Saturday, April 14, 2012

Kiongozi asiyekuwa mkweli hatufai


Na Albano Midelo
ASKOFU mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega ametahadharisha kuwa kiongozi asiyekuwa mkweli hafai kwa kuwa anapoteza sifa za kiongozi bora. 
Akihubiri kwa nyakati tofauti siku ya mkesha wa sikukuu ya Pasaka na Jumapili ya pasaka kwenye kanisa la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini hapa alisisitiza kuwa kiongozi ambaye sio mkweli hawezi kuongoza  taasisi ya aina yeyote ile iwe ya kidini au kijamii.

Kwa mujibu wa mhashamu Mtega  mafundisho na maagizo ya Yesu kristo daima yalizingatia ukweli na kwamba mafundisho hayo yanatakiwa kutumika kwa binadamu wote ulimwenguni wakiwemo wale ambao wamepewa dhamana ya kutawala.
Hata hivyo  alisema dola nyingi  zinawakandamiza watu wanyonge huku viongozi wachache wakiendelea kujipatia utajiri ambao hauwajali  kwa kushindwa kuwatimizia  mahitaji ya muhimu katika maisha ya binadamu.
“Utawala wa namna hii una mambo ya kisanii,kwa kuwa daima hauzingatii ukweli na maamuzi yake yanakuwa  hayana ukweli jambo ambalo ni kinyime na maagizo ya kristo mwenyewe’’,alisema.
Mhashamu Mtega alibainisha kuwa leo waumini wa kanisa katoliki ulimwenguni wanapoadhimisha ufufuko wa Yesu kristo wawe mstari wa mbele kwa kutoa ushuhuda  na kuheshimu sakramenti na kudumu katika maisha ya sara,kuhudhuria jumuiya ndogo ndogo na kujenga tabia ya kusoma Biblia takatifu.
Katika hatua nyingine mshamu Mtega alikemea tabia  ya baadhi ya watu wanaopotosha ukweli kuhusu kufa na kufufuka kwa Yesu kristo na kusisitiza kuwa  anayemkashifu ufufuko wa Yesu ni shetani  kwa kuwa Yesu ni Mungu kweli na alifufuka kweli.
“Kuna nabii gani  amewahi kufa na kufufuka zaidi ya mwokozi wetu Yesu Kristu?alihoji Askofu mkuu Mtega. Katika nafasi hiyo alikemea pia tabia  iliyozoeleka  ya watu waliopewa dhamana kuomba rushwa na kusisitiza kuwa tabia hiyo inawanyima haki watanzania wengi wanyonge .

albano.midelo@gmail.com

No comments:

Post a Comment