Na Albano Midelo
WAHENGA walisema akili ni nywele kila mmoja ana zake. Baada ya kujitokeza uhaba wa vyumba vya madarasa, kijiji cha Mkili kilichopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kiliamua kuomba fedha katika mfuko wa TASAF ili wakamilishe mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule.
TASAF wilaya ya Mbinga walitoa kiasi cha Sh. 35 milioni ambazo zilitumika kujenga vyumba viwili vya madarasa, ofisi moja ya walimu na vyoo. Jumuiya ya shule ya Mkili ilifurahi mradi huo wa mwaka mmoja kufikia hatua nzuri.
Bahati mbaya, jumuiya ya Mkili haikuwa kwenye kichwa cha ofisa mtendaji wa kijiji cha Mkili, Bosco Mapunda. Wakati shule wanafikiri kutumia miundombinu hiyo, Mapunda alikuwa anafikiria namna ya kuwadhibiti na kuwatia adabu wakorofi katika kijiji hicho, hivyo akaamua jengo jipya la shule hiyo lenye ofisi moja ya walimu litumike rasmi kama mahabusu.
Licha ya shule ya msingi Mkili kukabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu ofisa mtendaji anatumia ofisi ya walimu kama mahabusu ya kijiji. Mapunda hivi sasa ni kaimu mtendaji wa kata ya Liwundi iliyoko tarafa ya Ruhuhu katika mwambao wa Ziwa Nyasa.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkili, John Ntanga anasema ameshangazwa na hatua ya kijiji kutumia jengo hilo kama mahabusu ya kijiji hali wakitambua kuwa shule hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu.Ntanga anabainisha kuwa mpaka sasa, ni mwaka wa tatu mradi huo ambao pamoja na nguvu za wananchi umegharimu zaidi ya Sh. 42 milioni haujakabidhiwa badala yake baadhi ya majengo yamebadilishwa matumizi na kuwa mahabusu ya kijiji.
Utawala ni wa chuma. Mathias Nkomola ambaye ni mjumbe wa kamati ya ujenzi wa jengo hilo, ametishiwa kuwekwa kwenye mahabusu hayo kutokana na kitendo chake cha kuhoji ulikofikia mradi huo ambao ndani yake kunanukia ufisadi.
“Sisi wajumbe wa kamati ya ujenzi tumekuwa tukidai watusomee mapato na matumizi ya ujenzi wa jengo hilo ambalo limetumia mifuko ya saruji 450 kwa ajili ya matofali. Nguvu za wananchi zimetumika huku kokoto na mchanga wamebeba wanafunzi wa shule ya msingi Mkili.
Viongozi wanakataa kutoa taarifa ya ujenzi,’’ anafafanua Nkomola.
Viongozi watatu (majina yao yamehifadhiwa) wanatajwa kuwa wamejinufaisha kupitia mradi huo kwa kuwa walihusika moja kwa moja katika ukandarasi wa jengo na utengenezaji wa samani za shule ambao haujakamilika hadi sasa .
Hata hivyo, mtuhumiwa mkuu katika ufisadi huo ametorokea jijini Dar es Salaam baada ya wananchi kutaka kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. Watuhumiwa wengine wawili, bado wapo na wameomba kuongezewa muda ili wakamilishe ujenzi na utengenezaji wa samani za shule.
Wananchi wanaofutilia ufisadi uliofanyika kwenye jengo hilo wameamua kukaa kimya vinginevyo watawekwa mahabusu ya shule kwa madai kuwa ni wapinga maendeleo ya kijiji hicho. Hadi sasa tayari wananchi wanakamatwa na kuwekwa kwenye mahabusu ambayo ni ofisi ya walimu.
“Mwandishi hebu fikiria wazazi wanawekwa kwenye mahabusu ya jengo la TASAF ambalo wazazi haohao wametumia nguvu zao kujitolea kwenye ujenzi kwa ajili ya watoto wao. Watoto watawezaje kusoma kwa uzingativu katika shule hiyo hiyo ambayo wanashuhudia wazazi wao wakikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kudai haki? Huu ni uungwana kweli?’’ anahoji Grace Hyera mkazi wa Mkili.
Uchunguzi unaonyesha kwamba kamati ya ujenzi wa jengo hilo inaogopa kukabidhi jengo hilo kutokana na ujenzi wake kuwa chini ya viwango hali ambayo imesababisha sehemu muhimu kama sakafu kuanza kupasuka na kuvunjika kabla hata ya mradi kukabidhiwa katika shule hiyo.
Ntanga anasema kazi ya ujenzi wa jengo hilo la TASAF ulianza mwaka 2009 na ulitakiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja, lakini mara baada ya kuvunjwa kwa serikali ya kijiji mambo yalianza kuharibika baada ya kamati ya ujenzi kuwa huru na kuendesha shughuli za ujenzi kwa matakwa yao.
Kamati hiyo haikuhusisha uongozi wa shule ya msingi licha ya kwamba madarasa hayo mawili, ofisi ya walimu na vyoo ni kwa ajili ya shule hiyo.
