Monday, April 23, 2012

Mamia wajitokeza ushuhuda wa Sr.Bernadeta


Na Albano Midelo,
WATU 130 wakiwemo wa madhehebu mbalimbali wamejiandikisha kwenye kamati ya mchakato wa  Sista Bernadeta Mbawala kwa ajili ya kutoa ushuhuda wao namna walivyotendewa na  mtumishi huyo wa Mungu katika maisha yao.
Akihubiri katika kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba la mjini hapa Jumapili wiki hii paroko wa parokia ya Songea padre Ananias Mbawala alisema kamati ya mchakato bado inaendelea kupokea majina ya watu ambao watatoa ushuhuda katika maisha yao uliotokana na  maombezi ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta.

Kwa mujibu wa paroko hao wata watatoa ushuhuda wao katika mambo mbalimbali baada ya kusali na kufanya maombezi kutumia kupitia mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala na kufanikiwa katika maisha.
“Baadhi ya matatizo ambayo wamefanikiwa ni pamoja na wale ambao walishindwa kupata watoto kwenye ndoa zao kwa muda mrefu wamefanikiwa kuwa na watoto,wengine wamefanikiwa kwenye masomo yao,kupata ajira na wazazi wengine watoto wao ambao walikuwa na tabia mbovu sasa wamekuwa watoto wenye maadili na kuwa mfano bora katika jamii na wengine wamepona magonjwa sugu yaliokuwa yanawasumbua kwa miaka mingi’’alisisitiza.
Paroko huyo alibainisha zaidi kuwa katika kipindi hiki cha  sikukuu ya pasaka ambayo waamini wa kanisa katoliki wanaadhimisha ufufuko wa Yesu Kristo ni  vema waumini wakasherehekea sikukuu hii kwa kuonyesha ushuhuda katika maisha yao na kusisitiza kuwa  injili inaendana na ushuhuda.
Katika hatua injini wakati mchakato wa kumtangaza Sr.Bernadeta kuwa mwenyeheri na hatimaye mtakatifu kuanzia wiki ijayo ujenzi utaanza wa eneo la kuweka masalia ya mtumishi huyo wa Mungu  ndani ya kanisa kuu la kiaskofu la Songea.
Paroko wa parokia ya Songea padre Mbawala alisema eneo ya ujenzi  wa kuweka masalia hayo tayari limeandaliwa na kwamba hivi sasa waumini wanahamasishwa kuchangia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
Uzinduzi wa mchakato wa kumtangaza  Sista Bernadeta Mbawala kuwa Mwenyeheri ulizinduliwa rasmi  na Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega katika kanisa kuu la kiaskofu la mjini Songea mapema mwaka huu.
 Makao makuu ya kanisa katoliki Vatican  hivi karibuni yametoa ruhusa kwa jimbo kuu katoliki la Songea kuanza mchakato wa utafiti  kuhusu maisha,fadhila za uhodari,sifa ya utakatifu na nguvu za kimaombezi za Sista Bernadeta Mbawala ili aweze kutangazwa kuwa mwenyeheri na hatimaye mtakatifu.
Sista Bernadeta aliyezaliwa Oktoba 27,1911 katika kijiji cha Likuyufusi wilayani Songea mkoani  Ruvuma alifariki Novemba 29,1950 na kuzikwa  katika makaburi ya Abasia ya Peramiho yaliopo kilometa 24 kutoka mjini Songea
albano.midelo@gmail.com

No comments:

Post a Comment