Na
Albano Midelo
TANGU
tupate uhuru,historia ya nchi yetu inaonesha kuna mambo mengi mazuri
yaliowezwa kufanywa katika utekelezaji wa sera na mipango ya elimu ya watu
wazima.
Mwaka 1968 Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa
nchi 12 ulimwenguni zilizochaguliwa na shirika la umoja wa mataifa la
Elimu,Sayansi na Utamaduni yaani UNESCO kufanya mradi wa majaribio ya kutumia
mbinu mpya ya kisomo chenye manufaa katika kufundisha watu wazima
kusoma,kuandika na kuhesabu.
Baba wa Taifa hayati mwalimu Julius
Nyerere aliutangaza mwaka 1970 kuwa mwaka wa Elimu ya watu wazima,tangazo hilo
la mkuu wa nchi wakati huo likaufanya mwaka huo kuwa mwanzo wa harakati za
kufuta ujinga nchini .
Mwaka 1974 na mwaka 1975 Tanzania
iliweza kuandikisha watu wasiojua kusoma wapatao milioni 4.5 kwenye madarasa ya
kisomo cha watu wazima na hivyo baada ya muda mfupi Tanzania ilifanikiwa kufuta
ujinga wa kutojua kusoma kutoka asilimia 69 mwaka 1970 hadi kufikia asilimia 39
mwaka 1975.
Kana kwamba haitoshi historia ya elimu
ya watu wazima inaonesha kuwa ilipofika Agosti mwaka 1975 Tanzania ilikuwa ni
nchi ya kwanza ulimwenguni kufanya mtihani wa kisomo kwa watu wazima wapatao
zaidi ya milioni 3.8 ambao walikuwa ni asilimia 77 ya wote waliokuwa
wanahudhuria kwenye madarasa ya kisomo.
Hata hivyo mwaka 1981 Tanzania ilikuwa
ni ya kwanza katika nchi za ulimwengu wa tatu kuanzisha kampeni ya kitaifa ya
kisomo cha kujiendeleza iliyohusisha watu wazima zaidi ya milioni 1.4 waliofuzu
kisomo katika hatua ya nne.
Kwa mujibu wa taarifa ya kitaifa ya
elimu ya watu wazima mnamo mwaka 1986 Tanzania ilifanikiwa kupunguza idadi ya watu wazima wasiojua kusoma hadi
kubakia zaidi ya milioni 1.36 ambao walikuwa sawa na asilimia 9.6.
Hata hivyo kutokana na kushuka kwa kwa
hali ya uchumi na baadhi ya wafadhili kusitisha misaada ya kuendeleza elimu ya
watu wazima,uwezo wa taifa uliyumba
kutekeleza mipango ya elimu ya watu wazima baada ya programu hiyo kukosa
mafungu ya fedha,vifaa na nyenzo muhimu za uendeshaji.
Ingawa hivi sasa juhudi zimeanza upya
na mipango thabiti imeandaliwa kufufua upya kisomo cha kujiendeleza,uchunguzi
umebaini kuwa taifa letu limo katika tatizo kubwa la ujinga wa kutojua kusoma
na kuandika kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania.
Kwa mujibu wa matokeo ya sensa
iliyofanyika mwaka 2002 na matokeo ya tafiti mbalimbali,inakadiriwa kuna watu wazima milioni 5.5 sawa na asilimia 32 ambao hawajui
kusoma,kuandika na kuhesabu.
Tafiti hizo zinaonesha kuwa hivi sasa
hatukabiliwi na tatizo la watu wazima wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu
pekee bali pia kuna idadi kubwa ya vijana wa miaka kati ya 11 na 18 ambao ama
hawakuandikishwa shuleni au wameacha shule hivyo hawajui kusoma, kuandika na
kuhesabu.
Kundi hili la vijana ni nguvukazi
kubwa ya Taifa ambao wangeweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya
kijamii na kiuchumi ,hata hivyo kutokana na kutojua kusoma,kuandika na kuhesabu
vijana hao hawatatoa mchango wowote wa maana iwapo taifa litawaacha kuendelea
kubakia katika hali ya ujinga.
Wataalamu uhusisha elimu hafifu na
umasikini,upeo mkubwa wa elimu na utajiri.uchunguzi umebaini kuwa sehemu ambazo
idadi kubwa ya watu wana elimu ndogo kiwango cha umasikini ni kikubwa na maeneo
ambayo wananchi wengi wana elimu ya kutosha huwa na maendeleo mazuri.
Serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya
ufundi inasisitiza na kuwahimiza wananchi kutokomeza tatizo la kutojua
kusoma,kuandika na kuhesabu ili kuwaondoa katika hali duni inayotokana na
ujinga na kuwawezesha kwenda katika hali nzuri zaidi ili kujikomboa kimaisha.
Huwezi kujinasua katika wimbi la
umaskini bila kupata elimu bora hivyo njia pekee ya kujinasua katika tatizo la
kukosa elimu ni kwa mtu yeyote mwenye
tatizo hilo kuamua kujiunga na darasa la kisomo cha watu wazima katika shule za
msingi .
Licha ya wimbi kubwa la watanzania
kutojua kusoma,kuhesabu na kuandika bado wananchi wanajua kusoma,kuandika na
kuhesabu wana mambo mengi wasiyoyajua
ambayo ni muhimu kwa maisha yao ambayo wanapaswa kujifunza katika madarasa ya
kisomo cha elimu ya watu wazima kutokana na ukweli kuwa elimu ni bahari na
kuishi ni kujifunza.
Hivi sasa dunia imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya
sayansi na teknolojia,ni wale tu ambao wana elimu ndio watakaoweza kufaidi
matunda ya sayansi na teknolojia na wale ambao hawana elimu watabakia kuwa
watazamaji tu hivyo basi kundi kubwa ambalo halijui kusoma,kuandika na kuhesabu
lililopo hapa nchini lina kila sababu ya kujikomboa kutoka katika hali hiyo ili
hatimaye waweze kufaidi matunda ya kuwa na elimu katika ulimwengu huu wa
utandawazi.albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129
No comments:
Post a Comment