Thursday, April 26, 2012

Uvuvi haramu unamaliza samaki ziwa Nyasa


  

Na Albano Midelo

  Takwimu zinaonesha uvuvi usiokuwa endelevu unaofanywa kwenye ziwa Victoria umesababisha kutoweka kwa aina 300 za samaki waliokuwa wanapatikana mwanzoni mwa miaka ya 1960 hadi 1970.

Uvuvi usiokuwa endelevu unafanyika pia katika ziwa Nyasa pamoja na uchafuzi wa mito inayoingia kwenye ziwa hilo na kusababisha samaki waliokuwepo katika ziwa hilo kuendelea kutoweka na kwamba endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa na wadau hususani wizara ya maliasili na utalii kuna hatari samaki wa aina mbalimbali wakatoweka.


Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbuji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500 toka usawa wa bahari ambapo kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750,urefu wake ni karibu  kilometa 1000 na upana mkubwa ni kilometa 80 ambapo upana mdogo ni kilometa 15.


Kutoweka kwa baadhi ya samaki katika ziwa Nyasa kumesababisha baadhi ya samaki kutopatikana kwa urahisi hali ambayo imesababisha bei za samaki wanaovuliwa katika ziwa hilo kuuzwa kwa bei mbaya na hivyo wananchi wengi kushindwa kumudu kununua kitoweo hicho.

Ukitembelea kwenye mapitio  ya mto Ruhuhu ambao unamwaga maji yake ziwa Nyasa utabaini uvuvi ambao hauruhusiwi kisheria ukiendelea kufanya jambo ambalo watalaamu wanasema kumechangia kutoweka kwa samaki kwenye mto Ruhuhu na ziwa Nyasa.

Mto Ruhuhu umechafuliwa na maji yake yanaonekana kuwa na tope kwa mwaka mzima kutokana na shughuli za kilimo na uchimbaji wa madini ambao ufanywa na wakazi ambao wanaishi kando kando mwa mto huo unaoanzia kwenye milima ya Matogoro wilayani Songea.
  
 Mtendaji wa kata ya Lituhi wilayani Nyasa Joseph Chawala anasema hadi kufikia miaka ya 2000 maji ya mto Ruhuhu yalikuwa hayajachafuliwa ambapo samaki wa aina mbalimbali hasa mbasa na mbelele walipatikana kwa wingi lakini hivi sasa samaki wametoweka na mto ni mchafu kwa mwaka mzima.

Anabainisha zaidi kuwa kilimo na usafishaji wa udongo wa madini aina ya dhahabu  kwa kutumia zebaki kumechangia kuharibu mazialia ya samaki na hata samaki kuhama kwa kuwa maji ya mto huo hivi sasa radha yake imebadilika na yanatoa harufu mbaya kwa viumbe hai kama samaki.

“Hivi sasa wavuvi wanaweza kukesha kwenye mto Ruhuhu na wasiambulie samaki hata mmoja hali ni mbaya,jambo la hatari zaidi ni kwamba wavuvi wanavua kwenye maingilio ya mto Ruhuhu na ziwa Nyasa sehemu ambayo  kisheria hairuhusiwi kufanya uvuvui kwa kuwa ni mazalio ya samaki hivyo wanaharibu mazalia ya samaki’’,anasisitiza.
   
Chawala anabainisha kuwa  uchafuzi huo wa mto Ruhuhu umeleta athari kubwa kwa wakazi wa kata ya Lituhi yenye vijiji vya Lituhi, Ngingama, Nkaya,Litumbakuhamba,Kihuru na Mwelampya ambapo zaidi ya watu 12,000 wanaathirika na hali hiyo kwa kuwa wanaishi kwa kutegemea uvuvi.

John Mpangala  mkazi wa Liuli anasema kwa miaka mingi walizoea kupata samaki aina ya mbasa na mbelele kutoka mto Ruhuhu lakini hivi sasa hakuna samaki wa aina hiyo na kusisitiza kuwa  watu wa mwambao wamezoea kula samaki kwa ugali wa mhogo hivyo kutokana na kupungua kwa samaki inawawia vigumu kupata kitoweo.

Mvuvi Martin Challe wa kijiji cha Lituhi anadai miaka ya nyuma samaki katika mto Ruhuhu na ziwa Nyasa  walikuwa wanapatikana kirahisi tofauti kubwa na hali ya hivi sasa ambapo wavuvi wanakesha usiku kucha hadi asubuhi na kuambulia samaki wachache sana au wakati mwingine wanakosa kabisa samaki.

 “Bei ya samaki aina ya mbasa,kambale,mbelele na ngumbo haikamatiki kutokana na kuuzwa samaki mmoja kati 10,000 hadi 15,000,kwa kweli aina hizo za samaki wanaoweza kula ni watu wenye uwezo tu hivyo kufanya maisha katika mwambao mwa ziwa Nyasa kuwa magumu’,alisisitiza Mary Haule mkazi wa Lituhi.

“Huku mwambao mwa ziwa Nyasa hakuna mifugo mingi kama ilivyo katika maeneo mengine nchini,sisi tegemeo letu kubwa ni samaki wa ziwa Nyasa hivyo hali hii ya kutoweka kwa samaki au samaki kupatikana kwa msimu ni balaa”,anasisitiza Victor Komba mkazi wa Liuli.

Komba anabainisha zaidi kuwa ziwa Nyasa linapochafuka huwa kunakuwa na dhoruba kali na hivyo kuhatarisha maisha ya wavuvi ambapo baadhi yao hupoteza maisha kutokana na kushindwa kujiokoa baada ya kutumia vifaa duni.

Stephano Vumu mfanyabiashara wa samaki wa Liuli anadai amewahi kwenda nchini Malawi  kujionea uvuvi wa samaki anadai kuwa kuna samaki wengi kwa sababu wananchi wa Malawi wanatengeneza vyakula viwandani na kuwalisha samaki hao jambo ambalo linafanya waendelee kuzaana kwa wingi.

Hata hivyo anadai kutokana na kutoweka kwa samaki ziwa Nyasa upande wa Tanzania hivi sasa wavuvi na wachuuzi wa samaki wamekimbilia upande wa Malawi wakidai upande huo kuna samaki wengi kuliko hapa nchini .

Anasisitiza kuwa nchini Malawi wamekuwa wakitumia vifaa vya kisasa kuvua samaki pamoja na kupiga marufuku uvuvi haramu ambao umekuwa ukiendelea kufanyika upande wa Tanzania hasa kutokana na wavuvi kutumia vifaa duni na ambavyo haviruhusiwi kisheria.

“Natoa wito kwa wadau wa uvuvi kuliangalia ziwa Nyasa na mito inayoingiza maji ziwa Nyasa ukiwemo mto Ruhuhu ili kuboresha uvuvi katika ziwa Nyasa ili sekta hiyo iweze kuwa endelevu na kuwafanya wananchi wa mwambao mwa ziwa Nyasa kuendeleza uchumi wao na kuachana uvuvi ambao haukubaliki”,anasema.

Barnabas Ruhumbi aliyekuwa afisa tarafa ya Ruwekei mwambao mwa ziwa Nyasa anasema takwimu zinaonesha kuwa mavuno ya samaki katika bandari ya Mbambabay ni chini ya tani   100  kwa mwaka mavuno ambayo ni kidogo mno ukilinganisha na idadi ya samaki waliopo katika ziwa hilo.

Kwa upande wake mbunge wa Mbinga magharibi Kapten John Komba anasema  sekta ya uvuvi bado ina nafasi kubwa ya kuwaendeleza  wananchi wa mwambao wa ziwa Nyasa ambao kwa kiwango kikubwa wanategemea uvuvi katika maisha yao.

Komba anasema hivi sasa amekusudia kuvalia njuga changamoto zote ambazo zinakabili sekta ya uvuvi katika ziwa Nyasa ikwemo kuweka mikakati ya kupata vifaa vya kisasa vya uvuvi sanjari na kupiga vita uvuvi haramu ambao unasababisha kutoweka kwa aina mbalimbali za samaki zilizokuwepo miaka ya nyuma.

Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na jumuiya ya nchi zilizo kusini mwa Afrika(SADC) kwa kushirikiana na  nchi ya Uingereza kwenye ziwa Nyasa,ulionesha kuwa ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki na kati ya kiasi hicho tani 35,000 za samaki ni jamii ya samaki wa maji ya juu ambao wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka.

Hata hivyo ofisa wa maliasili na uvuvi katika wilaya ya Mbinga Peter Mdaki anasema kuna uwezekano wa kuongeza mapato ya uvuvi katika ziwa Nyasa hadi kufikia tani 81,000 iwapo njia  za uvuvi zitaboreshwa.

Anabainisha kuwa uvuvi ambao unaendeshwa katika ziwa Nyasa ni ule ambao unafanyika katika maeneo yenye maji mafupi umbali usiozidi kilometa mbili kutoka ufukweni kwa kutumia mitumbwi ya kuchongwa.

“Wavuvi katika maeneo hayo wamekuwa wakiendesha uvuvi  usio kuwa endelevu kwa kutumia makokoro wanayoyatega ziwani kwa kutumia nyavu zenye macho chini ya inchi tatu na kutega nyavu hizo kukinga mto Ruhuhu hivyo kuharibu mazalia ya samaki nawaomba wananchi waachane na  uvuvi huu ambao pia sio endelevu”,alisisitiza.

Mdaki anabainisha kuwa uvuvi huo haramu umesababisha samaki aina ya mbasa na  mbelele kuelekea kutoweka hali ambayo inadidimiza uchumi wa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambao wanategemea uvuvi kuendesha maisha yao.

Amesisitiza kuwa uvuvi ambao unafanywa ufukweni mwa ziwa hilo kwa kutumia  nyavu za kokoro,vyandarua vya kuzamia na kutega nyavu ambazo zina macho chini ya inchi tatu sio uvuvi endelevu kwa kuwa zinaharibu mazalia ya samaki na kuua samaki wenye umri mdogo.

Anasema pamoja na elimu kutolewa mara kwa mara kwa wananchi kuhusu kuepukana na uvuvi usiokuwa endelevu,bado wananchi mwambao mwa ziwa hilo wanaendelea na uvuvi haramu hali ambayo inaharibu mazalio ya samaki na kusababisha aina mbalimbali za samaki kuanza kutoweka  kwa kasi.

 Uchunguzi umebaini kuwa wavuvi wanaokamatawa kwa kuendesha uvuvi usiokuwa endelevu wamekuwa wakimudu kulipa faini ambazo zinatozwa na serikali  kupitia mahakama  na kuonekana kuwa na hatia hali ambayo inafanya wavuvi hao  kuendeleza aina hiyo ya uvuvi licha ya kupigwa marufuku na kisheria.

Baadhi ya mambo ambayo yanaendeleza uvuvi usiokuwa endelevu  kuwa ni pamoja na utoaji wa rushwa kwa maofisa uvuvi wasiokuwa waaminifu hivyo kuruhusu wavuvi haramu kuendelea kulihujumu taifa hali ambayo inaangamiza mazalio ya samaki na kuhatarisha samaki kutoweka.

Uvuvi haramu unaathiri kizazi cha sasa na kijacho hivyo inatakiwa watu wote ambao wanaendesha uvuvi haramu kufichuliwa ikiwa ni pamoja na watumishi wa maliasli na utalii ambao wanashikiliana na wavuvi haramu haona hivyo kuokoa maisha ya samaki ambao wataendelea kuzaana kwa wingi na hivyo kuboresha maisha ya wavuvi na taifa kwa ujumla wake.





                      
























1 comment:

  1. Duh! itakuwa tatizo kubwa sana kwa kweli kwa sisi wanyasa tunakula samaji tu....

    ReplyDelete