Mkurugenzi wa chuo kikuu huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma Gubwe Kalalambe akizungumza siku ya kuwapongeza wahitimu 31 wa mwaka 210 wa kituo hicho kwenye ukumbi wa OUT mjini Songea,waliokaa kutoka kulia ni mwenyekiti wa serikali ya wanachuo Christopher Haule,mtaaluma wa OUT kituo cha Ruvuma Andrew Komba na katibu wa serikali ya wanachuo Sekela Mwamwezi.
Na Albano Midelo,Songea.
MKURUGENZI wa chuo kikuu huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma Gubwe Kalalambe ameelezea masikito yake kuhusu mwamko mdogo wa jamii ya mkoa wa Ruvuma kujiunga na masomo ya chuo kikuu huria.
Kalalambe alitoa kauli hiyo wakati anazungumza kwenye hafla ya kuwapongeza wahitimu 31 wa mwaka 2010 kati yao shahada ya kwanza ni 12 na wahitimu wa kozi ya mafunzo ya awali 19 kwenye ukumbi wa chuo kikuu huria kituo cha Ruvuma .
Kutokana na changamoto hiyo mkurugenzi huyo alitoa wito kwa waajiri kuwahamasisha watumishi wao ili waweze kujiendeleza kupitia chuo kikuu hicho.Pia aliwaasa viongozi wa vyama vya siasa na dini wasaidie kuhamasisha katika mikutano pamoja na mikusanyiko mbalimbali ya wananchi .
Changamoto nyingine ambazo zinakikabili chuo kikuu hicho ni pamoja na ubovu wa barabara inayokwenda chuoni hapo kupitia Bohari kuu ya serikali,mikopo michache inayotolewa kwa baadhi ya wanachuo haikidhi mahitaji hali inayosababisha wanachuo kushindwa kulipia ada,gharama za vitabu na utafiti.
Akisoma risala ya wanachuo kwa niaba ya wenzake,Luya Ngonyani alisema kituo cha Ruvuma kilizinduliwa rasmi Desemba 1996 kikiwa na wananchuo 53 wakiwemo wanaume 48 na wanawake watano ambapo hivi sasa kituo hicho kina wanachuo waliodahiliwa 1279 kati yao wanaume 972 na wanawake 307.
Kwa mujibu wa risala hiyo chuo kikuu huria cha Tanzania kinatoa mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kozi ya maandalizi(Foundation course) shahada ya kwanza ,shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu.
Mhadhiri anayeshughulikia taaluma katika chuo kikuu huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma Andrew Komba amesema wahitimu hao 31 wanafanya jumla ya wahitimu katika chuo kikuu hicho kufikia 137 tangu kuanzishwa na kuanza kutoa wahitmu mwaka 1999.
Hata hivyo ametoa mwito kwa wananchi mkoani Ruvuma kujitokeza kupata elimu ya juu katika chuo kikuu huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma hasa kutokana na kuwa ndiyo chuo kikuu pekee nchini ambacho kinatoza ada nafuu zaidi.
Chuo kikuu huria cha Tanzania kilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1992 ,chuo katika nchi nzima kilianza kudahili wanachuo ambapo jumla ya wanachuo 766 walidahiliwa mwaka 1994 wakiwemo wanachuo 15 kutoka mkoa wa Ruvuma .
amidelo@yahoo.com
No comments:
Post a Comment