Tuesday, February 14, 2012

55 watunukiwa shahada OUT Ruvuma

 
 
Na Albano Midelo

MKURUGENZI wa habari jimbo kuu katoliki la Songea padre Noe Duwe ni miongoni mwa wahitimu 55 waliotunukiwa shahada baada ya kuhitimu chuo Kikuu Huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma.
Wahitimu hao katika shahada mbalimbali wanafanya chuo Kikuu Huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma kufikisha jumla ya  wahitimu 161 tangu mwaka 1999 hadi 2010.

 Risala ya wanachuo iliyosomwa mbele ya mgeni rasmi mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabiti Mwambungu kwenye hafla ya kuwapongeza wahitimu hao kwenye ukumbi wa chuo kikuu hicho mjini hapa iliipongeza serikali kwa kuanzisha  chuo kikuu kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1992 ambayo umetoa fursa kwa watanzania wengi kupata elimu ya juu.
Risala hiyo imebainisha kuwa wafanyakazi wengi waliohitimu katika chuo kikuu huria cha Tanzania ,wamefanikiwa kupanda vyeo katika nyadhifa zao na kwamba wanaishukuru serikali kwa kutoa mikopo kwa baadhi ya wanachuo kwa ajili ya gharama za vitabu na utafiti.
Hata hivyo risala hiyo imezitaja changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho kuwa ni pamoja na mazingira duni ya kusomea,kukosekana kwa wahadhiri katika fani mbalimbali,majengo chakavu yanayohitaji ukarabati,ukosefu wa vitendeakazi ikiwemo mtandao wa uhakika wa intaneti na mwamko mdogo wa wanawake kujiunga na chuo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kituo cha Ruvuma Andrew Komba  alisema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1992,kasi ya kukua imeongezeka ambapo  hivi sasa mikoa yote ina matawi ya chuo hicho na kwamba chuo kina programmu 50 za masomo kwa ajili ya cheti,shahada,shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu.
“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimekuwa msaada mkubwa kwa wanyonge,wasiokuwa na nguvu za kiuchumi, waliopembezoni na kutengwa na mifumo mbalimbali,leo hii sio ajabu hata mfungwa anaweza kusoma’’,alisisitiza.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo mkuu wa mkoa wa Ruvuma aliyewakilishwa na afisa elimu wa mkoa  Paulina Mkonongo aliwapongeza  wahitimu hao kwa uvumilivu ambao umewawezesha kuhitimu shahada mbalimbali.
Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania kituo cha Ruvuma kilianza na wanachuo 15 mwaka 1994 ambapo hadi kufikia hadi hivi sasa kituo kina wanachuo 219 kati yao wanaume ni 153 na wanawake 66
albano.midelo@gmail.com

No comments:

Post a Comment