila kitu bei juu,rudi baba,tunaangamia sisi watoto wako ,hatujui maisha haya mwisho wake utakuwa nini”,alipiga kelele mwanamke huyo huku akilia na kububujika machozi ambayo yalisababisha pia watu wengine waliokuwepo jirani naye kuanza kutoka machozi.

Hata hivyo kilio hicho ambacho mwandishi wa habari hizi alikuwa jirani na kukishuhudia hakikuweza kumfikia Rais mstaafu Mkapa kwa kuwa wakati anapita katika lango hilo kutokea kanisani gari lake lilikuwa limefungwa vioo na msafara wa magari kutoka kanisani uliendelea kuelekea ukumbini baada ya misa kanisani.
 Baadhi ya maaskofu wa kanisa katoliki nchini wakimsubiri askofu mkuu katika maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya askofu Mtega ambapo jumla ya maaskofu 38 kutoka nchi nzima walishiriki.
Rais mstaafu Benjamin Mkapa akizungumza katika jubilei ya miaka 50 ya Askofu mstaafu wa jimbo la Bukoba Gervas Nkalanga katika Abasia ya Hanga jimbo kuu la Songea  alitamka wazi kuwa tangu alipomaliza kipindi chake cha miaka 10 ya urais hapendi kuoneka onekana na kwamba alipoalikwa na kanisa katoliki kuwa mgeni rasmi katika jubilee za maaskofu alitafakari na kusita hata hivyo alikubali baada ya kuguswa na ucha Mungu wa maaskofu hao katika jimbo kuu la Songea.
             

Awali akitoa salamu zake katika maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 ya uaskofu ,miaka 38 ya upadre na miaka 66 ya kuzaliwa kwa Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea,Rais mstaafu Mkapa   amempongeza Askofu mkuu Mtega kwa kazi nzuri ambayo ameifanya katika jimbo kuu la Songea katika harakati mbalimbali za maendeleo hasa katika nyanja za elimu,afya,teknolojia ya habari na mawiliano,ufundi pamoja na kilimo.
 Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa akiwa pamoja na mkewe Anna Mkapa kwenye kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini Songea akifuatilia kwa makini misa ya jubilei ya miaka 25 ya askofu mkuu Norbert Mtega
Rais mstaafu Mkapa huku muda wote akishangiliwa na waumini waliofurika katika kanisa kuu la kiaskofu la Songea, alimwelezea Askofu mkuu Mtega mbele ya maaskofu 38 wa kanisa hilo nchini kuwa  katika kipindi chake cha miaka 25 amejitolea kuishi maisha ya utakatifu  katika utendaji wake wa kutukuka na kwamba Askofu Mtega ni muhubiri mahiri na kwamba sifa yake kubwa  ni kuwa mwanaharakati wa kueneza  haki elimu kwa waumini na watanzania wote.

“Askofu mkuu Mtega ni muhubiri mahiri mimi binafsi nimehudhuria katika misa zake hapa Songea na Dar es salaam,sifa yake kubwa ambayo hata mimi naithamini sana ni kwamba yeye ni mwanaharakati wa haki elimu kwa waumini wake  na watanzania wote  amefanikisha kufunguliwa kwa chuo kikuu cha Ruaha Iringa,amefanya ushawishi wa kuanzishwa kwa  vyuo vikuu vya TEKNOHAMA na sasa nasikia anasimamia uanzishwaji wa chuo kikuu cha kilimo Songea,hongera sana baba askofu”,alisema.

Hata hivyo Rais mstaafu Mkapa amempongeza Askofu mkuu Mtega kwa dhana yake ambayo ameijenga kwa waumini wake kujitegemeza na kujiletea  maendeleo wao wenyewe badala ya kuendelea na dhana potofu ya kuwategemea wahisani na wafadhili ambayo imejengeka katika maeneo mengi nchini.

“Mimi huwa nafadhaishwa sana siku hizi ninaposikia  baadhi ya viongozi wakisema watawaletea wananchi maendeleo,dhana ya serikali kuwaletea wananchi maendeleo ni potofu na inaviisha juhudi zetu wenyewe za kujiendeleza,nawaomba  viongozi wenye mtazamo huu waje kuzungumza na Askofu mkuu Mtega waje jimbo la Songea na Mbinga waone matokeo ya watu walioamua kujiendeleza”,alisisitiza Rais mstaafu Mkapa.

Rais mstaafu Mkapa amemsisitizia Askofu mkuu Mtega kuendelea kuwaelimisha waumini wake na watanzania kwa ujumla kutambua kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na watanzania wenyewe na kwamba wahisani wanaweza kusaidia harakati za maendeleo lakini jukumu  ni la wananchi wenyewe.
Picha inamuonesha Kadinali Pengo akiwa na Askofu mkuu Mtega wakimsindikiza Rais mstaafu kutoka ndani ya kanisa la kiaskofu la Songea kwenda kwenye gari yake mara baada ya kumalizika misa ya jubilei.
Kwa upande wake kiongozi wa kanisa katoliki nchini na Askofu mkuu wa jimbo kuu la Dar es salaam Mhadhama Porcapy Kadinari Pengo akihubiri katika jubilei hiyo  amempongeza Askofu mkuu Mtega katika juhudi zake za kuhubiri injili pamoja na kupigania maendeleo  katika nyanja mbalimbali .

“Wamisionari wabenediktine katika jimbo kuu la Songea wamefanya kazi kubwa ya uinjilishaji,hata hivyo Askofu mkuu Mtega ameendelea kuwatafuta wamisionari wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo wa nchini India kwa lengo la kutosheleza shughuli za injili na huduma nyingine za kijamii”,alisema.

Askofu mkuu Mtega  kwa upande wake amekiri maendeleo yote ambayo yamepatikana katika kipindi chake cha miaka 25 ya uaskofu  jimbo kuu la Songea, yametokana na ushirikiano mkubwa ambayo ameupata kutoka serikalini pamoja na waumini wote kwa ujumla.

Hata hivyo alisisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa huru  hadi hapo  itakapojengwa misingi imara ya kujitegemea wenyewe kiuchumi na kijamii na kwamba msingi mkuu wa uchumi wa Tanzania unapaswa kuwa katika uzalishaji mali kutokana na nchi kuwa na rasilimali zote muhimu kwa maendeleo endelevu.


 


No comments:

Post a Comment