Kamati hiyo ilipewa fedha za kutengeneza madawati 30 lakini madawati yaliyotengenezwa hadi sasa ni 15 tu. Pia walipewa kazi ya kutengeneza viti na makabati ambayo hayajakabidhiwa hadi leo.
“Sasa ni mwaka wa tatu bado mradi wa jengo la TASAF haujakabidhiwa, uongozi wa shule unaendelea kufuatilia mradi huo ambapo wahusika wanadai bado hawajakamilisha licha ya fedha zote za mradi kuzitumia. Naomba serikali ya wilaya iweke msukumo ili jengo hilo tukabidhiwe haraka kwa kuwa msongamo wa wanafunzi ni mkubwa, vyumba vya madarasa vilivyopo havitoshelezi,” anasisitiza mwalimu wa shule ya msingi Mkili.
Kwa mujibu wa Ntanga, tangu kuanza kwa ujenzi huo uongozi wa shule haujashirikishwa kikamilifu kuanzia ujenzi hadi mradi wa utengenezaji wa samani za shule.
Uchunguzi umebaini kuwa licha ya mradi huo wa jengo la TASAF kudaiwa kuwa umekamilika, majengo yake yapo chini ya viwango.
Hata mradi mwingine wa chumba cha darasa la tatu uliojengwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulikuwa chini ya kiwango na jengo liko katika hatari ya kubomoka kutokana na ukuta wake mmoja kuvunjika na kuweka ufa mkubwa kuanzia juu hadi chini.

Mtendaji wa kijiji cha Mkili Aratas Mwakipokile anasema ni kweli kijiji kinatumia jengo jipya la shule ya msingi Mkili kama mahabusu kwa kuwa kijiji hakina mahabusu na kwamba hata ofisi ya serikali ya kijiji inatia aibu, ni sawa na kijiji kutokuwa na ofisi.
“Baada ya serikali ya kijiji kuvunjwa, sheria ndogo ndogo za kudhibiti wananchi wanaopinga kujitolea kwa shughuli za maendeleo inakuwa ngumu kutekelezeka. Wananchi ni wabishi kushiriki kazi za kujitolea kama vile ujenzi wa shule. Kwa mfano, watu watatu kati ya 100 ndio wanaojitolea, karibu wote hawataki kujitolea,” anasema.
Kaimu mratibu wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Godfrey Kayombo amekiri TASAF kutoa shilingi milioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu na kwamba mradi huo ulitakiwa kukamilika mwaka 2009. Amesema sasa watafuatilia kujua sababu inayofanya mradi huo kutokabidhiwa hadi sasa.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Amos Mtweve ameahidi kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote ambaye atahusika kwa namna moja au nyingine amejinufaisha kupitia mradi wa jengo la shule ambao umefadhiliwa na TASAF pamoja na nguvu za wananchi.
Wakati bado kuna kitendawili juu ya jengo hilo, wanafunzi zaidi ya 75 ambao wanasoma katika chumba hicho, wapo hatarini kwani ukuta huo, wakati wowote, unaweza kuanguka. Mwalimu mkuu anaiona hatari hiyo lakini hana namna wala mahali pengine pa kuwaweka kutokana na upungufu vya vyumba vya madarasa.
Ntanga amekuwa mwalimu mkuu katika shule hiyo kwa miaka 30 sasa. Shule hiyo ina wanafunzi 421, mikondo 15 , walimu watano wakati mahitaji ni walimu 12.
Shule ya Mkili iliyoanzishwa mwaka 1977, ina vyumba vya madarasa vinane wakati mahitaji ni vyumba 14, darasa moja lina wastani wa wanafunzi 75 badala ya 40, madawati yapo 102 upungufu ni 45, nyumba za walimu zilizopo ni mbili tu kati ya mahitaji ya nyumba 12, kuna matundu sita ya vyoo wakati mahitaji ni matundu 18.
Mbali ya tatizo hilo la mgogoro wa matumizi ya jengo hilo, kikwazo kingine cha elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo na nyingine zilizoko kata ya Liwundi na Ngumbo ni mazingira.
Wakati wa masika wanafunzi wanapoteza vipindi vingi kwa kuwa mawingu yakijikusanya au mvua zikianza walimu huwaruhusu wanafunzi waondoke ili wawahi kuvuka mto Ndumbi ambao mvua zikinyesha hufurika na kuhatarisha maisha ya wanafunzi wanapovuka kwenye mto huo.
“Vipindi vingi vinapotea hasa kuanzia mwezi Januari hadi Aprili. Tulipeleka taarifa TANROAD walijenga daraja la chini ambalo lilivunjika siku ya kwanza tu baada ya ujenzi kutokana na nguvu kubwa ya mvua kwenye mto Ndumbi, hivyo wameshauriwa kujenga daraja la juu ili kumaliza tatizo hilo linaloathiri taaluma katika shule hii,’’ anasisitiza.
0766463129
albano.midelo@gmail.com
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment