Thursday, April 26, 2012

Mwekezaji anapotukuzwa mwananchi kutupwa nje



Na Albano Midelo
WAKAZI wa kijiji cha Lipokela wilayani Songea mkoani Ruvuma  wanamuomba waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi  Profesa Anna Tibaijuka kuwasaidia kuirejea ardhi yao eneo la Luchili  yenye  ekari 4000  inayodaiwa kupewa mwekezaji.
Wakizungumza na mwandishi wa habari katika kijiji hicho baadhi ya wananchi walidai kuwa  mwekezaji mwenye asili ya Asia   Khalim Meraly  tangu mwaka 1985 alipewa ardhi kinyemela bila Baraka za wananchi na kusababisha ardhi hiyo kuingia kwenye mgogoro mkubwa.
Wananchi  wamedai kuwa mwekezaji huyo aliyewekeza katika kilimo alipewa  ardhi hiyo katika mazingira ya kutatanisha kupitia aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho  Joseph Komba pamoja na aliyekuwa katibu wake Gervas Mbonde .
Hata hivyo walikiri kuwa mwekezaji huyo alipewa ardhi  kwa maamuzi ya wananchi yenye ukubwa wa eka 1000 tu mwaka 1984 na kwamba mwaka 1985 aliomba tena ardhi eka zaidi ya 4000 ambazo alipewa bila Baraka za wananchi na kuleta mgogoro ambao unaendelea hadi sasa.
``Kuanzia mwaka 1985 wananchi wa kijiji cha Lipokela hawakujua kama ardhi yao ya ekari 4000 amepewa mwekezaji hadi mwaka jana  takriban miaka 25 ndipo ilipofahamika na kusababisha wananchi zaidi ya 200 wanaolima mashamba pamoja na makazi kwenye  eneo hilo  kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mwekezaji ’’,walidai wananchi hao.
  Akizungumza kwa niaba ya wenzao mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Faustine Komba alibainisha  kuwa ardhi hiyo yenye  mgogoro ilianza kutumika na wananchi kuanzia mwaka 1993 ambao walipimiwa kihalali na uongozi wa kijiji na kuendelea kuitumia mwaka hadi mwaka bila kutambua kuwa amepewa mwekezaji kinyemela.
 Komba alisema mwekezaji alipewa kisheria eka  1000 tu upande wa kulia mwa barabara ya Songea - Mbinga na kwamba eneo lenye ekari zaidi ya 4000 upande wa kushoto ambazo mwekezaji huyo anadai kupewa sio zake kwa kuwa ni mali ya wananchi ambazo walipewa kihalali na serikali ya kijiji.
Wananchi  wakiwemo  Gofrey Lupindu,Agustino Komba,Filbert Kinunda, Vestina Hyera, Bomba Nchimbi wakizungumza kwa uchungu ,wanadai msimu huu hawana mashamba ya kulima baada ya kuzuiwa kuendelea kulima katika mashamba yao na kwamba hivi sasa hawana imani na mwenyekiti wa kijiji aliyopo madarakani John Nchimbi ambaye anadaiwa kumsaidia mwekezaji badala ya kuwasaidia wananchi waliomweka madarakani.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Nchimbi amekanusha kumsaidia mwekezaji bali  amesema amepewa ekari hizo  chini ya mihutasari halali ambayo walikaa viongozi waliomtangulia na kusisitiza kuwa viongozi waliomtangulia ndiyo wenye makosa kwa kuwa waliendelea kuwagawia wananchi mashamba wakitambua kuwa eneo hilo ni mali halali ya mwekezaji.
“Wenyeviti wa serikali za vijiji waliotapeli wananchi ardhi  wakiwa madarakani Faustine Komba, Regnad Komba,John Lupindu,Anton Komba na Joseph Komba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa kijiji cha Lipokela ndiye aliyeidhinisha wakati Meraly anapewa ardhi’’,anadai Nchimbi.
Muhtasari wa kwanza unaonesha kuwa  Mei 10,1984 ulifanyika mkutano wa kijiji wenye wajumbe 25 waliokubali ombi la mwekezaji Meraly  kupewa ekari 1000 na muhtasari wa pili unaonesha kuwa ulifanyika mkutano wa Halmashauri ya kijiji cha Lipokela Marchi 26,1985 wenye wajumbe 24 ambao walikubali  maombi ya nyongeza ya ekari 4000 kwa mwekezaji ili kufikia ekari 5000 ambazo ndiyo mahitaji yake .
Hata hivyo afisa mtendaji wa kijiji cha Lipokela Sabinus Nyoni   Oktoba 17 mwaka jana aliwaandikia barua yenye kumb.Nolvc/ARDH wanakijiji wapatao 200 wanaoishi katika eneo la Luchiri  kusimamisha kufanya shughuli za kilimo katika eneo la Luchiri ambako anadai ni eneo la mwekezaji Meraly ambaye anatumia jina la Southern Farm Ltd.
Katika barua hiyo Nyoni aliwakumbusha wakulima hao kuwa eneo hilo ni mali ya Southern Farm Ltd na kwamba lina hatimiliki ya kisheria yenye shamba namba 40 na kwamba kwa  serikali itamtuma mtaalam wa kuthamini shughuli zilizofanyika kwa miaka 23 ili wananchi wapate fidia.
“Endapo mwananchi yeyote atakiuka na kuendelea kufanya kazi kwenye eneo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuwa atakuwa ni mvamizi wa eneo la Southern Farm Ltd na atakuwa amekosa fidia ambayo alistahili kupata’’,anasisitiza Nyoni katika barua yake ambayo nakala amepewa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea.
Kwa upande wao wakazi wa eneo hilo baada ya kupata barua ya afisa mtendaji walijibu barua hiyo kwa kupinga amri ya kusimama kufanyakazi za kilimo katika eneo hilo kwa madai ya kutotambua uhalali wa kupata eneo ambalo wao wamelitumia kwa zaidi ya miaka 18 na kwamba eneo hilo wamepewa na kijiji kisheria tangu mwaka 1993.
“Eneo hili hatukuvamia,tulipewa kwa kutekeleza hatua zote za maombi katika serikali ya kijiji,tulipewa kwa kujadiliwa na kupimiwa,wananchi tunatambua suala hili lipo ngazi za juu, tumeshindwa kulima hadi sasa hatujui familia zetu mwaka huu tutaishi vipi bila kuwa na chakula’’,wanadai wananchi hao.
Juma Thomas ni wakili wa kujitegemea anasema sheria inasema mtu akitumia ardhi ambayo sio mali yake kwa miaka zaidi ya 12 ,mtumiaji ana haki ya kumilikishwa hivyo kwa kuwa wananchi hao wametumia ardhi hiyo kwa miaka 18 wana haki ya kumilikishwa kisheria.
Mwekezaji  wa Southern Farm Company  ana hati ya kumiliki eneo hilo shamba namba 40 iliyotolewa Februari 25,1988,lakini nao wananchi  wanazo hati na risiti ambazo wamelipia katika serikali ya kijiji cha Lipokela kuanzia mwaka 1993 hadi wanapoambiwa kuwa eneo ni la mwekezaji.
Mwekezaji Bwana Meraly kwa upande wake kuanzia msimu huu tayari ameanza kuendeleza  shamba lake ekari 1000 kwa kuanzisha shamba kubwa la kahawa ambalo amepanda  miche laki tano ya kahawa.
Meneja wa shamba hilo Ally Said akizungumza kwa niaba ya mwekezaji wa Southern Farm anasema shamba hilo litatoa ajira kwa watu 6000  na kwamba tayari watanzania  600 wamepata ajira kwenye shamba hilo.
“Mwekezaji amepania kufanya mapinduzi ya kilimo cha kahawa  anawatumia wataalamu wa kilimo cha umwagiliaji wa matone kutoka nchini Israel na Somalia  lengo likiwa ni kuwekeza kwa miaka 100’’,anasisitiza.
Afisa wa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Japhet Mungashwa amekiri kwamba  mwekezaji huyo amemilikishwa eneo la eka 5000 kihalali kwa kipindi cha miaka 99 kwa sheria ya ardhi ya mwaka 1923 ambayo inawaruhusu wajumbe wa kijiji kupitisha maamuzi bila kushirikisha maamuzi ya wananchi wote kama ilivyo katika sheria mpya ya ardhi ya mwaka 1999.
Sheria ya ardhi ya vijiji  namba tano kifungu cha tano ya mwaka 1999 inasema kuwa Halmashauri ya kijiji haitagawa ardhi au kutoa hakimiliki ya kimila bila ya kwanza kupata idhini ya mkutano  wa kijiji ambapo katika kifungu cha sita katika sheria hiyo kinaeleza  Halmashauri ya kijiji italazimika kutoa taarifa na kuzingatia maoni ya mkutano wa kijiji kuhusu uendeshaji na usimamizi wa ardhi ya kijiji.

No comments:

Post a Comment